Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenijalia uzima nami kuweza kutoa mchango wangu katika hii Bajeti Kuu ya Serikali. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya katika nchi yetu hususan katika Jimbo la Kilolo, kwa mambo makubwa na miradi mingi ambayo tunaendelea kuipokea na Wanakilolo wanamshukuru sana, kazi yake wanaiona na wanaendelea kujiandaa kwa ajili ya kutoa malipo 2025. Inshallah Mwenyezi Mungu ajaalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nawashukuru sana Waheshimiwa Mawaziri na Waheshimiwa Manaibu Mawaziri, Wizara ya Fedha na pia Wizara ya Mipango. Kwa upande wa Wizara ya Fedha, kwa ushirikiano mkubwa ambao tunaupata hasa katika utengaji wa fedha na utoaji wa fedha. Tumepokea fedha nyingi sana za miradi na tunajua hii ni kazi nzuri ya Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri wake. Sisi Wanakilolo tunawashukuru na kuwapongeza sana, kazi yao tunaiona na Mwenyezi Mungu awajaalie waendelee kufanya kazi hiyo kwa uaminifu na uadilifu kwa ajili ya wananchi wa Tanzania pia kwa ajili ya wananchi wa Kilolo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Naibu wake kwamba wameanza vizuri, na sisi tupo tunaendelea kuwaangalia na kuwashauri kwa mambo machache yale ambayo tunaamini yatatoa mchango katika ujenzi wa Taifa letu. Siku hii ya leo, pamoja na shukrani na pongezi hizi, ninayo michango michache ninayoweza kushauri katika Bajeti Kuu. Jambo la kwanza kwa Waheshimiwa Mawaziri, ni kuhusu utaratibu wa ukusanyaji wa mapato kwa mazao ya misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inajulikana wazi kwamba Mkoa wa Iringa ndiyo unaotoa mazao ya misitu ya kupandwa hasa mbao nyingi kuliko mikoa mingine mingi hapa nchini na wananchi wa Wilaya kama ya Mufindi na Wilaya ya Kilolo, hawana shida na ulipaji kodi. Wanapenda kulipa kodi na wasingependa kuingia kwenye migogoro na Serikali kuhusu ulipaji wa kodi hasa za mazao ya misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo haiwezekani hii nchi kila anayezalisha mbao kuwa na mashine ya EFD, haiwezekani. Wazalishaji wa mazao ya misitu ni wazalishaji wadogo wadogo; mtu anajichangachanga, ananunua mashine, anaenda msituni, anachana mbao, anaweza akajaza gari moja au magari mawili, anaanza kupeleka sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, ili tusilete udanganyifu wa wale wakulima, wanapokuwa wameshajaza gari, kuanza kumtafuta mwenye risiti ili wanunue risiti, badala ya wao kutoa risiti halali, ni vizuri mikoa inayozalisha mazao ya misitu, wale Mameneja wa TRA wa Mikoa na wa Wilaya, wakakaa vizuri na kuelekezana namna bora ya ukusanyaji kodi kwa mazao ya misitu bila kusababisha biashara haramu ya risiti ambayo inaleta usumbufu mkubwa na kusababisha udanganyifu ambao hauna tija yoyote kwa mkulima, wala kwa Serikali, wala kwa mtu mwingine yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana pia Waheshimiwa Mawaziri hawa waagize Wizara zao kufanyia kazi haraka kwa sababu inatakiwa kuondoa ile kero ya wale wafanyabiashara haraka iwezekanavyo. Hili linawezekana kufanya majadiliano kwa sababu hamna aliyekataa kulipa kodi. Kwa mfano, gari kumi zinakamatwa, maana yake mwenye gari amekamatwa na gari yake haifanyi kazi. Wakati huo huo mwenye biashara amekamatwa, biashara yake imesimama. Hatuendelezi biashara, lakini hapo tunakwamisha tu uchumi na wale wafanyabiashara wa mbao wanapata shida, wafanyabiashara wa magari wanapata shida na hao wote hakuna hata mmoja aliyekataa kulipa kodi, bali ni utaratibu ambao hautekelezeki uliowekwa