Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kunifanya niwe mchangiaji wa kwanza kwenye session hii ya jioni. Kwanza kabisa naunga mkono hoja, lakini kwa kuwa mimi ni mkulima na Jimbo la Mbinga Vijijini na wananchi wangu ni wakulima, naanza mchango wangu kwa kuishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi hiki chote kukifanya kilimo ni kipaumbele kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona kipindi hiki ndipo tuliposhuhudia bajeti kubwa ya Serikali kutoka shilingi bilioni 294 mpaka kufikia bajeti hii ya shilingi trilioni moja na zaidi, lakini kipindi hiki ndicho tulipoona mbolea ya ruzuku inapatikana, kipindi hiki ndicho tulipoona wakulima wetu wanatumia mbegu bora na za kisasa karibu kwenye kila zao. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa kujitoa kimasomaso kweli kweli kwenye sekta hii ya kilimo na kuonesha sasa tunaweza kuona matunda ya uwekezaji huu mkubwa yanaonekana kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha inasema hapa kilimo kimetutoa kutoka shilingi bilioni 2.4 mpaka shilingi bilioni 4.3 na ukizipeleka hizi fedha kwenye fedha za Kitanzania ni matrilioni ya fedha. Kwa hiyo, naishukuru na kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kukishikilia sana kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya hayaji hivi hivi, yanakuja kutokana na utashi wa Rais tuliyenaye madarakani, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amedhamiria kukitoa kilimo kutoka kule kilikokuwa na kukifanya kiwe cha sasa na chenye tija kwa wakulima wake. Tunamshukuru sana, lakini hatuwezi kuwaacha wasaidizi wake, hapa kipekee nampongeza sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, amesimama kidete kusimamia mipango yote inayopangwa katika Wizara yake kuhakikisha kwamba inatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona sasa hivi hata kelele za wakulima wale ambao wanauza mazao yao zimepungua sana. Zipo, lakini zimepungua sana. Pia tunaweza kuona mazao yanayolimwa yanapata masoko. Binafsi, kwenye jimbo langu sisi ni wakulima wazuri wa mahindi. Mahindi katika miaka hii mitatu yameendelea kuuzwa vizuri, na kwa bei nzuri. Mwaka huu tumeahidiwa hapa na Serikali kwamba wakulima watulie, wasiuze mazao yao kwa bei ya kutupa kwa sababu, Serikali ina mipango mizuri, inaenda kununua mahindi haya kwa bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kupitia Bunge hili niwatangazie wakulima wangu wa Jimbo la Mbinga Vijijini wasiwe na haraka ya kuuza mahindi yao, kwa sababu nimeambiwa sasa hivi mahindi yanauzwa kwa kilo shilingi 300, kilo shilingi 350, hiyo bei bado iko chini, lakini Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, ameongea hapa na ninajua kwenye kuhitimisha atatamka hapa kuhusiana na mahindi yatauzwa kwa bei gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natumia nafasi hii kuwashukuru sana na kuipongeza Serikali hii ya Awamu ya Sita. Nisiishie hapo kwenye upande wa kahawa, pia sisi wakulima wa kahawa kipindi hiki tumeuza kahawa kwa bei nzuri. Hatujafikia kule kuzuri zaidi, lakini ni bei nzuri kulingana na miaka ya nyuma. Tumeuza kahawa kuanzia shilingi 3,500 mpaka shilingi 8,000 kwa kilo. Ni bei kubwa sana. Upo mwaka ambao tuliuza kahawa kwa shilingi 8,000; upo mwaka tumeuza kahawa kwa shilingi 6,000, lakini mwaka uliopita bei ilifika shilingi 4,000 ni bei nzuri kwa mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kwa mipango iliyopo na taratibu zilizowekwa tunaweza kwenda kuuza kahawa kwa bei nzuri zaidi. Ombi langu hapa kwa Serikali, nimeona Serikali imefanya vizuri upande wa korosho, wenzetu wale sasa hivi mambo yao yanakwenda vizuri sana. Pia Serikali imefanya vizuri kwa kahawa upande wa robusta. Wenzetu wale sasa hivi hawana malalamiko, lakini sisi wakulima wa Mbinga Vijijini bado tuna shida kidogo. Kahawa tunauza, lakini bado baadhi ya wakulima malipo yale hawayapati, na kama wanayapata, basi ni kwa kuchelewa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali vile ilivyofanya kwenye upande wa wakulima wa robusta mkoani Kagera, wakulima wale wakiuza kahawa hawachukui muda mrefu kupata malipo yao na wanapata malipo yao kwa mkupuo. Naomba vivyo hivyo utaratibu uliotumika kule Kagera basi uje utumike pia, kwa sisi wakulima wa arabica Wilayani Mbinga, kwa sababu, tunalima, tunauza, lakini tunapata dosari kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ziko baadhi ya AMCOS ambazo haziwalipi wakulima. Hivi ninavyoongea wako baadhi ya wakulima ambao bado