Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. PROF. SOSPETER M. MUHONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Naomba niwashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba hii bajeti tuipitishe kwa sababu nina miradi mingi huko Musoma Vijijini inasubiri fedha ikiwemo barabara yangu ya lami inasubiri fedha na mradi mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji na wenyewe unasubiri fedha. Kitu cha pili ni lazima tuiunge mkono Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita sana kwenye uchumi. Uchumi wetu unakua kwa taratibu sana, sasa nitajaribu kueleza nini tufanye ili uchumi wetu uende kwa kasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uchumi unakua kati ya kiwango cha asilimia 5.1 mpaka 5.5. Kipimo kingine cha ukuaji mdogo wa uchumi wetu ni, sijui Kiswahili chake HDI (Human Development Index) hii ndiyo inachukua kila kitu, mambo ya afya, elimu na kila kitu, Tanzania hatujafanya vizuri hapo. HDI index yetu ya mwaka 2022 ni 0.532, hii inatufanya tunakuwa nchi ya 167 kati ya nchi 193, ukilinganisha na Seychelles ambayo HDI yake ni 0.802, inakuwa ni nchi ya 67 duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo letu tulijiwekea kwenye mpango wetu wa maendeleo tufikie GDP per capital ya dola 3,000 na uchumi unapaswa kukua kwa asilimia nane mpaka 10%, lakini uko chini ya hapo. Ili twende mbele ni lazima tuangalie historia ya ukuaji wa uchumi wetu, nimechukua hapa takwimu kidogo ambazo zinajenga hoja ya kuharakisha ukuaji wa uchumi. Mwaka 1960, tulikuwa Watanganyika milioni 10, thamani ya dola kwa shilingi ilikuwa dola moja ilikuwa shilingi saba. Miaka 20 baadaye 1980, tulikuwa watu milioni 19, dola moja ilikuwa sawa na shilingi nane za Tanzania. Maana yake ni nini? Kwa miaka hiyo 20, Watanzania wameongezeka kwa 90%, lakini thamani yetu ya dola ongezeko lake lilikuwa karibu 14%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mwaka 2000, Watanzania tulikuwa milioni 34 na mwaka 2020 miaka 20 baadaye, tulikuwa watu milioni 62 lakini mwaka 2000 dola moja ilikuwa sawasawa na shilingi 800 za Tanzania na mwaka 2020 dola moja ilikuwa sawasawa na shilingi 2,320 za Tanzania. Maana yake ni nini? Ni kwamba, kwa hiyo miaka 20 Watanzania tumeongezeka kwa 82% lakini thamani yetu ya dola imepungua na imekuwa kiwango cha zaidi ya 190%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa hali kama hiyo lazima tukubali kwamba uchumi wetu haujaenda kasi na nimechukua mifano, kila siku tunasema tuchukue nchi ambazo tulifanana miaka ya 1950 na 1960. Hapo nachukua India na China siyo nchi nyingi zaidi, kwa leo hii mwaka 2024 nchi tano tajiri kabisa duniani, Nchi ya ya kwanza ni USA, Nchi ya pili ni China. Kwa hiyo, China tuliyokuwa nayo sawa sawa miaka ya 1960, mwaka 2024 tayari imekuwa ya pili kwa ubora na kwa utajiri duniani na Nchi ya tatu ni Ujerumani, Nchi ya nne ni Japan na Nchi ya tano ambayo tulikuwa nao sawa sawa miaka ya 1950 na 1960, leo hii GDP ya India ni trilioni 3.9.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatayarisha dira ya maendeleo ya mwaka 2050, angalia nchi tano tajiri tukifika mwaka 2050. Nchi ya kwanza itakuwa ni China, itakuwa tayari imeitoa Marekani na itakuwa na GDP ya trilioni 58. Pili itakuwa ni US, Nchi ya tatu itakuwa India itakuwa na trilioni 22, Nchi ya nne itakuwa Indonesia na Nchi ya tano ni Ujerumani. Kwa hiyo, tunavyotengeneza dira yetu ya maendeleo ni lazima tuwekee hivi vitu maanani kwa nini wenzetu wametoka nyuma na leo hii wanaongoza dunia kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali letu kubwa, ili uchumi ukue kati ya asilimia nane na 10% tunapaswa tufanyaje? Kitu cha kwanza kabisa ni nchi hizo zenye mafanikio ni kwamba elimu yake ni bora kweli kweli. Maana yake ni kwamba, sijui nitaliwekaje kwa Kiingereza, ni quality education and train at all levels. Hicho ndiyo kitu cha kwanza kwa nchi zilizofanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ni lazima ipatikane nishati ya uhakika na ya bei nafuu. Ukweli ni kwamba tulipiga