kwamba kila anayepakia gari ya mbao, awe na mashine ya EFD kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linawakera sana wananchi wa Wilaya ya Kilolo, Mufindi, wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao wanafanya biashara ya mbao. Hii ni kero ya muda mrefu na tumeshalizungumza sana hapa Bungeni. Tunaomba lifanyiwe kazi ili liondoke, na kama kuna suala na utaratibu mzuri wa kodi, uwekwe ili jambo hili liweze kuondoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia hili na ninaamini kabisa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Mipango pale wamenisikia, sasa naenda kwenye suala lingine linalohusu uwekezaji kwenye viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza hapa na kumekuwa na majadiliano mengi ya changamoto. Natoa mfano mmoja wa changamoto ya sukari na asubuhi hapa limejibiwa swali kwamba Wilaya ya Kilolo ina eneo la hekta 10,000 zinazoweza kupandwa miwa. Wakati huo huo, tunavyo vyombo au mashirika ya Serikali ambayo yameshajitolea kutengeneza mitambo midogo ya kuzalisha sukari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamka hapa TEMDO ambayo ipo Serikalini, sasa, kama tusipowekeza kwenye kuhakikisha kwamba TEMDO inawezeshwa ili kuzalisha ile mitambo ya kuchakata sukari ili wale wakulima wadogo wapate hii mitambo midogo midogo, maana yake tunaendelea kuvutia uingizaji mwingi wa sukari na kwenye uchumi tunaondoa ile dhana ya balance of payment kwa sababu sisi tutanunua sukari nyingi, lakini wakati huo huo tuna uwezo wa kuzalisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Wizara ya Mipango, ni kuangalia hizi taasisi ambazo zinajihusisha na uzalishaji wa mitambo. Nimetoa mfano wa kiwanda cha sukari na mitambo yake, lakini, pale TEMDO pia wanazalisha vitanda. Vitanda vile ni kwa ajili ya hospitali. Sasa ukienda kwenye bajeti ya mwaka 2023, tumenunua vitanda vingi sana vya hospitalini kutoka nje ya nchi na TEMDO wanazalisha vitanda hapa hapa nchini ambapo tusingetoa dola kwenda nje, tungeweza kuwawezesha TEMDO wakazalisha vile vitanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TEMDO ni ya Serikali, Serikali hiyo hiyo ndiyo ambayo imenunua nje wakati TEMDO iko pale na pengine uzalishaji wao wa vitanda ni vichache kwa sababu hatukuweza kuwawezesha kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango yetu, tuangalie hizi taasisi zinazojihusisha na ubunifu na uzalishaji wa mitambo ili ziwezeshwe kupunguza uagizaji wa bidhaa nje, halafu sisi tuzalishe wenyewe ili tuweze kuimarisha uchumi wetu. Kwa hiyo, mimi nimetoa mfano mmoja wa TEMDO, lakini ziko SIDO na taasisi nyingine na hizi zinafanya kazi nzuri kama zitawezeshwa, lakini zisipowezeshwa, ndiyo wanaweza kuzalisha vitanda kumi au mashine moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo mashine kwa mfano ya kupeleka Kilolo kwa ajili ya kujaribu uzalishaji wa sukari, bado hadi leo haijakamilika. Ni moja hiyo kwa sababu ya uwezeshwaji wa kiuchumi. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, aipe TEMDO fedha izalishe. Ule mtambo wa kuzalishia sukari, ukafungwe pale Kilolo ili tuujaribu tuone kama unafanya kazi vizuri ili na maeneo mengine ambayo wanataka kutengeneza sukari kwa viwanda vidogo, waanze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutoe mfano huo. Mimi sijajua wanahitaji kiasi gani, lakini wakimletea Mheshimiwa Waziri, basi atoe hiyo fedha tukajaribishe ule mtambo naye mwenyewe pia ataona kwamba kuna manufaa kwa sababu tukitoa dola nje, tunapata hasara zaidi kuliko tukiwa tunazalisha