Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arumeru-Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema yeye ambaye ametupa uzima kwa siku ya leo kuwepo katika Bunge hili. Pia, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayofanya kuendelea kulijenga Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri Fedha ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa kuwasilisha bajeti hii ambayo ni bajeti ya matumaini kwa wananchi wa Tanzania. Nianze tu kwa maeneo kadhaa nikianza na eneo la suala la makusanyo ya Serikali. Katika makusanyo ya Serikali tunakusanya fedha ndiyo, lakini bado hatujaweza kufikia katika kiwango kile ambacho kinatakiwa kwa ajili ya kukidhi nakisi ya bajeti ambayo tumejiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika tafiti mbalimbali ambazo zimefanyika ukiangalia hakuna mwaka ambao tumeweza kufika tukaweza kuvuka yale malengo ya bajeti ambayo tumeweka. Kwa hivyo suala hili linahitaji umakini na umahiri wa hali ya juu na kwa jinsi ambavyo namfahamu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na kazi zake na timu yake ni lazima wahakikishe sasa kwamba wanafikia bajeti hiyo waweze kuikusanya kwa kiwango ambacho bajeti inatakiwa kama Bunge ambavyo tunakwenda kupitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukusanya mapato kuna changamoto nyingi ambazo zinaikabili Wizara hii, kwa mfano suala la rushwa. Rushwa katika kukusanya mapato kwa baadhi ya watumishi (siyo wote) wanafanya bargain kwamba wewe lipa labda shilingi bilioni 15 ndiyo kodi yako, lakini baada ya hapo yule mfanyabiashara atakapokuwa analalamika, basi inarudi kwamba wanaenda kupatana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupatana wanarudi kwenye makubaliano fulani kwamba sasa wewe lipa shilingi milioni tano lakini unipe shilingi bilioni 10 ije kwangu. Ninayasema haya siyo kwamba ni suala ambalo siyo ukweli kwa sababu siyo baadhi ya watumishi wanaofanya hiyo kazi, lakini wachache ambao hawaitakii Tanzania mema, wachache ambao hawaitakii Wizara hii mema wanafanya hivyo. Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ana kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba Wizara yako hiyo katika kukusanya fedha za umma kunakuwepo na uadilifu na uaminifu wa hali ya juu ili mwisho wa siku tupate watumishi ambao wanaweza kuwa waadilifu zaidi japo wengi wanafanya kazi yao vizuri, lakini kuna baadhi ya wachache ambao wanaharibu ile taswira ya TRA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, ningeomba kuishauri Wizara hii Sheria ya suala la kujadiliana kwamba ulipe kodi ya kiasi fulani. Ninadhani hii Sheria Mheshimiwa Waziri wangeendelea kuiangalia namna ya kuiboresha zaidi. Suala la kukaa mezani au mtu kukaa kukadiria kodi inasababisha rushwa zaidi. Kwa sababu kama ingekuwa kuna fixed kwamba mtu ana biashara fulani Sheria ndiyo inatamka wazi siyo mtu anakisia, ninaamini tungepunguza suala la rushwa na tungekusanya fedha nyingi sana kwenye nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la kutofikia kiwango hicho ni kwamba hatutaweza kutimiza miradi yetu ya maendeleo...
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa.
TAARIFA
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza nakubaliana naye kwamba Sheria yoyote ambayo inatoa hiyari ya afisa yeyote wa Serikali au TRA ku-negotiate ile kiasi cha kodi, basi hiyo Sheria itakuwa ina matatizo makubwa kwa sababu inakaribisha rushwa; yaani kama Sheria inapanga kwamba atoe kati ya 10,000 au 30,000. Kama ni cutting iseme tu kama ni 30,000, iwe 30,000 basi na kama ni 20,000 iwe 20,000 basi, siyo ku-negotiate. Ahsante sana.
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Noah unapokea taarifa ya Mheshimiwa?