mahesabu tukitaka kuwa nchi ya kipato cha kati, lazima tupate megawatts 10,000. Naomba tena hili nilisisitize ndugu zangu, umeme lazima tufike megawatts 10,000 kama tunataka kuwa nchi inayoendelea kwa haraka sana. Kwa zaidi ya miaka kumi vyanzo vya umeme ambavyo duniani vimezalishwa kwa wingi cha kwanza ni solar, cha pili ni upepo. Kwa hiyo, nadhani energy mix yetu tutaiweka vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha tatu ni lazima tuwe na bidhaa bora na nyingi za kupeleka kwenye soko la dunia, walengwa hapa ni wananchi wa dunia hii. Sasa hivi tuko bilioni nane, lakini 2025 ambapo tunatengeneza dira tutakuwa watu karibu bilioni 10. Sasa nini tupeleke sokoni huko na nini kifanye uchumi wetu uende kwa kasi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha kwanza ni kilimo cha umwagiliaji, hapa tutafute mazao au bidhaa ambayo inatumiwa na watu wengi duniani. Kwanza ni mchele ambao unatumiwa karibu na nusu ya dunia na uzalishaji kwa sasa ni tani milioni 524. Je, sisi hapo tunachangia kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ni ngano. Theluthi moja ya watu wa duniani wanatumia ngano kama chakula kikuu, uzalishaji ni tani milioni 785, lazima tuchangie huko. Viazi mviringo sasa hivi kimekuwa chakula cha tatu duniani na wanazalisha tani milioni tatu kwa mwaka na sisi tuzalishe. Baadaye mazao mengine ni mahindi, mihogo, maharage, soya beans, korosho na matunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ni ufugaji na uvuvi. Lazima tuwekeze huko kweli kweli, yaani hapa tuuze nyama, maziwa na samaki. Kwa mfano, sasa hivi uzalishaji wa maziwa duniani ni tani milioni 930. Je, sisi tunachangia kiasi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha tatu kitakachofanya uchumi wetu ukue kwa kasi ni madini, lakini tusibaki na madini tuliyoyazoea kila siku. Tuwasaidie wachimbaji wadogo lakini lazima tutafute uwekezaji mkubwa kabisa hasa kwenye hizi critical minerals, madini ambayo ni muhimu kabisa duniani yanayohitajika kwenye nishati, kwenye mambo yanayohusu vifaa vya ulinzi pamoja na mambo ya teknolojia ya sasa, soko hilo sasa hivi la critical minerals ni la dola bilioni 320 na litaongezeka mara mbili ikifika mwaka 2080, litaongezeka mara nne ikifika mwaka 2050. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho kitakuza uchumi wetu, ni natural gas na helium. Natural gas tunazo zaidi ya TCF 57 trilioni hatujazifanyia kazi. Majadiliano ya LNG kama walivyoongea wengine lazima yaende kasi. Msumbiji waliokuwa nyuma yetu wameanza kuzalisha na kusafirisha LNG na wanaweka plant ya pili na plant ya tatu ya total energies itakayokuwa inasafirisha tani milioni 43 itaanza kazi mwakani. Helium ambayo inapatikana huko Rukwa, Lake Eyasi mpaka saizi tunakisia kuwa na kama bilioni 150 cubic feet, hatujafanyia chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kitakachotuongezea mapato ni utalii. Tunafanya vizuri lakini tuendelee. Angalia Morocco mwaka jana walikuwa na wageni milioni 14.5, Egypt walikuwa na wageni milioni 15, sisi tulikuwa na milioni 1.8. Lazima tujiongeze uchumi ukue kwa kasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha mwisho kwa ruhusa yako, dunia ya sasa hivi inapokea fedha kutoka nchi zingine yaani kuna labour export na remittance. Tutafute hizi Dola zinazopungua lazima vijana wetu wawe na sifa za kufanya kazi popote duniani ili walete fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naangalia hapa, India mwaka jana wameingiza bilioni 125, China bilioni 50, Nigeria bilioni 21, Egypt bilioni 24 na mahesabu ni kwamba kufika mwaka 2030 tutakuwa na upungufu wa wataalam milioni 80 duniani, tulenge hapo
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho la kustawisha uchumi wetu na uchumi kukua ni kuwa na gold reserve. Lazima tuwe na dhahabu Benki Kuu.China ambao wanachukua dhahabu yetu, sasa hivi wana tani 2,265, India wanaochukua dhahabu yetu wana tani 822 kwenye benki yao lakini sisi Tanzania bado tuna kilo 418. Naomba tujitahidi uchumi ukue kwa kasi. Ahsante. (Makofi)