Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia. Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyenijaalia uzima kusimama tena kwenye Bunge lako Tukufu. Pia nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa ushirikiano ambao wanaendelea kunipatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitaanza na Deni la Taifa. Kukopa siyo dhambi na nchi zote zinakopa hasa nchi zinazoendelea. Najua haki hiyo tunaipata kwenye Katiba yetu Ibara ya 141(i) – (ii) ambacho kinasema Deni la Taifa litadhaminiwa na Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa madhumuni ya ufafanuzi wa Ibara hii, Deni la Taifa maana yake ni deni lenyewe na pia faida inayolipwa juu ya deni hilo, fedha zinazowekwa akiba kwa ajili ya kulipa deni polepole na gharama zote zinazoambatana na usimamizi wa deni hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie tu kwenye usimamizi. Kwa kuwa tuna haki ya kukopa, lakini kama Bunge tuna wajibu wa kushauri juu ya mikopo tunayokopa. Kama ambavyo nimeanza kuzungumza, kukopa siyo dhambi wala siyo kosa, lakini tunakopa fedha hizo kupeleka kwenye miradi gani? Kama Taifa tunanufaikaje na mikopo hiyo? Watanzania wananufaikaje na mikopo tunayokopa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuona kwamba kuna umuhimu sasa pamoja na kwamba bado tunakopesheka, lakini tuangalie, lazima kama Taifa tuwe na mtazamo kwamba tunakopeleka fedha hizo kuna wakati kama Taifa tutahitaji kule ambako tumepeleka sasa fedha hizo tuweze kujiendesha kama Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukikopa tukapeleka kwenye miradi ya uzalishaji siyo kosa, tunaenda kuzalisha ajira kule lakini miradi yenyewe ile itachangia baada ya kuzalisha kuendelea kujiendesha kama Taifa. Mimi siyo muumini sana, pamoja na kwamba tuna changamoto ya vyoo mashuleni, tunayo changamoto ya madarasa, siyo muumini wa kusema fedha tunazokopa kwa gharama kubwa tupeleke kujenga vyoo shuleni, isipokuwa tukikopa fedha tukapeleka kwenye miradi ya uzalishaji, miradi hiyo ambako tumepeleka, kama ni kwenye kilimo tunajua tukizalisha tutaenda kujenga vyoo, tutajenga madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna madarasa ambayo tulijenga kipindi cha COVID, yaani shule hazijamalizika yale madarasa wanayojenga yameshaweka ufa, lakini hayo madarasa lini yata-mature ili tulipe deni? Kazi ya Bunge ni kuishauri Serikali na niko hapa kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia leo tumewekeza kwenye kilimo, ni jambo jema, nami naunga mkono kwa sababu tunaamini kwenye kilimo kuna uzalishaji. Leo tumeweka ruzuku kwenye mbolea, ni jambo jema kwa sababu tunataka Watanzania wengi wapate mbolea wazalishe na Taifa liendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri kidogo tu. Pamoja na ukuaji ambao kwa sasa sekta ya kilimo inachangia kwenye pato la Taifa, leo tuna Watanzania wengi ambao wanatamani kulima zaidi ya ekari 100 na kuendelea, lakini nini tunaweza tukafanya? Ni wajibu wa Serikali kuweka vizuri kwenye mipango sasa. Hapa tumeona Kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Mheshimiwa Prof. Kitila, watu wangu wa Nkasi kule hawana shida na hizo taaluma zenu, wanataka wazione taaluma kwa kuenda angalau kubadilisha maisha yao ya sasa. Naamini Mheshimiwa Rais kuwateua hakufanya bahati mbaya, tunataka tuone ushauri utakaoendana na taaluma zao kwenda kusaidia maisha ya Watanzania kutoka kwenye ugumu wa maisha waliyonayo sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kama mtu ana-trend ya miaka mitatu, ananunua mifuko 200 ya mbolea ambayo ina ruzuku, ni kwa nini mkulima huyo, kwa sababu mmeshaona trend yake, usitengenezwe utaratibu akapewa mbegu, akapewa na mbolea akaja kulipa baada ya mavuno? Kwa sababu tutakuwa tumemwongezea uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu natambua wapo wakulima ambao anatamani hata shilingi 70,000 hana, kwa sababu nchi yetu hatuna shida ya maeneo ya kulima, lakini watanzania hao wanahitaji kuwezeshwa ili nao watoke kwenye zile sekta wanazoziita siyo rasmi. Kwa sababu, tunajua ni wajibu wa kila Mtanzania kulipa kodi, lakini tuchukue kodi ambazo ni halali. Kodi ambazo tumewatengenezea mazingira rafiki ya uzalishaji ili waweze kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siyo muumini wa zile kodi ambazo tunafikiri tunataka kujaza idadi, mimi ni muumini wa wananchi waliowezeshwa mazingira rafiki watimize wajibu wao wa