Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Mwanakhamis Kassim Said

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Magomeni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti hii ya roho ya nchi yetu na roho ya chama chetu. Kuna shairi linasema:-

“Huko barabarani kumeingia shabuka, kuna vituko,
Ikishawaondoka, wanatia huzuni na masikitiko”

Mheshimiwa Mwenyekiti, shairi hili Naibu Waziri, Mheshimiwa Chande, atawafafanulia. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, nafikiri alipoingia kwenye madaraka wengi walidhani hawezi, lakini waje kumtazama au kumsikiliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dkt. Samia Awamu yake ya Sita amefanya mambo makubwa sana na sote ni mashahidi. Hata hivyo, huwezi kumzungumza Mheshimiwa Dkt. Mama Samia ukawaacha Mawaziri wake, Naibu Mawaziri na Makatibu Wakuu. Hawa ndiyo wasaidizi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Tunapozungumzia barabara Waziri yupo, unapozungumza afya Waziri yupo, unapozungumza Elimu Waziri yupo, na kadhalika, na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashangaa sana kumkuta Mbunge anaacha kuzungumza maneno Bungeni au kwenye chama chake anakwenda kuzungumza kwenye mitandao au kwenye vyombo vya habari. Ukimkuta Mbunge kama huyu ana lake jambo. Tena Waheshimiwa Wabunge tusilichukulie jambo hili kwa urahisi, hawa ndio wanaoturejesha nyuma katika maendeleo, hawa ndio wanaoirejesha nyuma Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na hawa ndio wanaomrejesha nyuma Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Sisi tunasema Mheshimiwa Dkt. Samia miaka mitano tena. Atakapoachia miaka mitano tena, basi na wewe utajipanga, kitaamua Chama Cha Mapinduzi au wananchi kukuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimesema barabarani huko kuna shabuka wanafanya vituko, wanawaahidi watu mambo ambayo hayapo kwa sababu, wananchi wanayaona mambo anayoyafanya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni mengi. Vilevile tunaambiwa siku zote tumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini umshukuru na binadamu mwenzako kwa yale aliyoyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wa Tanzania sasa hivi sio wajinga, ni waelewa, yanayofanywa wanayaona. Mheshimiwa Dkt. Mama Samia yanapoingia maafa amekuwa ni Rais wa mwanzo anayewakimbilia wananchi. Hajamhamisha mwananchi yeyote kwenye maeneo yake, isipokuwa anamhamisha mwananchi aliyefikwa na maafa au pale alipo yatamfika maafa ndipo anakwenda kumwondosha. Vilevile hamwondoshi kwa mtutu wa bunduki wala kimabavu, anamjengea, anamwekea mazingira mazuri ndipo anakwenda kumweka pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanatokea Watanzania wachache, wanaume, ninawashangaa sana. Hata hivyo, mwanaume huyu, Waheshimiwa Wabunge leo nitasema neno kama nitakosea nitaomba radhi, ukimkuta mwanaume anamtukana mwanamke kwenye viriri, huyo alichelewa kufanyiwa jando. Mwanaume huyo alichelewa kufanyiwa jando mpaka akaingia huko mitaani ndipo wakamwambia bora uende ukafanyiwe jando na waliomwambia ni wanawake. Kwa hivyo, leo ndiyo unamkuta kinywa chake kipana kumtukana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, haiwezekani na haikubaliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wanawake tunasema Mheshimiwa Dkt. Mama Samia ametufikisha mahali pakubwa sana. Tunajiamini na tunajielewa. Tunafanya kazi zetu kwa maono makubwa kuwa, hatujali kama mimi siwezi, mimi ni mwanamke. Mfano mdogo ni dada yetu Mheshimiwa Jenista anapofanya kazi zake kwa kweli, huyu mama ninampenda sana na ninamfagilia sana. Anaisaidia Serikali ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, lakini pia, anakisaidia Chama Cha Mapinduzi na analisaidia Bunge hili kwa nguvu zake zote. Waheshimiwa Wabunge tunapokaa kuzungumza ni lazima mambo mengine tupongezane, tushukuriane na tujaliane, isiwe kila kitu hatufanyi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamefanyika. Bajeti zilizopita tulisema hapa, jamani Barabara kutoka Dodoma – Dar es Salaam iko vibaya sana. Hata hivyo, leo Wabunge tunaokwenda Dar es Salaam asilimia kubwa tunaona barabara inavyotengenezwa, imepiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Waziri wa Fedha, tunapita pale Chalinze, usiku unakuta taa barabarani zimejipanga. Pia