Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Kasalali Emmanuel Mageni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hii nafasi ya kuchangia kwenye bajeti ya Serikali yetu. Awali ya yote niwapongeze Mawaziri husika, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha; Mheshimiwa Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Mipango; na Naibu Mawaziri wao, Mheshimiwa Chande na Mheshimiwa Nyongo kwa namna ambavyo mmewasilisha bajeti hii nzuri ambayo imegusa maeneo mengi katika maendeleo ya nchi yetu. Ninawapongeza kwa kazi hii na Wabunge kazi yetu sasa ni kushauri ambapo hamjaweka mambo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuwashauri, naomba nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza sana Rais wa nchi yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri, njema na ya kizalendo anayoifanya kwenye nchi yetu. Nadhani sisi sote ni mashahidi, Rais wetu amekuwa muungwana, amekuwa mvumilivu, amekuwa mstahimilivu, amekuwa kiongozi mwema kabisa kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Watanzania wanayaona yote anayoyafanya na mwaka 2025 watafanya kinachopaswa kwa kummwagia kura, nami kwa niaba ya watu wa Sumve niseme kwa yote aliyoyafanya Mama, Rais wetu tutampa kura nyingi sana. Kama zitatokea chache za kutokupata, basi itakuwa bahati mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ameonesha uvumilivu mkubwa sana, usikivu kwa kuruhusu mambo mengi ambayo yalikuwa yamezuiliwa hapo kabla. Naweza nikatoa mfano, Vyama vya Upinzani vililalamika kuhusu mikutano ya hadhara, kuhusu mambo ya demokrasia na kadhalika; amewaruhusu wameanza mikutano ya hadhara, wanasema wanavyosema, lakini kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya, sasa bahati mbaya sana zile sera za kusema, zimeisha kwa sababu kazi nzuri inafanywa, wameruhusiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri wamehamia kwenye matusi, kwenye kugawa nchi, kwenye udini na ukabila na hizo ni sifa za watu ambao wanakuwa wameishiwa sera. Kwa hiyo, hiyo ni moja ya mafanikio makubwa ya Mheshimiwa Rais, kufanya kazi nzuri mpaka wanaompinga wanaishiwa sera, hivyo, tunampongeza kwa kazi hiyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais pia amekuwa msikivu, hapa Wabunge tulisema tukashauri kuhusu kikokotoo, nadhani mmeona kupitia bajeti hii, kuna mwelekeo wa usikivu na mabadiliko kwenye kikokotoo. Kutoka ile 33% kwenda 40% ni hatua kubwa, lakini sisi kama Wabunge, mimi ninajua bado ninalo jukumu la kushauri Serikali yetu ya CCM iendelee kulitazama jambo hili kwa sababu chama chetu ni cha wakulima na wafanyakazi. Tufanye zaidi, ikiwezekana tufike ile 50% iliyokuwepo na ikiwezekana wale ambao tayari walishashughulikiwa na kikokotoo, hii nafuu iliyopatikana iwapate wakati huo tukijadili namna ya kufanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba sasa nijielekeze kwenye kuzungumza mambo yaliyoko kwenye Jimbo la Sumve. Watu wa Sumve tunayo shukrani kubwa ya kimaendeleo kwa Rais wetu. Tulikuwa tuna mambo machache nitayatolea mfano ambayo tulikuwa tunayalilia na ameyatekeleza. Wakati yeye anaingia madarakani na mimi nakuwa Mbunge, Sumve ilikuwa na vituo vya afya viwili tu, lakini leo tunazungumza viko vitano. Kazi nzuri ya Mheshimiwa Rais na sisi watu wa Sumve tunashukuru kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tulikuwa hatujawahi kuona mradi wowote wa kuleta maji ya Ziwa Victoria na hayakuwepo. Tuko kwenye Mkoa wa Mwanza, lakini ladha ya yale maji hatuijui, lakini kwenye uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia, ametupatia mradi wa shilingi bilioni 39, unatoa maji Misungwi, Koromije, Sumve mpaka kwenye Jimbo zima la Sumve kupata maji ya Victoria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ametoa mradi mwingine wa maji ya Ziwa Victoria, unatoka Hungumalwa kupitia Jimbo la Mheshimiwa Mashimba Ndaki mpaka Malya kwenye Jimbo la Sumve. Hii ni heshima kubwa kwa watu wa Sumve na mambo mengi kwenye sekta za elimu na barabara za vijijini yamefanyika. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekoiti, sasa, Serikali ya CCM ni Sikivu na mimi ni Mbunge wa CCM na ni Mbunge wa Jimbo la Sumve, sasa nami naomba yale ambayo hayajatekelezwa, nishauri namna ya kuyatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa hapa nadhani kama huwa tunasikilizana vizuri, nimekuwa nikizungumza shida kubwa sana iliyoko kwenye Jimbo la Sumve. Siasa ya Sumve ni barabara, na nimekuwa nikizungumza kweli kuhusu siasa ya Sumve ya barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikiwaambia kwamba, historically, labda leo unipe nafasi nitoe elimu kidogo. Jimbo la Sumve na Wilaya ya Kwimba ni moja ya maeneo ya kiutawala, makongwe na mama kwenye nchi hii. Wakati wa ukoloni tulikuwa na Mkoa wa Nyanza Province, ulikuwa na Wilaya za Mwanza, Musoma, Bukoba, Shinyanga na Wilaya ya Kwimba. Tulipopata Mkoa wa Mwanza, Wilaya za mwanzo ni Geita, Mwanza, Ukerewe, Kwimba yenyewe pamoja na Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kwimba ni Wilaya kongwe, imezaa Wilaya ya Magu, imezaa Wilaya ya Misungwi na ina mjukuu anaitwa Busega. Ni Wilaya kongwe kweli kweli, lakini ninavyozungumza hivi, mimi Mbunge ninayetoka Kwimba Jimbo la Sumve. Wilaya ya Kwimba ni Wilaya pekee kwenye Mkoa wa Mwanza ambayo haijaungwa na Makao Makuu ya Mkoa na barabara ya lami. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sizungumzii leo, nimekuwa nikizungumza kila mara na kusisitiza, wakati mwingine ninakasirika na wakati mwingine nakuwa mpole nikiwaeleza ninyi ndugu zangu wa Serikalini kwamba, kule Sumve tunaomba mtujengee barabara ambayo hatujajiahidi sisi, tuliahidiwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, nami niliiuza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inatoka Magu – Bukwimba – Ngudu – Hungumalwa, kwa kiwango cha lami na ni barabara ya kilometa 71 tu, siyo barabara ndefu sana. Kwa sababu yapo maeneo mengi yanajengewa hizi Barabara, tunaona na wengine mpaka zinabanduliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona mwaka huu janga la mafuriko limezoa lami za watu, wakati wengine wanazolewa lami na bajeti inahamishiwa kwenye kuzirudishia zile lami, sisi hatuna. Jimbo la Sumve hata milimita. Yaani, hivi unaelewa nikisema milimita! Sentimeta ni kubwa kwa milimita, hatuna hata milimita moja ya lami Sumve na sisi ni Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nimelisema hapa kwa Mawaziri wote wakiwepo. Nilianza na Mzee Chamuriho akaniahidi ahadi haikutekelezwa. Kwa hiyo, kwa Kiswahili kizuri akanidanganya. Nikaja hapa Mheshimiwa Prof. Mbarawa nikamwomba akaniahidi ahadi haikutekelezwa, kwa hiyo lugha ya kistaarabu ni kwamba alinidanganya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nina imani na Mheshimiwa Bashungwa, hujapata nafasi ya kunidanganya. Naomba usinidanganye. Naomba utujengee barabara na kule watu wetu kama walivyo watu wengine, nilikuwa naona kule Mtwara, umefanya kazi nzuri sana wakati wa haya mafuriko ya kuwafikia watu na kuwatia moyo na kurekebisha miundombinu, lakini hao uliokuwa unaona lami zao zimesombwa, sisi hatuna kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii nchi haiwezekani wengine wanarudishiwa barabara zilizosombwa, wengine hawana. Hao waliosombewa lami zao wasubirie sisi ambao hatuna hata lami ya kusombwa na mafuriko tuwekewe ili walau na sisi ije isombwe tuone, kwamba lami huwa zikisombwa this is what happens. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiendelea hivi, sio sawa. Sasa hivi nimeona bajeti unarudishia kwa wale waliosombewa lami zao, sisi bado hatuna, tufanyeje? Turushe ngumi humu! Kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, umewahi kuniahidi hapa mpaka ukaniambia unachukua mkopo kunijengea, hamna kitu, hujajenga brother. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, naomba, naomba; mimi sasa hivi imani nitakayoamini hapa ni kuona magreda yako Sumve yanajenga lami, kwa sababu ahadi nimeshapewa, na Mheshimiwa Katimba leo wewe ndiyo Waziri Mkuu wetu. Nikwambie, si ndiyo anakaimu! Mimi ninakushtakia, watu wa Sumve tumedanganywa sana kuhusu Barabara, na Mbunge wao sasa niseme nini humu? Kama utaona uvivu kwenda kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri Senior akina Mheshimiwa Jenista hapo, kuna Mheshimiwa Simbachawene hapo nyuma, wanisaidie. Sisi tumedanganywa sana. Tunaomba sasa na sisi tujengewe barabara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani inafika wakati tunaona sasa sisi hapa...