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa hiyo kwa mikono miwili na ndiyo madhumuni hasa ya kusema hilo eneo ndilo linalosababisha kutokukusanywa kwa mapato ya Serikali kwa sehemu kubwa. Pia ndiyo inayosababisha hata TRA kushindwa kufikia malengo na Serikali kufikia malengo ya kukusanya fedha ili kwenda kuhudumia miradi ya maji, miradi ya kimkakati kwa maana ya Bwawa la Nyerere na miradi mingine yote ile ambayo inatakiwa Wizara ipeleke fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Sheria hii tunaweza tukaibadilisha naomba sana iletwe hapa Bungeni tuiweke vizuri, wataalam wakae ili basi tuhakikishe kwamba tunakuwa na Sheria ambayo haina ukakasi wa kuendelea kutoa mwanya wa rushwa ili basi wale wala rushwa wasiendelee kuhujumu nchi yetu na kuhujumu hii miradi ambayo tungetegemea kwamba iweze kupelekwa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara kwa mara pia kila ripoti inayokuja ya CAG kunakuwepo na masuala ya madudu ya udokozi udokozi na ulaji ulaji. Hii inatokana na nini? Inatokana na watumishi pia ambao siyo waadilifu na watumishi ambao hawafikiri kuhusu uzalendo wa nchi hii kwamba wananchi hawana maji, wananchi hawana barabara, mafuriko yametuvamia barabara zimeharibika na mambo mengi makubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie suala hili kwa sababu tusipofikia mahali pa kuweza kuwasimamia watumishi wakaweza kuhakikisha kwamba wanakusanya mapato kwa ukamilifu na uadilifu mkubwa, kila mwaka Taarifa ya CAG itakuja hapa na tutakuwa kwenye mazingira magumu ya kutokuwa na aibu ya kila mwaka kuna ufisadi, rushwa, mambo ambayo hayafai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Waziri ajitahidi kujitathmini kwenye Wizara yake, Waziri wa Fedha, sijui Waziri wa Maji, kama kuna vitu vyovyote ambavyo vinatokea kwenye Wizara zao wajitahidi na ninaona wanajitahidi kweli, lakini waongeze juhudi na wale watu wote walioko chini yao wahakikishe kwamba wanafanya kazi vizuri kwa uaminifu na uadilifu ili bajeti hii ambayo tunaenda kuipitisha ikapate kuzaa matunda na ikapate kuwa na matumaini makubwa kwa wananchi Watanzania na kuweza kumsaidia Mheshimiwa Rais kufikisha malengo yake ya kuwahudumia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kama ambavyo anajitahidi kwenda huku na huko kutafuta fedha na sisi tunakuja kuneemeka huku. Kama suala la makusanyo likisimamiwa vizuri naamini nchi yetu itakwenda mbali na itasonga mbele zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la misamaha ya kodi; nilipokuwa napitia ripoti kuna misamaha mingi ya kodi ambayo inafanyika, lakini hatuangalii sana maslahi makubwa ya Taifa. Niombe kwa wale wahusika, misamaha ya kodi ilenge katika kuhakikisha kwamba ina tija kwa Taifa na inaleta matumaini kwa wananchi. Wasisamehe kodi bila utaratibu kwa sababu tukisamehe kodi bila kuangalia uchumi wa nchi yetu, bila kuangalia Serikali inanufaika na nini, ninaamini hapa tutakuwa tunahujumu Taifa, tutakuwa tunahujumu wananchi wa Tanzania, tutakuwa tunafanya jambo ambalo ni kinyume na nafasi zetu ambazo tumepewa. Naomba sana tuhakikishe kwamba tunaacha kutoa misamaha ya kodi isiyokuwa na utaratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni ukosefu wa watumishi TRA; watumishi ni wachache TRA na kwenye taasisi zingine za fedha ambazo zinakusanya fedha. Suala lingine ambalo linaikumba TRA, TRA ni miongoni mwa taasisi ambazo zinatajwa katika tafiti mbalimbali, nenda kasome, inaonekana ni miongoni mwa taasisi ambazo zinaongoza kwa rushwa na rushwa yenyewe inatokana na suala la kujaribu kufanya ajira, ajira ya TRA ni changamoto sana kwa wananchi wengine wa kawaida kupata. Kwa nini ajira za TRA zisirudishwe kwenye utumishi ili utumishi ndio uwe unasimamia kwa sababu matumaini makubwa ya Watanzania yako kwenye Wizara ya Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ili tupate watumishi waadilifu, TRA na Benki Kuu ni ajira ambazo haziko wazi, ziwekwe wazi ili wananchi wote Watanzania waombe na waweze kufanikiwa kwa sababu bila kufanya hivyo ina maana kutakuwepo na ubaguzi na hapo ndipo ambapo tunakwenda kukidhi matakwa ya nepotism katika kutowapa wananchi wetu usawa katika kupata ajira zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niombe kumalizia kwa kusema, ninajua Wizara ya Fedha na Wizara zote wana kazi kubwa ya kutekeleza bajeti hii, sasa ni jukumu letu sisi wote kuungana kwa pamoja tukiwemo sisi Wabunge na ninyi Waheshimiwa Mawaziri na Makatibu Wakuu na wote wanaohusika katika kutekeleza bajeti hii kuhakikisha kwamba tunakwenda kutekeleza bajeti hii kwa kiwango ambacho kinatakiwa kwa kupeleka fedha, kwa kuwapa makandarasi fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ili kuepuka suala la kutowapa makandarasi fedha ambapo baadaye zinatokea zile penalty ambazo inakuwa ni gharama kubwa kuja kuwalipa makandarasi kwa sababu hatukuweza kulipa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua Serikali inajitahidi kwa kiwango ambacho imeweza na bado tunaona jitihada zao kubwa wanazozifanya, basi naomba waendelee kuongeza jitihada na juhudi kubwa katika kuhakikisha kwamba shughuli hizo zinakwenda vizuri na nina imani na wao, tuna imani na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na tuna imani na wote ambao wamepewa madaraka na Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)