Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Emmanuel Lekishon Shangai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Mipango na Uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nawapongeza Mawaziri wote wawili kwa kazi nzuri pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili hasa ndugu zangu hawa wawili, mimi sitawaita Singida Boys ila nitawaita watani wangu kwa sababu they are no longer boys. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa nimepitia Hotuba ya Waziri wa Mipango na Uwekezaji na Waziri wa Fedha. Waziri wa Fedha ameenda kwa jinsi ambavyo Waziri wa Mipango na Uwekezaji amefikiria. Kwa hiyo, naye amepanga kwa mikakati ya ushuru pamoja na kodi kwa sababu Waziri wa Mipango yeye anapanga nini kinachotakiwa, lakini Wazri wa Fedha anaenda kutuambia kwamba ni kwa namna gani tunapata fedha kwa ajili ya ku-finance Mipango ya Serikali kwa Mwaka 2024/2025. Kwa hiyo, nawapongaza sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiuhalisia mmetuonesha njia, lakini najaribu kuangalia kwamba katika dunia ya sasa hivi au Tanzania, hatujawahi kuwa na tatizo la mipango, kama alivyosema Mheshimiwa Profesa Alexander Mkumbo. Tatizo letu ni katika utelelezaji wa mipango yetu kwa sababu kupanga na kutekeleza ni vitu viwili tofauti sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia Hotuba ya Waziri wa Mipango, amesema kwamba ni lazima tulinde viwanda vyetu vya ndani, lakini kwenye ushuru nimejaribu kupitia kwenye Hotuba ya Waziri wa Fedha ameondoa baadhi ya tozo na ushuru kwa baadhi ya bidhaa ambazo zinazalishwa nchini ambazo zinalinda viwanda vyetu. Kwa mfano, viwanda vya bati, nimeona pia nondo na vifaa vingine vya chuma, Waziri wa Fedha ameondoa ushuru pamoja na ushuru wa forodha na maeneo mengine kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu. Nawapongeza sana kwa hilo kwa sababu mmejitahidi. Hatuwezi kukusanya kodi kama hatuna watu ndani ya nchi yetu ambao wana uwezo wa kuzalisha pamoja na kupata fedha ambazo Serikali inaenda kupata kodi kutoka kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima tuendelee kuwasaidia Watanzania wanaowekeza mitaji yao ndani ya nchi yetu ili Watanzania wanunue bidhaa zao pamoja na wao kupata fedha ambayo Serikali itapata kodi kutoka kwao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia kauli moja ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kuna kauli moja hapa ambayo alisema wakati anasoma hotuba yake, inahusiana na wafugaji. Kauli hiyo inasema kwamba, “Mtu mwenye ng’ombe 9,000 kutokulipa kodi na kutaka kujengewa josho au bwawa kwa ajili ya mifugo yake kwa kodi ya mtu mwenye kipato cha shilingi 300,000 kwa mwezi, siyo sawa.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kwa Tanzania au wafugaji wa Tanzania ninaowajua mimi nafikiri kama kuna mtu mwenye ng’ombe 9,000, labda kwa mfano nichukulie kwenye Jimbo la Ngorongoro ninapotokea, sijui mtu yeyote mwenye ng’ombe hata zaidi ya 1,000. Leo hii, kauli hii is too general, na akasema kwamba; “Napendekeza kila halmashauri zenye idadi kubwa ya mifugo kuratibu ushirika wa mifugo na kuanzisha mfuko wa kuendeleza huduma za ugani za mifugo na miundombinu ya mifugo kama majosho kwa kutumia mifuko hiyo na magari ya Serikali ya kuchimba mabwawa na visima yaliyopo mikoani mwetu. Vyama vya wafugaji wakubaliane kuhusu utaratibu wa uendeshaji wa mifuko hiyo, kama inavyofanyika kwa vyama vya ushirika kwenye mazao kwa mfano, korosho, tumbaku, pamba na kadhalika.