Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mchango kwenye Bajeti Kuu ya Serikali. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi na afya njema na imempendeza muda huu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mwigulu amekuwa akifanya kazi kubwa na nzuri sana ambapo mambo yote kwenye upande wa Wizara ya Fedha yanakwenda vizuri pamoja na Kaka yangu Naibu Waziri Mheshimiwa Chande wanafanya vizuri sana, nikisema wanafanya vizuri ni pamoja na Wizara yote ya Fedha wanafanya kazi nzuri, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu wanafanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu, nikiwa ni mwakilishi wa wananchi wote wa Mkoa wa Mbeya, nampongeza Kaka yangu Profesa Kitila Mkumbo anafanya kazi nzuri sana. Hotuba yake niliisikiliza vizuri sana imesheheni mambo mazuri ya mipango mingi ambayo Serikali inafanya, nampongeza sana pamoja na Naibu Waziri wake kwa nafasi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi sana nimekuwa nikimshukuru Mwenyezi Mungu kwa ajili Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo Mwenyezi Mungu anaendelea kumpatia macho ya rohoni kwa wateuzi wake wote anaowapa nafasi za kusimamia Serikali yake na kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasimama hapa nikiomba sana Barabara ya njia nne ya Mkoa wa Mbeya na barabara hiyo iko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, barabara hiyo ya kutokea Igawa mpaka Tunduma. Kwa mapenzi mema na makubwa sana ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alisikia maombi ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya, alisimama akaeleza kwamba wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwa kuanzia naomba tuanze na kilomita 29 ambazo zinaanzia Nsalaga mpaka Ifisi, kwa kuliona hili barabara hiyo ambapo Mheshimiwa Rais alisema ianzie, barabara hiyo inapita katikati ya Jiji la Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mapenzi mema hayo ya Mheshimiwa Rais ninachoelewa mimi na wananchi wa Mkoa wa Mbeya Mheshimiwa Rais atakachokisema hayo ni maagizo na hayo ni maelekezo kinachosubiriwa ni utekelezaji. Wananchi wa Mkoa wa Mbeya wanampenda sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na wana mapenzi mema sana naye, lakini sasa sijui ni kwa nini, sijui ni watendaji, sijui ni watumishi, wanataka kumchonganisha Mheshimiwa Rais na wananchi wa Mkoa wa Mbeya, wananchi wa Mkoa wa Mbeya wamemkubali sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba barabara ile imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 138, mpaka sasa zimetolewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 17 ndizo alizopewa mkandarasi, ambapo barabara hiyo mkataba wake ni wa miaka miwili. 14% ndiyo fedha iliyotolewa bado 86. Kati ya hiyo miezi, miezi 16 ndiyo 14% bado miezi nane. Nina wasiwasi na wananchi wa Mkoa wa Mbeya, tuna wasiwasi kwamba je, ndani ya hii miezi nane mkataba unavyoonesha hiyo barabara itakuwa tayari?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kaka yangu hapo Profesa Mkumbo nakuomba mipango yako unayoipanga kuhusu maendeleo ya Taifa hili la Tanzania, naomba sana uelekeze pale Mkoani Mbeya, kwa sababu tunakokwenda sasa tunaelewa kabisa pale barabara zinapotakiwa zipite barabara nne tunaelewa kabisa kwamba pale ndipo Jiji lilipo na Jiji hilo linaeleweka ni Jimbo la nani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, maeneo yale yote tunayoyaongelea, Mbeya ni lango la biashara. Nchi ya Zambia, Malawi na Congo wanategemea sana pale, lakini ukiangalia magari makubwa yote yanayopita kwenda nchi zote jirani na Tanzania magari yale yanapita pale. Ninaiomba sana Wizara ya Fedha tuelekeze kibubu chote cha fedha kwenye barabara zile njia nne za Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapata shida sana wakati tukiwaeleza wananchi na kuwaaminisha, barabara ya njia nne iko kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ambapo tumeambiwa kwamba kufikia 2025 barabara itakuwa imekamilika. Sasa je, kwa mambo kama haya yanavyoendelea kwa fedha zinavyotolewa kidogo kidogo, je, hii barabara itakamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mapenzi makubwa ambayo tunaheshimu kiti na viti alivyonavyo Mheshimiwa Dkt. Tulia, tunaheshimu sana nafasi alizonazo kuwa yeye ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Dunia, lakini sasa pale usoni kwake barabara ile inasuasua sana. Naomba sana barabara ile Serikali iitizame kwa umakini sana ili kuhakikisha inakwenda kufanikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia kwenye Wizara ya Ujenzi majibu niliyopata hapa wananchi wa Mkoa wa Mbeya wakasikia kwamba barabara ile ya Mkoa wa Mbeya kilichokuwa kikiichelewesha ni miundombinu kwa maana kwamba kuhamisha mabomba ya maji, sijui mambo ya umeme na nini. Sasa hivi ile imefanyika na imekuwa tayari, sasa mkandarasi anachoomba ni kuelekezwa fedha za kutosha ili aendelee kufanya kazi aweze kukamilisha barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanyakyusa tabia yao kubwa ni huruma na upendo, ndiyo maana wakipita mahala akasikia kuna msiba anakatisha anaanza kulia kwenye ule msiba, akilia saa nzima anaanza kuuliza aliyekufa hapa ni nani, wakimwambia aliyekufa ni nani anaanza upya msiba mzito. Sasa ule ni msiba wa mtu hata hamfahamu. Sasa wananchi wa Mkoa wa Mbeya wana msiba wao wenyewe, wanalia juu ya barabara, kwa sababu ni tatizo kubwa sana. Unategemea wanalia kiasi gani kwa sababu msiba ule ni wa kwao wenyewe wanalia ndani ya nyumba yao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba hili mlichukulie kwa uzito sana, lakini najua Wizara yote ya Afya, Wizara ya Mipango pamoja na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Serikali yote kwa ujumla inaitazama kwa jicho la huruma na upendo barabara hiyo. Kwa hiyo, tunategemea sana kwamba barabara ile ikamilike kwa wakati kama mkataba unavyoonesha, kwa sababu ya kusema ratiba zote zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya uendeshaji wa ile barabara zimekamilika, sasa ninachotegemea kwamba pale patakwenda kushambuliwa kama mpira wa kona ili kuhakikisha barabara ile inakwenda kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachangia sehemu moja kwenye Wizara ya Habari, kwenye Wizara hii Wilayani Kyela kuna Kata nane ambazo baadhi ya maeneo ukifika kwenye zile Kata unaambiwa tu karibu nchini Malawi, yote hiyo ni kwa sababu ya minara ya kule inaonekana kwamba ni hafifu. Kwa hiyo, naiomba Serikali iweke utaratibu wa kujenga minara kule na Kata zenyewe nazitaja hapa. Kata zenyewe ni Kata ya Matema, Kajunjumele, Ngana, Njisi, Ibanda, Ngonga, Ikimba na Katumba Songwe. Kwa maana hiyo wananchi wanaoishi maeneo yale hawaweki vocha kupitia huku kwetu Tanzania, ina maana vocha wananunua za kule. Mapato inapata nchi nyingine wakati wao ni Watanzania na mapato hayo yanatakiwa yaingie kwenye Taifa letu hili la Tanzania. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali iliangalie hili.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma Ikenda samahani, Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, taarifa.
TAARIFA
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, anachokisema ni sahihi kabisa. Siyo tu kwamba wananunua vocha za Malawi, pia wanasikiliza Redio Malawi kwa sababu tayari kila kitu kinakuwa nje. Kwa hiyo, tunaomba waliangalie kwa umakini. Anachokisema nakiunga mkono na nakisisitiza zaidi.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Suma Ikenda, unaipokea taarifa ya Mheshimiwa Sophia Mwakagenda?