hii barabara ya Dar es Salaam ni kubwa na ni barabara ya biashara. Hebu na sisi tujipange kutia zile taa za barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwantumu alizungumza akasema kuhusu kadhia ya bandarini. Mheshimiwa Waziri wa Fedha pale pana Wizara nyingi, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Wizara ya Bandari (Wizara ya Uchukuzi), wakae wajadili. Wanaopita pale ni wananchi wetu na wapigakura wetu, ninadhani wakae watazame vizuri na vilevile wale waliopo pale bandarini wawape elimu. Wakitaka kuzungumza kitu kizuri hata kama hakiwezekani, basi wazungumze na mtu vizuri. Hakiwezekani, lakini zungumza naye vizuri akuelewe kuliko ukiwa unampa maneno ya shombo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba sana suala la pale bandarini limezungumzwa kwa muda mrefu, miaka mingi sana, walikalie kitako, kwa sababu, pale mwananchi anayepita anasema hao ni CCM, huyo ni Dkt. Samia, haiwezekani! Kwa hiyo, haipendezi. Mheshimiwa Waziri, tunakuomba walisimamie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mabasi yanayokuja mikoani. Mabasi yanayokuja mikoani yana vituo vyao vidogovidogo vya kupakia abiria kutoka mjini kwenda Magufuli, Mbezi. Watu wengi wa karibukaribu walioko Dar es Salaam watakwenda pale Shekilango na maeneo mengine. Hata hivyo, toka juzi watu pale wamekuwa wanazuiwa wanaambiwa wasiende kuingia, watu wanafukuzwa na wanapata shida sana. Kutoka pale mjini mpaka kuelekea Mbezi ni shilingi 30,000 au shilingi 50,000 kwa taxi. Suala hili linakuwa gumu na wananchi wetu wanapata tabu. Tusijitazame sisi tuwatazame wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi viongozi tuwajali zaidi wananchi wetu na ndiyo tunaisaidia Serikali yetu, chama chetu na Rais wetu. Ikiwa wale wananchi wa chini hatuwatazami na hatuwasikilizi matakwa yao ndiyo tunajiharibia sisi wenyewe. Leo utasikia DC ndiyo amezuia. DC hana uwezo wa kuzuia mabasi yasipakie Shekilango kwa sababu, kuna Sheria, sasa aisome ile Sheria. Vilevile ma-DC wamepelekwa kule, ili wakasimamie wananchi wamsaidie Rais na kukisaidia chama chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ukifanya lazima ujiongeze. Tusiwe tu kwa sababu, tumekuwa kwenye magari makubwa wale wa chini tunawaacha, tunakosea na tunakosea sana. Sisi wanawake tunapowakuta wananchi wetu kama wale roho zinakuwa zinatuuma sana kwa sababu, moja kwa moja anakuwa analengwa mkuu wetu wa nchi wakati lile suala ni la DC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine wazee wetu walikuwa wanasema “mnakuwa mnajitakia”, lakini sio kweli. Hatujitakii, ila ni lazima tujiongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kumzungumzia Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Ninampongeza sana, anafanya mambo makubwa sana Zanzibar. Aliyekuja jana na juzi kwa kweli, Zanzibar imepiga hatua kubwa sana ya maendeleo. Zanzibar kila wiki, kila mwezi ukienda kuna jambo jipya, mambo yamebadilika. Sasa wale wanaotia chokochoko Mheshimiwa Dkt. Mwinyi anaendelea kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Zanzibar kuna wazee, nyumba za wazee na Wazee Welezo. Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi wazee wale amewaweka kwenye Nyumba za Serikali Amani kwa Wazee. Hata hivyo, anawalisha, anawavisha na anawahudumia. Vilevile kuna wazee walioko mitaani, amewachukua wazee wale, kila mwezi alikuwa anawalipa shilingi 20,000 na sasa anawalipa shilingi 50,000. Wale wazee anawaenzi, tunasema Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi anafanya mambo makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja lilizungumzwa neno tukaambiwa tunataka passport. Sisi Zanzibar suala lile hatukuliunga mkono na wala hatukuliafiki. Sisi Zanzibar tuko na amani na tunapenda wageni kwa sababu, sisi Zanzibar tunapenda kutembea. Sisi Wazanzibari asili yetu ni kutembea na kufanya biashara kila maeneo na kila sehemu. Kwa hiyo, madhali tunatembea kwa watu na sisi tunasema Zanzibar ni njema atakaye na aje. Aje kwa maendeleo, upendo na kuishi na Wazanzibari, hilo kwetu sisi hatuna shida. Passport hii sisi bado hatujawa tayari, wala hatukuunga mkono na wala hatukumtuma mtu aje alizungumzie suala lile. Tunalilaani na sisi Wanzanzibari tunalilaani kwa nguvu zetu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)