Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, nimesoma hotuba yake anataka kuleta mabadiliko ya sheria ya sukari. Mimi ni mfanyabiashara na ninauza sukari. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na ningependa kuwashauri Waheshimiwa Wabunge wenzangu, sisi kama nchi hakuna tatizo kubadilisha sheria na ndiyo kazi ya Bunge. Suala la sukari ni suala kubwa sana na limekuwa na kelele nyingi sana karibu kila mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka mwaka 2019 wakati Mheshimiwa Waziri wa Kilimo akiwa Tizeba na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara nadhani alikuwa Mwijage, wao walitoa sukari kwenye ma-godown kwa kutumia ma-SMG. Sasa nashauri sana, tunapoona kama suala hili linawakera wananchi na ni tatizo, ni vizuri tukabadilisha sheria ili haya masuala yakakaa vizuri na watu wakaacha kukaa kwenye tension.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichopita hapa mimi ni mfanyabiashara wa sukari pia na ninaishi Mwanza. Ninataka kuzungumza tu kuhusiana na suala dogo la cartel. Kwa wale wanaotoka Kanda ya Ziwa sukari ilikuwa inauzwa kwa mtu mmoja tu. Ni kweli baadhi ya viwanda wanasema wana ma-agent lakini ni ma-agent bosheni, hawana sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Kanda ya Ziwa (mimi nakaa Mwanza mjini katikati ya mji) watu walianza kwenda kupanga foleni saa 9.00 usiku na huyo aliyetajwa hapa VH-SHAH ambaye ndiye alikuwa agent mkubwa alikuwa na sukari imejaa kwenye ma-godown. Tunaona anashusha meli kila siku kutoka Kagera, lakini ili uuziwe sukari labda mifuko 50 inabidi ununue na toilet paper lazima ununue toilet paper au ununue biskuti. Sasa hii nchi ya wastaarabu hatuwezi kuwa na design hiyo ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri zibadilishwe Sheria. Tumechoka kuona kila mwaka ukifika mwezi wa Januari, Februari na Machi tunaanza kupiga kelele ya sukari humu ndani haiwezekani. Misamaha inatolewa lakini matatizo ni yale yale, haiwezekani! Ukienda Zambia mpakani sukari inauzwa rahisi, ukienda Mutukula inauzwa rahisi. Sisi kwetu kila mwaka ikifika wa Januari, Februari na Machi kelele inaanza humu ndani Bungeni na wananchi wetu. Ninataka kusema ukweli, mimi natoka Jimbo la Geita Vijijini, wananchi wangu wa Izumacheli walinunua sukari shilingi 11,000 acha kusema 10,000 na ushahidi ninao. Sasa hatuwezi kuwa na nchi ya design hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupongeza sana Mheshimiwa alete hiyo Sheria hata kesho tubadilishe. Tunachotaka ni nafuu ya maisha ya Watanzania. Hatuwezi kung’ang’ana na sheria ambazo watu wetu wanakandamizwa. Inawezekanaje wewe unang’ang’ana na sheria halafu sheria imetungwa miaka 30? (Makofi)
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunadhani tunataka kusaidia nchi hii ni vizuri tukaweka Sheria viwanda vyote vya sukari vitauzia NFRA halafu NFRA ndiyo ianze kusambaza. Leo Watanzania tumefika mahali pa kuweza kuepuka hili tatizo kubwa ambalo tunahangaika nalo la ku-import sukari tuamue kwamba tu-import sukari, tafsiri yake tunaua viwanda, tukiua viwanda halafu matokeo yake ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukweli tuzungumze ukweli tofauti na hapo maana yake ni kwamba tunarudi miaka 47 mahali tulipotoka. Ahsante.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Musukuma unaipokea taarifa?
