Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi. Jambo la kwanza, nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio na kazi kubwa ambazo anazifanya katika nchi yetu. Tunampongeza sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wote kwa kazi kubwa mnazoendelea kuzifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nawapongeza Mawaziri wawili; Waziri wa Fedha na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, kwa hotuba nzuri ambazo wameziwasilisha humu Bungeni. Pia, nawapongeza watumishi wa Wizara hizi mbili na taasisi zote zilizoko chini ya hizi Wizara. Zaidi ya hapo tunaipongeza Kamati ya Bajeti kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kuchambua bajeti hii na mipango hii, mmeifanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua na katika kuchagua lazima uangalie unachagua nini na kwa wakati gani? Katika kipindi tulichonacho, tunayo matatizo ya msingi ambayo mipango yetu lazima iende kujibu hoja hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mambo yanayotusibu katika nchi hii ni pamoja na ukosefu wa ajira kwa vijana wetu. Tatizo la ajira ni kubwa na tatizo hili lazima mipango hii tuonyeshe tunavyoenda kulitatua na tuwe na mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la pili tulilonalo ni umaskini mkubwa ambao wananchi wanao katika nchi ambayo ni tajiri sana. Tatizo la tatu ni uchumi mdogo tulionao katika rasilimali nyingi zilizopo katika nchi yetu. Tatizo la nne ni tija ndogo katika maeneo mbalimbali, na la tano ni ujinga na teknolojia duni tunazotumia katika uzalishaji na mambo mengine mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kabisa bajeti yetu na mipango yetu lazima ijielekeze katika kujibu hoja hizi. Tukitatua hizi ndiyo tutaweza kuijenga nchi yetu, tutaweza kuwasaidia wananchi wetu na nchi itapiga hatua kubwa. Sasa, ukipitia bajeti ya leo ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, inatuonyesha sura ifuatayo:-)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, mapato ya ndani ya TRA ni shilingi trilioni 29.4, mapato yasiyo ya kikodi ni shilingi trilioni 3.8, mapato ya halmashauri ni shilingi trilioni 1.3. Jumla ya mapato yote ya ndani ni shilingi trilioni 34.5, sawa na 70% ya bajeti nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inaashiria nini? Maana yake ukichukua bajeti yetu yote ya shilingi trilioni 49, shilingi trilioni 34 tu ndiyo tuna uwezo wa kuzikusanya na kuzizalisha wenyewe. Kwa hiyo, fedha nyingine lazima zitoke kwenye misaada na mikopo. Sasa bajeti inatuambia mikopo na misaada ni shilingi trilioni 14.7 ambapo mikopo ya ndani ni shilingi trilioni 6.5 na mikopo ya nje ni shilingi trilioni 8.2. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya maendeleo ya nchi yetu ni shilingi trilioni 11.1. Hii maana yake ni nini? Kama bajeti ya maendeleo ya nchi yetu ni shilingi trilioni 11 na bajeti ya mikopo na misaada ni shilingi trilioni 14 na mapato ni shilingi trilioni 34, maana yake katika bajeti hii mapato yetu ya ndani hayatoshelezi na hayawezi kwenda kutumika kuwekeza katika miradi mbalimbali tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake bajeti ya kwetu sasa hivi ya maendeleo lazima ni bajeti tegemezi. Maana yake tukikosa hiyo misaada, tusipokuwa na mikopo, maana yake hatutaweza kutekeleza mradi hata mmoja wa maendeleo. Sasa hii maana yake nini? Ni kwamba kwa wale wanaosema hatutakiwi kukopa, maana yake tusimamishe miradi yote ya maendeleo, na hii nchi hatuwezi kufanya hivyo. Sana sana, sasa hivi lazima tukope tukawekeze kwenye miradi hii ya maendeleo, lakini tuwe na muda kwamba ikifika kipindi fulani sasa tujitegemee. Kwa hiyo, lazima sasa tuache kukopa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake kujitawala ni kujitegemea na ili tufike kujitegemea ni lazima tukope, tuwekeze, na tuzalishe. Tukizalisha sasa, tuanze kujitegemea. Kwa hiyo, nadhani kwa msingi wa bajeti hii, lazima tuendelee kupata misaada na mikopo, lakini tuielekeze kwenye sekta za uzalishaji zitakazoweza kujenga uchumi imara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia hii bajeti, mchango wa taasisi za umma yaani mashirika ya umma na taasisi mbalimbali, zinachangia shilingi trilioni tatu tu. Nimeangalia, wameweka ile ruzuku au gawio tunalolipata. Sasa, bajeti zao zile wanazozizalisha, fedha zote wanazozalisha mashirika ya umma na taasisi za umma hazipo kwenye hii Bajeti Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri model inayotumika katika kupanga hizi bajeti, sasa Waheshimiwa Mawaziri wangu wawili wapendwa, mwangalie ile model ili tuweze ku-capture mapato yote yanayozalishwa na taasisi za umma yaingie kwenye Bajeti Kuu, ije hapa na Bunge liwe na mamlaka ya kuidhinisha hizo bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hivi bajeti za mashirika ya umma haziidhinishwi na hazipitishwi na Bunge hili. Hii ni kinyume kidogo. Kwa hiyo, nafikiri umefika wakati tuangalie ile model ili bajeti ya TANESCO, Bandari, TTCL, mashirika mbalimbali zije hapa Bungeni iwe ni sehemu ya Bajeti Kuu na mapato yataweza kuongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sisi kule Mbozi tunahitaji maendeleo na tunahitaji vitu vingi kwa sababu ni mkoa wa wakulima na ni wilaya ya wakulima. Kuna vihenge vilianza kujengwa vikaishia katikati havijakamilika. Vile vihenge ni muhimu sana kwa kuhifadhi chakula. Tunaomba Serikali mvimalizie vile vihenge vianze kufanya kazi kwa sababu vilikuwa vimefika 85%. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba Barabara ya Londoni – Iganduka – Msia – Isalala, Barabara ya Ihanda – Ipunga – Chindi, Barabara ya Chimbuya – Ludewa, Barabara ya kutoka Mahenje – Kimondo – Hasanga na barabara nyingine ni muhimu sana zikapewa fedha ili kusudi ziweze kuchangia katika mendeleo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nchi iweze Kwenda, tunahitaji import substitution na tunahitaji tuweze kutatua changamoto tulizonazo. Nini tukifanye? Kitu cha kwanza, tuwekeze fedha nyingi katika sekta za uzalishaji na ninawapongeza mmeweka fedha nyingi kwenye sekta za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona kilimo kilivyopewa fedha nyingi, tunaona uvuvi ilivyopewa fedha nyingi, mifugo ilivyopewa fedha nyingi. Kikubwa Mheshimiwa Dkt. Mwigulu peleka hizo fedha zikazalishe zaidi, zisimamiwe vizuri na ziongeze uzalishaji kwenye nchi hii. Hapo nchi tutaweza kupiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuanza kutafuta mazao ambayo tutayazalisha hapa na bidhaa ambazo zinachukua fedha zetu za kigeni kwa wingi ambazo tunaagiza nje. Kwa mfano, mafuta ya kula yanatumia shilingi bilioni nyingi sana za hela za Tanzania kwenda kuagiza nje. Nchi yetu tulipofika hatuhitaji kuagiza mafuta kutoka nje. Tunahitaji mafuta ya kula, tuzalishe hapa alizeti kwa wingi, tuchakate na kuhakikisha kwamba tunapata mafuta ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuongeza uzalishaji wa kilimo cha miwa ili tuzalishe sukari yetu hapa hapa nchini. Hatuhitaji, nchi ndogo kama ya Uganda, siyo vizuri ikatushinda kuwa na utoshelevu wa sukari kuliko nchi ya Tanzania ambayo ni tajiri sana kwa ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kujitosheleza kwa chakula lakini zaidi ya hapo tunahitaji mfuko wa kuchochea viwanda na ujenzi wa viwanda. Nilisema na nitaendelea kusema, bila kuwa na mfuko wa ujenzi wa viwanda, hapa tutaimba tu kujenga viwanda. Viwanda ndiyo vitatusaidia kupunguza tatizo la ajira, ndiyo tutazalisha bidhaa za kwetu za kwenda kushindana katika soko la dunia. Kwa hiyo, lazima tuwekeze, tujenge miundombinu, Serikali iweke fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuimarisha miundombinu mbalimbali kama ile ya bandari, TAZARA na SGR. Miundombinu hii ni msingi mkubwa wa maendeleo ya nchi yetu. Uwekezaji lazima uendelee na ndiyo maana nimesema lazima tuendelee kukopa lakini tunahitaji pia kuimarisha maslahi ya watumishi wa umma ili waweze kufanya kazi kwa weledi, tija, kujituma na waweze kuchangia na kuwa wabunifu zaidi kusudi nchi iweze kupiga hatua kubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kukuza Sekta Binafsi. Sekta binafsi lazima iwe supported. Hii ndiyo msingi wa kulipa kodi, na hii ndiyo itakayokuwa mhimili wa kujenga uchumi wetu na Watanzania walio wengi walioko kwenye sekta binafsi. Hata kilimo tunachosema ni sekta binafsi, lazima kiwe supported, waweze kuchangia katika uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tunahitaji kuanzisha Baraza la Tija. Baraza la Tija litatusaidia kuongeza tija kwenye kilimo, viwanda na maeneo mengine. Tuliliondoa siku nyingi, nami naendelea kulisema kwamba Baraza la Tija ni muhimu sana katika kuweza kuchochea maendeleo ya nchi yetu. Tunahitaji kuongeza jitihada katika kutangaza utalii na miundombinu yote iliyopo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya pamoja na mambo mengine yote, eneo kama la kule Songwe, Tunduma pale bandari kavu tunahitaji ile iimarishwe na uwekezaji uwe mkubwa. Nchi za SADC na nchi za huko kusini mwa Afrika zije kununua bidhaa mbalimbali pale. Pale Dar es Salaam tuimarishe tuwe na maduka makubwa. Wale badala ya kwenda China, waje Tanzania wachukue, tufanye biashara na hapo ndipo nchi yetu itaweza kupiga hatua na tutaweza kukusanya kodi na tutaongeza wigo wa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa nafasi. Naunga mkono hoja na ninawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri wanayoifanya, ahsante sana. (Makofi)