ndani na dola zinabaki kwa ajili ya manunuzi. Kwa hiyo, tunakuwa na urari wa malipo ambao ni mzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia hili, nazungumzia suala lingine kuhusu dharura. Hivi karibuni kuna mvua nyingi sana zimenyesha na sisi wote tumeathirika. Nina hakika hata Waheshimiwa Mawaziri wote waliokaa pale ni Wabunge wa Majimbo na huko kwao mvua zimenyesha, maana mvua hazikuchagua kwamba huku ni kwa Mheshimiwa Waziri wa Mipango, wala huku ni kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha, mvua zilinyesha nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya zile mvua kwisha, tumepata madhara makubwa sana ya uharibifu wa barabara. Tunapozungumzia dharura, maana yake ni dharura. Madaraja yakivunjika, maana yake watu hawapati huduma. Tunapozungumzia dharura, maana yake ni kwamba mazao yanaoza. Kuna watu wana mazao yao, walikopa, wanataka wasafirishe wakalipe madeni yao benki. Hadi hivi tunavyozungumza, bado fedha za dharura kwenye maeneo mengi kwa ajili ya barabara, hazijaenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunapofanya hivi, wakati wa bajeti, inabidi tuangalie. Tunaweza tukamlaumu Mheshimiwa Waziri wa Fedha, lakini sisi hapa kama Wabunge, na kama Taifa, ni lazima tuwe na utaratibu na mfuko maalum wa majanga yanapotokea, ili tunapompigia simu Mheshimiwa Jenista kwamba huku kuna janga na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wajue hiyo hela wanatoa wapi ili sisi kule tuweze kukubaliana na madhara kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hilo hatujalifanyia kazi, basi maana yake ni kwamba, hizi barabara itabidi zisubiri bajeti ya kawaida ambapo maana ya maafa, wala maana ya majanga haitakuwepo. Kwa hiyo, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri wa Mipango pamoja na Serikali kwa ujumla, ni kwamba, sasa tuanze kuangalia fedha za dharura zinatoka wapi? Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea, kwa hiyo, tutaendelea kupiga simu kwamba huku kuna dharura, lakini je, fedha hizo za maafa hayo tunazitoa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza, bado kuna kata karibu nne mpaka leo barabara hazipitiki, wananchi hawawezi kusafiri kwa sababu fedha haijaenda. Nikienda TARURA, watasema hatujapokea fedha kutoka Serikalini ambazo nami nikikaa nikitafakari, naanza sasa kuangalia, je, Mheshimiwa Waziri anazo hizo fedha? Kwa hiyo, naomba sana, kwa hii dharura iliyotokea, tufanye lolote linalowezekana fedha zipatikane huku tukiendelea kujadili kwamba tutapata wapi fedha za dharura kwenye miaka ijayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni kuweka mfuko wa dharura, mfuko huo uwekwe ili wakati mwingine tusipate shida tunapopata madhara kwenye maeneo yetu, kwa sababu hicho ni kitu ambacho tunaweza tukakitabiri. Ndiyo maana tumeweka utabiri wa hali ya hewa na watabiri wengine wanaoweza kutabiri madhara. Sasa, yanapotokea, lazima tujue kinachoitwa dharura ni dharura. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha akipokea simu ya dharura, anakaa siku ya kwanza, ya pili, ya tatu, mwezi, yeye mwenyewe anajua ni dharura, huwa anajisikiaje? Lakini pengine hana cha kufanya kutokana na kutokuwepo kwa fedha. Kwa hiyo, lazima hili sisi kama nchi na kama Bunge, tulifanyie kazi ili yale maeneo ambayo yana changamoto yaweze kutatuliwa kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumzia kidogo jambo moja ambalo Wizara ya Kilimo inaweza kulirekebisha, lakini na nyie mnaweza kuliangalia. Tunazungumzia sana kuhusu mazao mbalimbali na jinsi