Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MWANTUMU DAU HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na hali ya uzima na afya, lakini niwashukuru na Wabunge wenzangu sasa hivi naona wako wazima na wana afya kabisa katika viti vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mawaziri wangu, Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa wanazozifanya katika Wizara zao na leo hii wapo hapa tunawapitishia bajeti zao. Kwa hiyo, kuna masuala ambayo tutaweza kuyachangia na wao wakayachukua wakaweza kuyafanyia kazi, kwa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nina suala hili la bandari na mizigo, hasa kwa wajasiriamali. Suala hili tunalizungumzia sana humu katika Bunge hili Tukufu lakini bado lina kadhia yake halijakaa sawa. Leo kama ya nne au ya tano nitasema, kuna jamaa yangu mmoja kapitisha mzigo mdogo tu mpaka kunipigia mimi huku akiniambia kwamba nina mzigo wangu, lakini watu wamenikamata na hasa watu wa TRA pamoja na watu wa Uchukuzi. Kwa maana hiyo Uchukuzi na TRA wanashirikiana na imebidi atoe pesa kwa hali yoyote ile ili ule mzigo upate kupita uingie katika boti uende zake Zanzibar, je, Serikali inalizingatia vipi suala kama hili na tukizingatia sisi ni watu wa muungano? Mwenye mzigo mdogo aachiwe apite akafanye shughuli zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio kama mzigo mdogo mtu akimwona mjasiriamali kama yule mwanamama, hali yake duni hana kitu, katupa nauli yake kutoka Zanzibar kaja Dar, kaja kutafuta mzigo wake unakwenda zake kule Zanzibar. Matokeo yake leo hii anafanyiwa kadhia kama hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango hili suala walichukue na wakalifanyie kazi na hili suala tusije tukaliona tena katika bandari ile kwa sababu wanatukera sana hasa sisi watu wa Zanzibar na wakati sisi ni watu wa Muungano, tunaomba hili lifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili, nazungumzia kuhusu suala la ndege, suala la utoaji wa tiketi za ndege kupandishwa nauli kila wakati, ukienda leo unakuta pesa nyingine, ukienda siku nyingine unaikuta pesa nyingine. Kwa hiyo, hili suala nalo linaumiza, bado hatujawa na mustakabali mzima wa Taifa letu ambapo tukienda kwenye ndege tunakuta shilingi 260,000 ama shilingi 350,000 kila siku tunapandishiwa nauli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala hili la nauli nalo naomba walifanyie kazi, kwa sababu mataifa ya wenzetu wa nje wao wana punguzo katika ndege zao, je, itakuwa sisi hapa Tanzania, ukizingatia kuwa ndege zetu zipo na hizi tunasema ndege zetu wenyewe. Hebu watufanyie wepesi wa hizi ndege kwa sababu na mabasi nayo wakati mwingine ukizingatia watu wazima hawawezi kuyapanda migongo inawauma, mwili wote hata akifika Dar es Salaam wa maji. Kwa hiyo, watufanyie wepesi katika nauli hizi za ndege. Mheshimiwa Waziri wa Fedha alifanyie kazi suala hili ili twende sambamba tuweze kupanda ndege kwa murua bila wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la tatu, ni kuhusu huu mpango wa unyanyasaji. Juzi tu hapa tulizungumzia mpango huu wa unyanyasaji katika Wizara ya Maendeleo, lakini tunazungumzia lile kumbe sisi tunapiga kelele kule wanatuambia mtakoma. Hapo hapo watoto wetu wananyanyaswa, walimu wanawanyanyasa watoto, kweli ni vizuri? Ustadhi mzima kanyanyasa watoto juzi tu hapa na nikasema hawa watu wahasiwe, jamani sheria iletwe Bungeni haraka kwa Wizara hii ya Mipango, Wizara hii ya Fedha, sheria iletwe hapa Bungeni haraka tuifanyie kazi ili hawa watu wanaowafanyia vitendo viovu wahasiwe. Mimi nasema tena wahasiwe ili hii kadhia wanayowafanyia watoto wetu kwa makusudi kwa kuwabaka na kuwafanyia vitendo vibaya hivi wanavyotaka sio vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mbunge mmoja pale kalia machozi ule unyanyasaji, mtoto kakatwa viungo kisha wamemwacha, wamechukua viungo vyao wameenda zao, kweli vile hii ni haki? Mtu kama yule mnamfunga maisha hatoki mpaka anakufa huko huko. Hili linakuwa sheria ipitishwe hapa vilevile, suala hili linatuuma na lifanyiwe kazi katika hizi Wizara zao. Hii Wizara ya Maendeleo waiongezee kipato ili na wao waweze kufanya kazi vizuri kwa sababu kipato chao wanachoingiziwa ni kidogo. Kwa hiyo, waongezewe kipato ili waweze kufanya kazi vizuri, watu wazima humu na akili zao hawana adabu wanabakabaka tu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nazungumzia suala la askari jamii katika nchi yetu kila mahali pana askari jamii. Wengine wanakubali kabisa kutumwa na wanatumikia vizuri na ukienda katika kijiji kimojawapo unakikuta kijiji kimetulia na kinafanya kazi vizuri hasa kijiji chetu cha Wilaya ya Kusini, Kijiji cha Kizimkazi, kwetu mimi nilikozaliwa, askari jamii wamepangwa vizuri na wanafanya kazi vizuri, kule hakuna uhalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hao askari jamii na wao wafanyiwe kazi ili waweze kufanya kazi vizuri wasiwe nyuma, tuwe nao watulinde usiku na mchana ili angalau sisi watu wazima tuweze kulala. Maana wewe unaingia ndani unalala huna raha, hujui nani ataingia ndani ya nyumba yako. Kwa hiyo, hawa askari jamii nao pia kwa Wizara hii ya Mipango na Wizara ya Fedha na wao wafanyiwe kazi ili waweze kufanya kazi vizuri, kama ni kuhusu suala la michezo, wafanye michezo vizuri, kama suala la kwamba mmoja mmoja mle anaweza akatolewa akawa yeye ni askari kabisa kutokana na juhudi zao wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na ahsante sana. (Makofi)