Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Bajeti hii ya Serikali ya mwaka huu 2024/2025, lakini pamoja na Mpango wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, IMF ilibainisha vihatarishi vinavyoweza kusababisha kutofikiwa kwa malengo ya ukuaji wa uchumi wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Nchi yetu ya Tanzania. Baadhi ya vitu hivyo ilikuwa ni upatikanaji wa mitaji, uhaba wa fedha za kigeni, gharama kubwa za mikopo na ukusanyaji duni wa mapato ya ndani. Hayo yaliainishwa huko lakini pia kuna vitu ambavyo vinaweza kusaidia kuimarika kwa uchumi kama tunavyo ambavyo ni upatikanaji wa dola za Marekani pamoja na kupungua kwa mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuzungumzia suala la gesi kwenye magari ambalo Waheshimiwa wenzangu wawili watatu wamezungumza. Tumeona siku zote kuna mfanyabiashara mkubwa Dangote yeye alikuja na magari yake na yakawa yanatumia gesi exclusively kabisa na yalikuwa na sehemu yake anayotumia. Sisi raia wa kawaida kwa Dar es Salaam ambapo tuna vituo vikubwa ambacho kipo Ubungo tuna kituo kingine kiko TAZARA na kuna kituo kingine kiko airport.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu tumegundua gesi ya kutumia kwenye magari tumekuwa na kituo mama ambacho ni cha Ubungo kikikorofisha ina maana vile vituo vingine haviwezi kupata kabisa gesi ya kuweka kwenye magari na sasa hivi watu wameanza kuhamasika. Watu wamehamasika kutumia magari wafanyabiashara, wenye magari ya uber, madereva wa malori na watu wengine wanajitafutia vipato wameanza ku-install vifaa vya kuweza kutumia gesi kwenye magari yao kwa sababu hiyo tunaona kwamba hili ni jambo zuri sana na linafaa kwa nchi yetu kwa nini? Kwa sababu kwanza hatuagizi gesi nje, gesi inapatikana nchini mwetu na kama inapatikana nchini mwetu ina maana kwamba hatutatumia dola kwenda kununua mafuta huko nje. Kwa hiyo ina maana kwamba sisi tutakuwa tumeweza kuhimili huo mfumuko kwa sababu tutakuwa na dola ambazo hazitumiki nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimeshtushwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyosoma ile hotuba kuongeza shilingi 382 kwa kila kilo ya gesi. Sasa hapo nikaanza kujiuliza unapoongeza mapema namna hii na watu wamehamasika watu wanaanza kutumia gesi na kubadilisha magari yao na kubadilisha ni gharama na ni kuanzia shilingi milioni mbili, milioni tatu na kwa malori milioni kumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa mtu anayenunua gari akatumia mafuta haiingii hizo gharama, sasa huyu anayetumia gesi ataingia kwanza hizo gharama za mwanzo za vifaa vya kuwekeza kwenye matumizi haya ya gesi, sasa hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba tunatakiwa tutoe hata incentives tuweke ruzuku kwa vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya kuweka kwenye magari yale ili wananchi waweze kuweka kwa gharama ndogo ama kama ni ruzuku basi waweke kwanza ili gesi iweze kutumika na inunulike itumike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gesi yetu ikitumika hivyo tutakuwa tumeweza kufanya kazi kubwa, kwanza kule tutakuwa tumewanyima kazi kwa sababu kule tunavyopeleka dola tunanunua mafuta wenzetu wanaendelea kuwa na viwanda; vijana wanapata ajira na kadhalika. Sisi huku vijana hawapati ajira kwa sababu gesi yetu hatuitumii vizuri. Pia mteja wa gesi ni TANESCO, lakini tukifanya hivyo Watanzania walio wengi, magari ya Serikali na magari mengine watakwenda kutumia gesi yetu vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutakuwa tumeacha kuagiza mafuta nje lakini sisi wenyewe dola tunaipata kwa shida yaani uuze korosho, uuze tumbaku, uende ukachimbe madini, uende kufanya utalii vitu vyote hivyo vinatufanya tutafute dola. Sasa kama tunatafuta dola halafu tunakwenda kununua mafuta badala ya kutengeneza namna ambayo tutafanya gesi yetu iweze kutumika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ndilo jambo ninalomwomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, anapokuja hapa hebu atueleze kwa nini ameweka hii gharama tena sasa? Badala ya kuacha kwanza angalau watu wahamasike waweze kuwekeza huko ndipo baadaye sasa tukiona kwamba ina manufaa tuone namna nyingine ambayo tunaweza tukafanya. Kwa hiyo, tutapata wateja wengi kama tutatoa ruzuku na tutaweza kuwasaidia wananchi. Vilevile, tutatengeneza ajira kubwa sana hapa nchini kwa sababu tutakuwa tumewafanya vijana wetu wamepata nafasi ya kuweza kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ni suala kushukuru Wizara imeweza