ambavyo tunatoa unafuu, na hapa nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa ajili ya ruzuku ya mbolea. Ruzuku ya mbolea imesaidia sana kwenye hii nchi hasa kwenye sisi ambao ni wakulima, tunajua manufaa ya ruzuku ya mbolea ambayo kama bei yake ingekuwa bila ruzuku, wakulima wengi sana wasingemudu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna jambo moja kwenye baadhi ya mazao, tunahitaji kuwa na tathmini ya kutosha. Mfano, mazao ya parachichi ambayo sasa hivi yanaendelea kulimwa kwenye mikoa ya Njombe, Iringa na maeneo mengine. Bado wakati tunatoa bure miche ya michikichi, miche ya kahawa na miche ya mazao mengine, bado miche ya parachichi inauzwa tena kwa bei kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko mipango na TARI wameshaifanya kwa ajili ya ruzuku kwenye miche ya parachichi. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, suala hilo lifanyiwe kazi na kwenye bajeti hizi, kama zipo fedha zitakazowekwa kwa ajili ya ruzuku, basi ruzuku kwa ajili ya miche ya parachichi iweze kuangaliwa, na tutakapofanya hivyo, tutaona kile kilimo kinakua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, huko tunakoenda, uvunaji wa parachichi unaendelea kwa kiwango kikubwa. Wizara na Idara mbalimbali za Serikali zimekuwa zikija hapa kuelezea mipango jinsi walivyojipanga kwa ajili ya masoko ya zao la parachichi. Ni wakati muafaka sasa kuhakikisha kwamba upo mpango maalum wa kuwa-link au kuwaunganisha wakulima na masoko ya parachichi ili kusiwe na mkulima anapoteza mazao ya parachichi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuharakisha ujenzi wa viwanda vya parachichi. Kwa Mkoa wa Iringa, najua kwamba kuna bajeti wa ajili ya kujenga kiwanda cha parachichi pale Nyororo Mufindi. Kwa hiyo, hicho kingeweza kusaidia mkoa mzima wa Iringa lakini pia na mkoa mzima wa Njombe kwenye hayo maeneo. Hilo nalo liangaliwe kwa haraka ili tusipoteze mazao haya, lakini ili tuendelee kuwatia moyo wakulima wa parachichi ambao wanaendelea kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, Mheshimiwa Waziri, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, kuna jambo wakati tunaendelea, tuliliangalia na tuliona linaweza likawa ni fursa ambayo haitumiki vizuri. Ni suala la uelewa wa halmashauri zetu kuhusu CSR (Cooperate Social Responsibility). Mashirika mengi yalioko kwenye maeneo yetu, hayatoi CSR kwenye halmashauri zetu, au kama yanatoa, hayatoi kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo tunapoteza mapato mengi kwa sababu CSR siyo hisani. Baadhi ya Wakurugenzi au maeneo mengi wanafikiri ni hisani kwamba mtu anatakiwa atoe CSR kwa hiari. Kwa kuwa ile ni sheria na ilipitishwa hapa Bungeni, ni wakati muafaka sasa wa kuwahamasisha na kuwapa maelekezo Wakurugenzi wote na wale wote wanaosimamia, kuhakikisha kwamba kila taasisi ya kibiashara inatoa CSR kwenye halmashauri husika na hapo itakusaidia Mheshimiwa Waziri, kupunguza kupeleka fedha kwa sababu kama CSR itatumika kujenga shule, maana yake tayari hapo bajeti ya Serikali imeokolewa. Kama CSR itatumika kujenga zahanati, maana yake hapo bajeti ya Serikali imeokolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ufuatiliaji wetu kwenye Kamati, tuliona jinsi ambavyo kuna fedha nyingi sana inapotea kwenye eneo la CSR. Ushauri wangu ni kwamba tuendelee kuangalia hilo eneo kwa sababu ni chanzo kizuri cha mapato na tunaweza kujenga nchi yetu kupitia hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsanteni sana na Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)