wanadai malipo ya msimu uliopita na tayari msimu huu uko jirani sana kwenda kuanza. Kwa hiyo, naomba kupitia utaratibu huu ambao Mheshimiwa Waziri ameufanya, ameusimamia kwa Mkoa wa Kagera, basi vivyo hivyo ausimamie upande huu wa Mkoa wa Ruvuma, hususan Wilaya yetu ya Mbinga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, msisitizo kwenye suala hili la viwanda, niliongea muda ule wa Bajeti ya Kilimo, niliongea pia muda wa Bajeti ya Viwanda kuomba viwanda kwenye Wilaya ya Mbinga. Sisi ni wazalishaji wazuri wa mahindi haya. Tuweke viwanda pale, hivi viwanda ambavyo kwenye mpango wetu wa awamu hii umeonesha. Mheshimiwa Prof. Kitila amesema hapa anaenda kuanzisha viwanda vidogo vidogo vikiwemo viwanda vya unga, ili mahindi yetu sasa sisi wakulima wa Mbinga, tusiyauze kama mahindi yenyewe, tuuze unga. Najua unga una thamani na unga utatupa fedha zaidi kuliko kuuza mahindi ghafi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana jambo hili Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa sababu, tayari imejionesha kuwasaidia wakulima basi, i-set viwanda kwenye maeneo haya ya uzalishaji, hasa Wilaya ya Mbinga, tunazalisha mahindi mengi. Watuwekee viwanda pale vya unga, watuwekee viwanda pale vya kahawa ili mwisho wa siku sasa malighafi yetu tuisage, tuuze sasa mali iliyo sahihi zaidi kuliko mazao yenyewe. Naomba sana suala hili lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niongelee suala la utekelezaji wa miradi. Naipongeza sana Serikali hii ya Awamu ya Sita kwa utayari wa kupeleka miradi kwenye maeneo yetu. Ni miradi mingi sana; niitaje michache kwenye Wilaya yangu au kwenye Jimbo langu. Mimi nina Mradi wa Ujenzi wa Barabara kutoka Kitai – Amanimakoro – Ruanda mpaka Lituhi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara kutoka Amanimakoro kuelekea Ruanda tayari mkandarasi yuko site, lakini kasi ya utekelezaji mradi huu iko nyuma sana. Mradi huu tulikuwa tukabidhiwe tarehe 18/12/2024, lakini mpaka ninavyoongea hapa bado mkandarasi hajaanza kuweka hata doti ya lami. Wananchi wangu wamenituma hili nilisisitize hapa. Barabara hii ndiyo inayopitisha makaa ya mawe, ndipo mahali ambapo uzalishaji mkubwa wa makaa ya mawe unatokea. Kwa hiyo, ni barabara ya kiuchumi na ni barabara inayoiingizia fedha nyingi nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hii Serikali ya Awamu ya Sita ambayo iko tayari kuijenga hii barabara iharakishe kupeleka fedha kwa mkandarasi yule ili barabara ijengwe na ikamilike. Nashukuru kipande cha pili kuanzia Ruanda kwenda Lituhi hadi Ndumbi ambako tumejenga bandari nzuri ya kisasa, tayari tumeingia mkataba na mkandarasi. Sasa naomba nako tupeleke fedha kwa haraka kwa mapema ili sasa kinapokamilika kipande hiki cha killomita 35 basi na kile kipande cha pili cha kilomita 50 hadi 60 kikamilike ili barabara yote iweze kutumika kwa manufaa ya kukuza uchumi upande ule wa kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo tuna barabara inayotoka Songea hadi Makambako. Barabara hii ni muunganiko wa barabara inayotoka Ndumbi - Mbamba Bay kufika Songea, lakini ije sasa Makambako mpaka Dar es Salaam kupeleka malighafi hizi. Barabara hii na wewe utakumbuka kwa sababu inakugusa katika kipande pale, imetamkwa muda mrefu, mpaka leo hii hatuoni ujenzi wa barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali yetu hii sikivu kwa sababu shida hapa ni fedha hazijaenda, itoe fedha barabara hii ianze kujengwa. Hali ya barabara hii sasa hivi ni mbaya sana, muda wowote tutahatarisha hali za watumiaji wa barabara hii. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali hii sikivu, naomba Mheshimiwa Waziri Nchemba, yuko vizuri, atuletee fedha kwenye hii miradi ili ikamilike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni mradi wa Umwagiliaji, Litumbandosyi ambao tumekuwanao na uko miongoni mwa miradi ile 19. Eneo hili tunazalisha sana mpunga, lakini tukipata huu mradi, ukikamilika, maana yake ni uwezo wetu wa kuzalisha utaongezeka na wananchi wetu watapata kipato kikubwa kwa sababu, watakuwa na uwezo sasa wa kuzalisha siyo kwa mwaka mara moja, bali wanaweza kuzalisha hata mara mbili kadiri mlivyotupangia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tulikuwa tuanze kutumia ule mradi, lakini bado na wenyewe unakwenda kwa kasi ya chini sana. Naomba sana mradi huu upelekewe fedha na wenyewe tuanze kuutumia.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha kipaza sauti. Nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)