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo kwa mikono miwili. Nakushukuru sana Mheshimiwa Sophia kwa taarifa hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, kwa hiyo nchi yetu ya Tanzania wananchi wale ambao wanaishi kwenye hizo Kata kule Wilayani Kyela wanakwama kabisa kusikiliza wakati fulani hata taarifa ya habari ya Taifa lao la Tanzania kwa maana muda wote wanasikiliza Redio Malawi, nitashukuru sana kwenye hili kama wamelifanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni pale ambapo wakandarasi wa Taifa hili la Tanzania wanafanya kazi kwa kujitoa sana wanapokuwa wamekabidhiwa mikataba katika kazi zao maana mikataba inawaamuru wafanye kazi kwa wakati, lakini wakimaliza kufanya kazi kwa wakati hawalipwi kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakandarasi wengi sana, wazabuni na ¬suppliers wa Taifa hili la Tanzania wakipewa order ama wakapewa kazi ya kufanya, siyo kwamba wanapewa advance kwanza Serikali, wao wanachukua jukumu, wengine wana mitaji, lakini katika mitaji hiyo wanatakiwa wazungushe, lakini walio wengi wanakwenda kukopa fedha benki ili waendeshe kazi hizo wakitegemea kulipwa, matokeo yake hawalipwi kwa wakati na hatimaye wanakwenda kuuziwa dhamana zao na watu hao hao wanakwenda kupata stroke kwa ajili ya mshtuko na wengine wanapoteza maisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mtu kwa sababu alikuwa ameweka dhamana nyumba anayoishi lakini inakwenda kupigwa mnada, anaanza kwenda kupanga, matokeo yake anapigwa stroke na wengine wanapoteza maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hilo hilo hapo, kinachoonekana ni kwamba mkandarasi huyu ama mzabuni ama supplier kama hajafanya kwa wakati, Serikali inampiga penalty aanze kuilipa Serikali, lakini mkandarasi huyu ama supplier na mzabuni wao wakicheleweshewa fedha zao hakuna chochote ambacho wanapewa kwamba ni nyongeza zaidi ama kwamba wataifanyia sasa kwenye ule mpango kwamba na sisi sasa hivi tuanze kulipwa fidia ya kucheleweshewa fedha zetu. Kama ali-supply vifaa miaka mitano iliyopita au miaka 10 matokeo yake anakwama, anaanguka mtaji na anapata shida sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, namwomba sana kaka yangu, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu na kaka yangu Mheshimiwa Prof. Kitila, wanapokuja hapa kuhitimisha watuambie sana wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuhusu ile barabara wana mpango gani na barabara ya Mbeya Jiji? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka majibu hayo yatukolee sana, yasiwe ya juu juu tu. Yawe ya uhakika kwamba barabara ile ya njia nne ambayo tunaiongelea kila siku, mambo hayaendi kama inavyotakiwa. Kila wakati barabara ile imeleta shida, ni kwamba haina hata service road, tunapita sehemu moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Waziri Prof. Kitila wanapokuja hapa ku-wind-up watuambie wananchi wa Mkoa wa Mbeya kitakachoendelea juu ya barabara ile ya wananchi wa Mkoa wa Mbeya tunayopiga kelele kila siku ukizingatia nimepata ajali juzi, wiki mbili zilizopita wamekufa watu wengi sana kwenye ile barabara. Magari matatu yamegongana kwa sababu ya ufinyu wa barabara…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
(Hapa Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wamekufa na wengine wamebaki walemavu. Tafadhali sana, nakushukuru sana kwa nafasi. Naomba kuwasilisha, na ninaunga mkono hoja kwa 100%. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana. Kwa ajili ya Hansard, nafikiri Mheshimiwa Suma Ikenda alipotamka Wizara ya Afya alimaanisha Wizara ya Fedha.
Nadhani ndivyo hivyo, Mheshimiwa Suma?
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ulimi uliteleza, ninaongelea Wizara ya Ujenzi, lakini tunaongelea hapa Wizara ya Fedha ambayo ndiyo imeshika kihenge chote cha nchi hii ya Tanzania. (Makofi)