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba unilindie muda wangu na niwaombe Waheshimiwa kwa sababu kila mtu ana dakika 10 zake tujipange tu kuchangia tusipigane taarifa, nilindie muda wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipi bora, kuwa na viwanda sawa kila mtu anataka kiwanda tunataka watu wetu wapate ajira, lakini tuwe na viwanda vya wanyonyaji ambao wanaweza kutengeneza kuipiga shoti Serikali halafu watu wakanunua sukari shilingi 10,000 pembeni hapa tu Mutukula, watu wananunua sukari 2,800 hivi ni viwanda au ni viwandani? Haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka kuwa na viwanda na ndiyo maana Bunge tunapitisha misamaha, lakini tunaowapa kufanya kazi ya viwanda na wao wawe waungwana. Haiwezekani tukawa tunasema tuwe na viwanda, kiwanda ambacho kinaweza kutengeneza shoti halafu kikauza kwa bei isiyotakiwa na Serikali imekaa kimya. Hii itakuwa siyo sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri leta Sheria tutaidadavua humu ndani tupitishe watu wapate nafuu ya sukari tuepukane na hili janga a kupigizana kelele na sukari. Hata ukiwauliza watu wa kilimo, ukiwauliza watu mipango, hakuna mtu anayejua sukari inazalishwa kwa gharama gani kwa kilo hakuna hata moja. Waambieni wawape gharama ya kilo moja ya sukari wanatengeneza kwa shilingi ngapi? Hakuna mtu anayejua. Sasa hii ni Serikali, lazima ilinde watu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha tena wote wanatoka mMoa mmoja wa Singida. Niwaombe kuwasikiliza wafanyabiashara na kutatua matatizo yao ni jambo kubwa ambalo wataacha legacy kubwa sana. Nakumbuka mwaka jana tulianza kuwaambia humu suala la Kariakoo wakawa wanapiga chenga akiwa dada yangu Mheshimiwa Dkt. Ashatu. Kikaumana Mheshimiwa Waziri Mkuu akaenda akaokoa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watu kila siku wanawaeleza na wamewaita kwenye Kamati wamewapa mapendekezo wanakwepa kuyatatua. Kuna ugumu gani kwa mfano wamewaeleza wanasema ukifika bandarini unaambiwa ulipe kodi 100 na kuna 100 nyingine ya mfukoni. Wao wako tayari kulipa hiyo 200 lakini iwe bei elekezi ya Serikali. Halafu Kariakoo nilishawaambia siku zote wafanyabiashara wengi ni darasa la saba hawajui mahesabu ya kodi. Kwa hiyo kodi unaenda kutegemea utakayemkuta leo yupo unalipa 50 kesho 100 na za mfukoni 100, haiwezekani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamewaomba na Kamati ya Bajeti wasikilizeni, wapo tayari kulipa lakini walipe kwa bei elekezi. Kama tunafuata viatu kontena ni 200 tulipe yote iingie Serikalini. Sasa haya majadiliano kila siku na Mheshimiwa Waziri Mkuu siku ile akiwa pale, nilikuwepo, kuna makubaliano waliweka lakini hawataki kutimiza; wawasikilize wafanyabiashara. Leo hii sisi watu wa Tanzania tunafuata bidhaa Uganda, hawaoni aibu? Tunafuata bidhaa Kenya, hawaoni aibu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari inatumika ya Dar es Salaam kuchukua mizigo kupeleka Uganda halafu sisi tunaifuata Uganda kuileta Tanzania hii haiwezekani! Tumekosea wapi? Lazima waangalie, tukiiua Kariakoo tutakuja kushikana mashati humu ndani. Kariakoo ndiyo kila kitu kwa Tanzania, kwa hiyo ni vizuri tupalinde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine waangalie namna Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kamata kamata Kariakoo ni nyingi mno. Hakuna mgeni anaenda kwenye nchi inayokamata. Ukinunua t-shirt una pini, ukinunua haka una pini. Mwisho wake watu wote wa Zambia sasa hivi wanenda Uganda sasa kweli haiwezekani. Mheshimiwa Waziri Mkuu siku ile alieleza vizuri sana kwamba operation walitajwa mpaka mapolisi wakatajwa na nani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipita hapa barrier ukipita huku, kila mtu siku hizi mle ana tai. Sasa kwa kweli niwaombe sana tuiangalie Kariakoo tusije tukaipoteza tutapata hasara kubwa sana. Ni vizuri wawasikilize kama wana mambo yao wawasikilize wasiwanyime muda wa kuwasikiliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kuhusiana na suala la spirit (ethanol). Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ni mchumi na kaka yangu Profesa tulikuwa tunakaa wote wakati akiwa huku nyuma, ana busara kubwa sana na bado namwamini. Sasa nataka niwaulize; sisi hapa wamesajili viwanda vya pombe hizi kali wamesajili wamevipa certificate, wamevipa leseni na vinalipa kodi nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa, najua labda wanalenga kuzuia fake, lakini walichokilenga ni kuua hii biashara. Haiwezekani Mheshimiwa Dkt. Mwigulu mchumi, dokta mwenzangu pipa moja la ethanol kulitoa nje kulileta hapa linagharimu shilingi 600,000, ukilipa na ushuru ilikuwa shilingi 200,000 na gharama zingine inakuwa shilingi 1,000,000. Leo wewe ushuru kabla ya kununua umeweka shilingi 2,000,000. Sasa pipa lililokuwa linauzwa shilingi 1,100,000 likauzwe shilingi 3,500,000 huo uchumi wa design gani? Maana yake wanataka watu wafunge viwanda, waliwapa leseni za nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mama kila siku anahamasisha watu wafungue viwanda wanawapa leseni, wanawapa vibali wakishakopa hela ya benki wanaingia tena na Sheria mpya; haiwezekani! Nimwambie Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Waziri Profesa Mkumbo tuwe hai. Watoto hawa baada ya kufunga hivi viwanda vya pombe watarudi kwenye ugoro na madawa ya kulevya hakuna starehe nyingine. Sasa hata konyagi haitatengenezwa, hakuna K-vant, hakuna kila kitu. Ni lazima wakae warudi waangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu akatoa ushuru wa shilingi 220,000 akapeleka 2,200,000. Hii ni biashara gani jamani au labda calculator zinakuwa zinaenda mbele na nyuma? Ninadhani tuwe makini sana tunapoamua kubadilisha. Hawa watu walishaingia kwenye mfumo wa biashara na walishakopa hela za benki halafu unam-disturb tena. Wataua wafanyabiashara halafu kila siku wanahamasisha suala la wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, nipo kwenye Kamati ya Nishati. Tulitembelea viwanda vya gesi ya magari. Kwanza tu kutengeneza ule mfumo wa gesi kwenye gari inaenda karibu shilingi 2,000,000 halafu vituo vyenyewe vya ku-refuel gasi ni viwili peke yake. Kituo cha Ubungo pale Urafiki mtu anaenda saa 8.00 usiku anapata huduma saa 7.00 mchana. Tulifika pale Kamati watu wanasema sisi hatutaki kuwaona Waheshimiwa Wabunge foleni imeshatuweka hapa mpaka gari za watoto anakwambia nimekuja sasa 7.00 usiku mpaka saa 5.00 asubuhi tunaenda pale, bado anasubiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu Serikali vituo viwili kingine Airport. Tukiwa kwenye hii hali ya kubembeleza watu warudi kwenye hiyo biashara ya kutumia gesi unaongeza tena ushuru jamani? Nilidhani Serikali itatoa subsidies kupunguza bei badala yake tena unataka kukusanya shilingi bilioni tisa kwenye gari 3,000; kweli hatuna chanzo kingine? Ni vizuri tusifanye bajeti ya ku-copy na ku-paste, ni vizuri waumize vichwa. Serikali inawalipa pesa waumize vichwa kutafuta vyanzo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirundika kila siku vitu kwa watu inaleta chuki kubwa sana kwenye Serikali. Nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Profesa Mkumbo suala la mashudu na bahati nzuri na mwenzangu jana alizungumza. Mashudu yanaangukia Singida na tunaenda kwenye uchaguzi. Mashudu ya alizeti yapo Singida peke yake, ukiyawekea ushuru hiyo withholding tax watu hawatayanunua. Kwa hiyo watu Wanyiramba pale watayalalia kitandani au yataenda wapi? Kwa sababu ng’ombe zinafuata majani sisi hatuna mfumo wa kulisha mashudu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekanaje tunakuza kilimo, tumeua pamba, tumekuja kwenye alizeti ndiyo inaanza ku-grow tena wewe unaiwekea makorokoro jamani? Nimwombe sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu tunamtakia kazi njema na wewe na Mheshimiwa Profesa Mkumbo, lakini waumize vichwa kutafuta vyanzo vya mapato tusifanye bajeti ya ku-copy na ku-paste. Ni vizuri sana Mheshimiwa Dkt. Mawigulu na bahati nzuri siku ile kwa mfano Kariakoo tulikuwa wote uliona mtiti ulivyokuwa sasa wa term hii ukiamka sijui nani ataenda kwa sababu tulitoa maelekezo hatujayatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vizuri watu wanalalamika wamemwomba punguza, sasa unaenda unaambiwa unalipa service levy halmashauri halafu ukimaliza service levy unakuja hela ya taka, hela ya kwenda kujisaidia na hela ya kupaki. Sasa service levy gani tunawachukulia watu hela? Ni vizuri Serikali tuamue kama tunaenda kutafuta vyanzo vipya tuumize kichwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)