kusikia na kuongeza kikokotoo ambacho wananchi walikuwa wanapiga kelele kwa muda mrefu. Japo wameongeza kutoka 33% kwenda kwenye 40% na ile kwenda kwenye 35% lakini mimi hoja yangu iko hapa kuna wale wastaafu ambao walishakuwa wamepata kiinua mgongo chao na wanalipwa kila mwezi hawajawahi kubadilishiwa wanakwenda na kiinua mgongo kilekile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi za wenzetu unaona kwamba wanavyopandisha kima cha chini na pensheni inapanda. Kwa hiyo unakuta kwamba yule ambaye amestaafu na yeye ananufaika na kuishi kwa wakati huo kama wanavyoishi wengine lakini mtu anakuwa na kiinua mgongo kile kiko vilevile miaka nenda miaka rudi mtu alistaafu akiwa mwekahazina mkuu na mwingine alikuwa ni mhudumu anakuja yule anapata kiinua mgongo kikubwa na ile pesa ya kila mwezi kubwa kuliko yule na hakuhuishwi kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba Wizara iweze kutekeleza na Wizara ya Mipango iweze kuweka kwenye mikakati yake kuhakikisha kwamba hawa waliokwishastaafu wanapohuisha mishahara, wanapohuisha masuala mbalimbali wawe wanawa-consider kwa sababu ni watu waliofanyia kazi nchi hii, wameitumikia nchi hii kwa uadilifu mkubwa na mpaka sasa hivi bado tunawategemea kwa sababu ni wazee ambao bado wanatupa busara zao. Kwa hiyo hawa wananchi walijenga nchi kwa busara kabisa, tunaomba wawafikirie hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila mwaka huwa tunapitisha Bajeti za Wizara zote ambazo zinaomba tukishapitisha tunajua kutakuwa na matumizi ambayo tumeyapitisha, lakini cha ajabu kwa mfano kuna Wizara ya Maji, Ujenzi na kadhalika lakini kinachosikitisha wakandarasi mbalimbali ambao wanafanya kazi maeneo tofauti wamekuwa hawalipwi fedha na hilo kwa kweli ni janga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kabisa wakandarasi wa Wizara ya Maji wengi hawajalipwa, kwenye Ujenzi huko TARURA hawajalipwa. Kutowalipa wakati tumetenga bajeti hawafanyi sawa kwa sababu kuna kuwa na malimbikizo ya riba ambayo hayo malimbikizo yanakuja kuathiri sasa kwenye bajeti zetu na hatimaye Watanzania wanakwenda kuwa na hali ngumu ya maisha kwa sababu fedha zinakwenda kutumika kulipa riba wakati tulitenga fedha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha hapa atuambie kwa nini tunatenga pesa halafu zile pesa haziendi kulipa hizo certificate ambazo zinakuwa ziko raised na tulipokuwa tukisema hapa anasema fedha zipo hawajaleta lakini inaonesha kwamba certificates nyingi zimekwenda na hawajalipwa pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Taarifa ya CAG inasema hivi kwenye matokeo ya ukaguzi wa kiufundi kuhusu usanifu wa usimamizi wa miradi teule ya usambazaji wa maji, jumla ya miradi mikubwa ilikuwa na mikataba ya jumla ya bilioni 110.7 hiyo ni miradi mikubwa na ilikuwa Fedha za Marekani milioni 523.84 na Euro milioni 52.44, ukaguzi ukabaini Wizara haikuwa na mipango kabambe ya kuwezesha utekelezaji. Hiyo Wizara haikuwa na mipango kabambe, sasa hii imepelekea kuwa na gharama kubwa za riba katika utekelezaji wa mikataba yake na imepelekea gharama za miradi kuongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 337 hadi shilingi trilioni moja ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huu ucheleweshaji wa wakandarasi wa usambazaji, kwa mfano nachukulia mfano mmoja tu wa Mradi wa Usambazaji wa Maji wa Arusha unaitwa Orkesumet ambao aliomba kulipwa riba ya jumla ya shilingi milioni 728.6 na dola za Marekani 284,546.9. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia hizo fedha zingeweza kwenda kutekeleza miradi mingi ya zahanati zetu, vituo vya afya vyetu kwenda kutekeleza miradi ya shule, kwenda kutekeleza miradi ya kuwapa taulo za kike watoto wetu, lakini huyo anaomba hivyo kwenye mradi lakini kule kwenye bajeti tulitenga na hakupata na ali-raise certificate. Kwa hiyo tukiangalia hili, ndiyo maana unaangalia IMF imesema kabisa tunadorora kupata uchumi unaotakiwa kwa sababu ya kutokusanya vizuri mapato ya ndani na kutosimamia fedha ambazo zinatoka hilo ni kosa kubwa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri akija atuambie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nishukuru Serikali kufanyia marekebisho kipengele cha 18, ukurasa wa 82 cha jedwali la msamaha wa kodi linalojumuisha magari pamoja na vifaa vinavyotumika na Jeshi la Wananchi. Tulizungumza sana hapa, tunashukuru Serikali imefanyia kazi kwenye vifaa vile kwa sababu ni mazao ya kijeshi ni vyema vikafanyiwa hivyo kulikuwa na shida. Nashukuru sana. (Makofi)