Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpendae
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. TOUFIQ SALIM TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Naomba nitangulize kumshukuru Mwenyezi Subhanahu Wata’ala kwa kutujalia uhai na uzima na kufika siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niipongeze Serikali kwa juhudi kubwa sana zinazotendeka kupitia Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Kwa kweli dira ya nchi hii inakoelekea na vision iliyokuwepo ndani ya nchi yetu ni ya kupatiwa faraja na fahari kubwa sana siyo ndani ya nchi yetu tu bali ndani ya Bara la Afrika na duniani kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna miradi hii ya kimkakati na nataka niipongeze Serikali hususani katika Mradi wa SGR pamoja na Nyerere. Kupitia miradi hii Tanzania ndani ya Bara hili la Afrika kupitia East Africa tutakuwa kinara. Sasa pamoja Mji wetu huu wa Dodoma leo Mheshimiwa hapa Bibi Mwantumu alikuwa anaongelea kuhusiana na suala la ndege kuja ndani ya capital city yetu hii imekuwa ni changamoto kubwa sana. Sasa hivi ndege inafika shilingi milioni moja mpaka shilingi milioni na nusu kwa sababu ndege zote zinakuwa full. Serikali walitazame suala hili la kuongeza ndege ili sasa Mji huu wa Dodoma uweze kunawiri na uweze kweli kuwa capital city. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kumsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Fedha wakati akihutubia Bunge letu hapa alituambia katika sababu zinazofanya Deni la Taifa kuongezeka ni kwa sababu sarufi imeshuka thamani. Tujiulize, changamoto hii imeikumba dunia yote, lakini ndani ya Tanzania sababu kuu iliyofanya sarufi yetu kushuka ni kuongezeka kwa import lakini pia kuwepo kwa scarcity ya dola imesababisha scarcity ya dola. Hii scarcity inatokana na kitu gani? Tuna imports ambazo asilimia kubwa ya import zetu ni mafuta na sababu nyingine kwa sababu ya loan repayment zetu zinahitaji forex. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, Mheshimiwa mwenzangu aliyenitangulia, Mheshimiwa Tendega aliaongelea suala zuri tu la CNG. Jamani ilipotokea vita Ukraine mafuta kwetu huku yanapanda, vita vinatokea Israel na Lebanon kwetu sisi vinapanda. Tuna rasilimali zetu Tanzania, hatuna ushawishi wala hamasa wala incentives ya kuongeza masuala ya CNG. CNG gesi tunayo leo tunaelekea kwenye kuzalisha umeme kupitia Nyerere Dam Hydro gesi yetu tutakuwa tunayo kwa wingi kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namna gani tunatazama hili suala la forex tukiweza ku-save forex tu basi tayari tulishalipa deni kubwa tu la Taifa letu. Kwa nini hatupi kipaumbele suala zima la forex tukasema hapa lazima rasilimali ya nchi yetu tuitumie ili sarufi yetu iwe imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatoka mjasiriamali Kariakoo alikuwa na pesa zake dola 10,000 akaenda zake China akaleta mzigo. Kafika zake Dar es Salaam kalipa kodi anauza bidhaa yake kakopesha kwa wiki mbili, kauza. Mwanzo alikuwa na milioni 25 kawekeza milioni 30 anauza mzigo anasema bwana kapata faida mwenyewe milioni tano, kumi anaenda ku-change ile dola anaambiwa umepata hasara ya milioni mbili, huyo Mtanzania anaelekea wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ifike sehemu jamani lazima tuwe na mkakati madhubuti, tumechukua mikopo ambayo ni mizuri kwa sababu ya Taifa letu tumewekeza katika mpango na maendeleo ya nchi yetu, lakini yako mataifa makubwa tu kama Spain, Marekani na duniani kote wana restructure mikopo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tumechukua mikopo ambayo tunatakiwa tulipe ndani ya miaka nane hadi 10, kwa nini tusiwarudie tukawaambia mikopo hii tunataka tulipe ndani ya miaka 15? Inawezekana, tukipandisha ule muda automatically ile EMI ya kila muda inapungua. Kwa hiyo, yale mahitaji ya dola yatapungua yataingia kwenye soko letu ndipo tutaweza kui-save forex yetu. Kwa hiyo, naomba sana kupitia Wizara hizi mbili, ya Fedha na Mipango, lazima waje na mkakati maalum wa kuhakikisha kupitia Wizara ya Fedha waje na restructure za loan. Lazima muda wa kulipa hii loan uwe mrefu ili wao wapate pumzi ya kuweza kuhimili kutokulipa dola.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni lazima tutumie rasilimali zetu. CNG ipo, hamasa ipo, lakini bado Serikali hatujaona kuwapa kipaumbele suala zima la gesi asilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, tukiwa tunatembea katika ndege hizi na tukienda safari hizi za mikoani, unaenda sehemu unakuta kwa mbali hakuna nyumba, unapita baada ya mwezi unakuta nyumba mbili, tatu, baada ya miezi sita zinaanza nyumba 10, 20 baada ya mwaka unakuta ni kijiji. Huu mpangilio wa ardhi wa nchi yetu inaonekana bado hatujaupa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna tunavyoendelea tutafika mwisho wa dunia tutasimama hapa itakuwa kilio chetu ni maji, barabara na umeme kwa sababu hatuna mpango wa ardhi, kuna umuhimu sana. Sasa hivi ni lazima ifike sehemu nchi nzima tuwe na mpango wa ardhi. Tujue wapi pa kulima, wapi pa kufuga na wapi kwenye maendeleo ya makazi ya watu kuishi. Haiwezekani leo mtu ajiamulie tu aende porini aweke banda lake, kesho amuite jamaa yake, mjomba wake na shangazi yake, waseme sasa hivi hii ni Kata hatuna maji! Nchi haiendeshwi hivyo! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata huko Marekani, Uingereza na uende sehemu yoyote iliyoendelea ziko sehemu haziruhusiwi kujengwa nyumba. Ziko sehemu za kujenga makazi na ziko sehemu za kufanyia biashara, lazima kuwe na mpangilio. Kwa hiyo, naiomba Serikali itizame suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujikita sasa katika suala la biashara hususani baina ya Tanzania Visiwani na Tanzania Bara. Wizara ya Fedha kuna changamoto kubwa sana ambayo inafanya Visiwani Zanzibar kutokuwa na advantage ya biashara. Leo hii mfanyabiashara anaponunua bidhaa zake Zanzibar anachukua VAT analipa 15%, anapokuja Bara anatakiwa alipe difference ya three percent, inakuwa 18 percent.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina hoteli, nataka ni-claim vitu ninavyonunua Zanzibar ile asilimia ya input ya 15% iweze kunisaidia. Ile haikubali kwenye mifumo yao. Kwa hivyo Sasa mfanyabiashara wa Bara anasema kwa nini ninunue Zanzibar ambapo siwezi ku-claim VAT yangu? Kwa sababu mifumo haioani. Kwa hivyo, namwomba Waziri awaelezee Wizara ya Fedha huko kuhakikisha mifumo yao iendane na ZRA kuhakikisha watu wa Bara waweze ku-claim VAT yao, hilo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili katika suala zima hata masuala ya bidhaa, hapa Mheshimiwa Mwantumu pia kaliongelea, suala zima la biashara unapoleta bidhaa zako kutoka Visiwani kuja Bara na Bara kwenda Visiwani. Jamani hakuna easy of doing business kabisa. Unapofanya biashara baina ya Visiwani na Bara ni kama unaenda zako vitani vile. Unajiwekea makombora yote na kadi zote, leo bwana akija huyu niwe na hiki, niwe na hili na niwe na lile maana inakuwa bugudha hata saa nyingine bora usifanye biashara! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba sana kuna umuhimu wa kuwa na kamati maalum ya kupeleka hizo kero, leo kuna kamati maalum za kupeleka kero hapa East Africa Community, kama kuna tatizo baina ya Kenya na Tanzania, ipo, baina ya Rwanda sijui na nani, ipo, kwa nini baina ya Zanzibar haipo na wakati ni nchi moja? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nenda TRA hiyo moja, huyu anakwambia hivi, yule vile, huyu lile na huyu lile, haiwezekani! Ifike sehemu lazima kuna sehemu twende. Kuna mambo mengine hayataki hata, kuna tatizo la sheria wala policy, kila kitu kipo. Ni mtu tu na tabia yake siku hiyo kakerwa kaamua na yeye akere kila mtu, haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku hizi kuna mifumo ya digitalisation, sasa hivi kuna e-office na kuna kila kitu, hata tunapozungumza committee siyo kama mtu utengeneze jambo lolote kubwa, inatakiwa ile mifumo ioane na kama kuna complains zifanyiwe kazi na siku hizi complains zinaonekana kwa graph tu, ngapi zimechukuliwa na ngapi zimefanyika, hutakiwi ku-address. Huko tunakotaka kuelekea hilo ndiyo Taifa, dunia ndiko inakoelekea katika masuala ya artificial intelligence. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi bado hatu embrace mifumo wala hatutaki kuitumia, bado tunataka Mungu watu. Maana lazima mtu asimame aseme bwana mimi ndiye kibambe, haiwezekani! Leo tuiachie mifumo ifanye kazi, watu wafanye kazi tuende katika easy of doing business tuwajibike. Ndiyo maana katika Sekta ya Elimu nikasema sana, jamani kuna umuhimu sana vizazi vyetu sisi tukiwemo na wajao, kuna umuhimu wa artificial intelligence. Kazi zitakazokuja baadaye siyo kazi za Mungu mtu, siyo kazi ya kuonekana wewe, ni kazi za maarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu vijana wetu wawe tayari katika hilo Taifa linalokuja baadaye. Uchumi unaokuja, nilizungumza mara nyingi hapa, tulipoanza dunia hii tuliambiwa landlords ndiyo walikuwa wenye pesa, wakaja industrialists, wakaja watu wenye mifumo (ma-ICT), Sasa hivi tunapoelekea ni artificial intelligence, roboti. Taifa letu limejiwekeza wapi? Katika research and development, bado tuko nyuma sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kupitia Bunge lako hili Tukufu Serikali ijielekeze katika suala zima la artificial intelligence na research and development, kwani Mabara yote yanayoendelea duniani sasa hivi na yaliyotajwa yatakayoendelea duniani yamejiwekeza katika digitalisation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache naomba niunge mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Turky kuna mahali ulitamka sarufi, nadhani ulimaanisha sarafu naomba ufanye marekebishio ili Hansard ikae vizuri.
MHE. TOUFIQ S. TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sarafu (currency), ahsante sana. (Makofi)