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui ni wapi ruzuku inatolewa kwa wafugaji, lakini naamini kwa wakulima mnawapa ruzuku ya mbolea. Kwa mfano, leo sisi wafugaji tunapata wapi au sisi kuwa na mifugo imekuwa ni tatizo? Kwa sababu kwa nchi hii mfugaji naye ni mtu anayejitegemea, hutegemea mifugo yake kuanzia mwaka mmoja anapozaliwa mpaka anapofikisha miaka sita ndiyo ana uwezo wa kuuza ili apate mapato kutokana na ile mifugo. Unajua ni gharama kiasi gani kwa mfugaji kutunza mfugo mmoja kutoka mwaka wa kwanza mpaka mwaka wa sita? Anatumia siyo chini ya shilingi 300,000 halafu baadaye anauza shilingi 600,000 kwa ng’ombe mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri wa Fedha tusitumie hii generalisation kwa ajili ya kwenda kuwahukumu wafugaji wote wa Tanzania. Ni lazima tuangalie, tufanye study kwamba ni wafugaji wangapi ambao wana mifugo mingi? Hakuna mtu ambaye anakataa kwa sababu wafugaji nao wanalipa ushuru na kodi. Anapoenda dukani kununua dawa, analipa kodi. Hata anapoenda mnadani kuuza mfugo wake analipa ushuru. Kwa hiyo, tuangalie namna ambayo tutawatengenezea wafugaji wa Tanzania njia ambayo itatuletea manufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia imependekeza kwenye malipo ya export permit kwamba iwe kutoka shilingi 30,000 which kwa kawaida siyo shilingi 30,000, ni shilingi 25,000, ikaenda kwenye shilingi 31,000. Nadhani, kama tunataka ku-discourage watu kuuza nje mifugo, tutengeneze mazingira ya ndani ambayo tutahakikisha kwamba Serikali inakuja na bei elekezi ya mifugo na wauze kwa kilo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwenye mapendekezo yote ya ushuru pamoja na kufuta au kutoa unafuu, sijaona eneo lolote ambalo linatoa unafuu kwa vifaa vya viwanda vya uchakatji wa mazao ya mifugo ambayo ingesaidia pia wafugaji kuweza kuuza mifugo yao au kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naishauri Serikali ije na mpango ambao tutaanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo Tanzania ikiwepo nyama, maziwa pamoja na mazao mengine. Pia tuwe tunauza mifugo yetu kwa bei, badala ya kwenda sokoni na kukadiria bei ya mifugo, hiyo haitawanufaisha wafugaji wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa Mheshimiwa Waziri wa Mipango, kwa sasa kama Tanzania tunataka kwenda kwenye uchumi wa kidijiti, mawasiliano ni kitu cha muhimu, lakini kwa Tanzania maeneo mengi hayana mawasiliano ukitoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Hakuna mkoa utasafiri Tanzania kukawa na mawasiliano, labda kilometa 100 mpaka 200. Ni lazima tuone ni namna gani ambapo kwa Tanzania hii tunawajengea watu uwezo kuwepo na mawasiliano na internet kwa kila mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunataka kuhamasisha wananchi wawe wanatumia lipa namba; kuna maeneo mengi Tanzania hapa hawana mawasiliano. Sasa ni lazima tufikirie ni namna gani ambayo Watanzania wanaweza kuwa na mawasiliano. Kwa mfano, kwenye Wilaya yangu ya Ngorongoro kwenye kata 28 kata ambazo zina mawasiliano ni kata 10 tu na siyo kote, ni partially; kijiji kimoja kinayo, kijiji kingine hakina. Kwa mfano, Kata ya Sale, Loswashi, Tinaga, Njoroi, Naan, Oloipiri, Karkamoru, Piyaya, Naiyobi, Ngoile, Kakesio, Meshil, Naiyobi, na maeneo mengine hakuna mawasiliano. Sasa hawa wananchi tutawezaje kuwashawishi waweze kwenda kwenye digital economy? Kama hawawezi kuwasiliana, hawawezi kufanya transaction. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mengine kwenye Jimbo langu la Ngorongoro, tunataka barabara ya lami kutoka Sale mpaka Kigongoni. Kwenye wilaya yetu bado kuna tatizo kubwa la usafirishaji. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini anajua, walikuja na Naibu Waziri Mkuu aliacha bumper la gari yake Ngaresero. Nampongeza Naibu Waziri Mkuu kwa sababu alikuja kwa gari mpaka Loliondo, ameona changamoto iliyopo, lakini baadaye ilibidi waruke na ndege kwa sababu hawawezi kufika Arusha tena kwa magari yao. Sasa hawa wananchi wa Ngorongoro tuwasaidie nao wapate barabara ya lami waweze kufanya shughuli zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana. (Makofi)