Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Dr. Jasson Samson Rweikiza

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukoba Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. DKT. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niseme kidogo kwenye hii Bajeti Kuu ya Serikali, niweke mchango wangu. Awali ya yote napenda kuipongeza Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwanza yeye mwenyewe kwa kazi kubwa anayoifanya, Serikali yake yote na wasaidizi wake wote kwa kuzidi kuboresha maslahi na ustawi wa Tanzania, nampa heko sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu, leo ningependa kuzungumzia jinsi ambavyo nafikiria ni njia gani ambayo itasaidia nchi yetu kuongeza viwanda au kuwa nchi ya viwanda. Nimemsikia Mheshimiwa Hasunga hapa amesema kwamba uchumi wetu tukitaka uimarike, tuwe na viwanda vingi na tuongeze viwanda, ni sahihi kabisa. Kwa hiyo, mchango wangu unajikita hapo kuhusu jambo hili la kuongeza uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia bajeti na mpango tunazungumzia maslahi ya Watanzania kuboresha ustawi na ufanisi wa maisha iweze kuwa himilivu na nzuri zaidi. Sasa ukiangalia kwa ujumla katika nchi yetu huduma zinazidi kuboreka; usafiri, mabasi yanakuwa mazuri. Juzi tumefungua reli ya kisasa imeanza kazi, huduma ya petrol stations (vituo vya mafuta ya magari na mafuta mengine maarufu sheli) kujenga hoteli na guest houses; huduma zinazidi kuimarika na kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2023 katikati nilifanya utundu kidogo, nilikuwa naelekea Dar es Salaam, nikahesabu petrol stations (hizi sheli) kuanzia Chalinze hadi Kibaha Maili Moja, nilipata sheli 68. Pale kuna kilomita 75, sheli 68 na leo nafikiri zimeshafika 100 na zaidi maana yake wanajenga kila siku. Ukipita unaangalia kushoto na kulia wanajenga, sheli zinazidi kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kujenga sheli moja kwa makadirio yangu nafikiri inaweza kugharimu shilingi bilioni moja. Ununue ardhi ambayo iko barabarani siyo hela ndogo, upate kiwanja cha ekari moja au mbili ni pesa nyingi. Uweke matenki yale na pumps chini ya ardhi na juu yapande matenki na pumps ni hela nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenge nyumba zile, ofisi, wengine maduka ya vyakula, restaurants, huduma za magari, service na kadhalika; ni hela nyingi kujenga nyumba zile. Kuweka zege au pavements kusudi ardhi isiwe ya matope pale, kwa hiyo, ni gharama kubwa, ikiwa ndogo nafikiri ni shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa urefu ule wa kilomita 75, sheli 100 ni za nini? Wanagombania magari, magari yakija wale wahudumu wanakimbia, njoo huku! Njoo huku! Wanashindania magari kwa sababu hawana wateja wa kutosha. Zingejengwa 10 pale zingetosha kuanzia Chalinze mpaka Kibaha Maili Moja pale zingetosha kabisa na watu wangeuza wale wenye sheli zao zile, wasingeshindania magari, na biashara ingekuwa nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyumba ya wageni moja, (guest house) kuijenga ndogo kabisa labda ya vyumba 10, au vyumba 20, unaongelea shilingi milioni 100 au shilingi milioni 150 kwa uchache; lakini unakuta kuna wageni wanaokuja pale kwa siku ni wawili tu, au mmoja, au sifuri, hatupati wateja kwa sababu zipo nyingi sana kuliko mahitaji ya wageni. Kwa hiyo, pale kwenye sheli, labda guest house 20, tano zingetosha, au nne, au mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikisema haya, naweka msingi wa kusema yafuatayo; kwamba, Mheshimiwa Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Uwekezaji, tumemsikia juzi hapa akielezea hotuba yake, nafikiri kwenye Wizara yake, TIC kile Kituo cha Uwekezaji, kinafanya kazi nzuri, tunakipongeza. Kusajili miradi, lakini zaidi zaidi naona kama kinasaidia sana kuleta miradi ya nje, wawekezaji kutoka nje, kujenga viwanda vya cement, akina Dangote, akina Twiga wale, watu wa nje, na kampuni kubwa. Viwanda vya tiles Mkuranga kule na Chalinze, vya Wachina kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri TIC iwe na kitengo pale ndani cha kuhamasisha viwanda vya wazawa. Sasa, ichoronge kiwanda kwenye makaratasi, siyo kwenye kukijenga; kwenye makaratasi. Iandike mradi wa kiwanda, tuchukulie labda kiwanda cha matairi ya pikipiki ambazo ziko nyingi sana, hivyo soko lipo. Kiwanda cha matairi ya pikipiki, iainishe mahitaji ya mtaji, iainishe mahitaji ya malighafi (raw materials), iainishe mahitaji ya uendeshaji, Meneja, Wahasibu na Wanasheria na nani wa kuendesha kile kiwanda. Iainishe ardhi itapatikana wapi? Labda heka mbili, heka moja, heka tatu, yaani vyote vikamilishe kwenye maandishi, iwe mradi umebuniwa, umekamilika. Baada ya hapo, itangaze kwamba tumebuni mradi wa kiwanda cha matairi ya pikipiki chenye thamani labda ya shilingi bilioni 100. Shilingi bilioni 100 ni sheli 100 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hao hao ambao ungewaweka kwenye sheli, kwa sababu hawana pa kuwekeza hela yao; mtu ana hela yake ya mtaji, anaona bora aende kwenye sheli, awekeze apate hela kidogo kidogo kuliko kukaa nazo akazitumia. Kwa hiyo, watakapokuja kununua hisa kwenye kiwanda ambacho kimebuniwa na TIC, watanunua hisa, watawekeza. Hiyo TIC isimamie, wabainishe utawala, watangaze kazi. Vijana wapo wengi wenye uwezo waliosomea mambo ya utawala, biashara, uhasibu na fani nyingine, waainishwe, waonekane kwamba wapo. Watangaze wauze hisa. Watakuja watu watanunua hisa halafu waanzishe kiwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo hivyo na wa guest house, na wa bodaboda, na miradi mingine ya huduma watahamia kwenye viwanda, vitakuwa vingi na tutakuwa tumetatua tatizo la ajira kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengine wamesema, kupunguza shida ya ajira kwa vijana wetu na kuongeza uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko yapo kama nilivyosema. Nchi hii ina pikipiki sijui milioni ngapi, matairi kwa siku yanakwenda sijui mia ngapi au elfu ngapi? Tukiwa na kiwanda cha matairi, watauza vizuri vijana, viwanda vitauza vizuri. Tukishindwa kuuza hapa, siyo kushindwa, hata nje kuna masoko, utauza Uganda, utauza Rwanda, utauza Malawi, na kadhalika. Masoko yapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kiwanda cha samani (furniture), tutauza kote tunakotaka kuuza, material zipo, mbao zipo nchini hapa, watu watapata tija kubwa sana ya fedha zao. Kiwanda cha Ngozi labda viatu au mabegi, ngozi zipo, raw material zipo nyingi na wataalamu wapo. Naomba sana kitengo cha kuhamasisha viwanda kwa wazawa chini ya TIC, kianzishwe na kiratibu utaratibu huu ambao utasaidia sana kuongeza uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)