kikatiba kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimezungumzia kwenye kilimo tu, nitolee mfano tu wa Mkoa wa Rukwa. Tuna maeneo mazuri sana yanayofaa kwa kilimo. Sisi hata kwenye mabwawa, fedha ambazo zinatumika, sisi tuna Ziwa Tanganyika, tunahitaji fedha tukawawezeshe vijana wetu ambao hawana ajira waende kwenye kilimo cha umwagiliaji, tuachane na kilimo cha kutegemea mvua kwa mwaka mara moja. Hao Watanznaia wapo. Nini ambacho hakijafanyika? Ni wajibu wetu sasa na yeye Mtanzania wa Nkasi aone mkopo uliokopwa safari hii, nami mwana-Nkasi nimenufaika na huo mkopo. Kitu ambacho nakiona kwenye nchi yetu, kwanza ni mipango. Hiyo mipango tunayopanga ni namna gani inaenda kuwanufaisha wananchi moja kwa moja kule chini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitolee mfano tu. Nilizungumza jambo moja kwenye hoja ya dharura hapa ukaniambia nitazungumza leo, ninaenda kulisema sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya uvuvi hatujawekeza sawasawa. Hapa ninapozungumza, eti mipango yetu tumejikita kupumzisha ziwa kwa miezi mitatu. Kwa sababu gani? Samaki wamepungua. Kwa hiyo, ukifunga miezi mitatu, samaki wanajaa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miezi mitatu, ukifungua, uvuvi haramu utaendelea na wale wavuvi haramu ndiyo watanufaika na huo uvuvi, badala ya sisi kufikiri kuongeza pato kupitia uvuvi, tuwawezeshe hawa wananchi wetu. Tumeamua kuweka vizimba, sawa; vyakula ni bei ghali. Kwa nini msiwakopeshe hivyo vyakula? Vyakula vyenyewe vinatoka nje ya nchi! Ili tuone fedha tuliyowekeza kwenye uvuvi, tumeweza kuongeza pato la Taifa kwa kiasi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufunga miezi mitatu ni mawazo mgando. Mimi sikubaliani hata siku moja, kwa sababu tutafungua, samaki wataonekana wamejaa. Wamejaa mwezi huu, anayenufaika ni yule ambaye anatumia uvuvi haramu. Atavua zaidi kuliko yule ambaye amelipa leseni, kalipa kodi zote za nchi hii, atapata mavuno ndani ya wiki moja, tunarudi kule kule samaki wamefanya nini? Wameisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na hayo mawazo, lazima tuwe na mpango endelevu wa namna gani tutatunza maziwa yetu makuu? Namna gani tutawainua wavuvi wetu? Aliyekuwa anapata angalau pato la shilingi milioni mbili kwa mwaka, tutegemee kwamba baada ya pale anaweza kupata shilingi milioni nne. Huyo tutamwambia unatakiwa utoke pale ulipokuwa unalipa kodi, uongeze kiwango cha kulipa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyozungumza hapa, hiyo miezi mitatu, Watanzania wenye haki ya kufanya shughuli halali ya uvuvi wa Ziwa Tanganyika wamefungiwa kwa sababu ya maamuzi ya mamlaka. Wamelipa leseni, hakuna siku tumetenga fedha ya kuwapa kwa kipindi cha mpito hawa Watanzania, ni kwa sababu hawana sehemu ya kusema. Kwa nini tunafanya mambo hayo? Bado tunasema alipe kodi; amelipa kodi. Ile kodi siyo halali, mmemnyonya huyu Mtanzania, tumempa umaskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu mtu ameenda kukopa fedha benki, lakini tulichokifanya ni kutumia nguvu yetu ambayo tunayo ya mamlaka kuhakikisha huyu Mtanzania anakosa haki yake halali. Narudia kusema tena, chanzo kikubwa cha nchi yetu pamoja na kukopa kwa nia njema, shida kubwa ya nchi yetu ni usimamizi wa fedha, nidhamu mbovu ya fedha kwenye Taifa letu, kuna upotevu mkubwa sana wa fedha. Kila ripoti ya CAG kuna upotevu wa fedha. Tujikite hapo tuweze kuzuia mianya ya upotevu wa fedha ili tuweze kuiona fedha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekii, jambo lingine, pamoja na upotuvu wa fedha, hata vyanzo tulivyonavyo tunakusanya sahihi? Bado kuna shida kwenye nchi yetu. Ukusanyaji tu ni changamoto, lakini hata kile kinachokusanywa kinakwenda sehemu ambayo inatakiwa kwenda hiyo fedha? Bado kuna shida kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kushauri kwa nia njema, changamoto kubwa ya nchi yetu pamoja na kukopa fedha ni usimamizi mbovu wa fedha hiyo na mianya mingi ya upotevu wa fedha. Kama nia ni njema, lazima tuangalie, hatuwezi kukopa miaka yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kushauri kwa nia njema, nchi ni yetu, tukope fedha tupeleke kwenye maeneo ya uzalishaji ili tuweze kulipa hayo madeni na baadaye kama Taifa tuweze kujiendesha. Tusikope kama fashion, tukope tukiamini siku moja kama Taifa hili tunaweza kujiendesha wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. (Makofi)