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Hamis, Taarifa.

TAARIFA

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Siku hiyo wakati anaahidiwa lami na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, mimi nilikuwepo. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuahidiwa lami, vikao vyote vilivyokuwa vinafanyika vya Marais wakati ule anagombea Mheshimiwa Mkapa, aliahidi lami ya kutokea Magu kwenda Hungumalwa, mimi nilikuwa Ngudu kwenye mkutano wa hadhara. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, akaja akaahidi Mheshimiwa Kikwete, nilikuwa tena Hungumalwa kwenye mkutano wa hadhara. Kaja kaahidi mama yetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikuja Kwimba niko kwenye mkutano wa hadhara. Sasa kama ahadi za viongozi wa Serikali hazitekelezwi, wasiwasi wangu ndiyo unakuwa mkubwa kwa sababu ni ahadi ya viongozi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Kasalali, unapokea Taarifa ya Mheshimiwa Hamis Tabasam?

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa heshima kubwa sana taarifa ya Mheshimiwa Tabasam. Pia ninasisitiza, ndiyo maana nimetaja cheo cha Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa sababu mimi wakati naomba kura pale Sumve aliyekuja kunishika mkono ni Mheshimiwa Waziri Mkuu, naye akasisitiza kwenye ahadi iliyokuwa imetolewa na Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais wakati ule alipokuja Sumve kuhusu kujenga barabara ile, akasisitiza itatekelezwa. Sasa tupo bado kwenye hatua za mwishoni mwishoni, hebu jamani tufanyeni hili tulimalize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo barabara ya msingi sana kwenye uchumi na utalii wa Kanda ya Ziwa, barabara ambayo inatoka Bujingwa au Fulo inapita Nyambiti inaenda Malya na baadaye inaenda Maswa kwa Mheshimiwa Nyongo. Bahati nzuri Mheshimiwa Nyongo sasa yupo kwenye Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii ni muhimu sana kwenye kufungua Mbuga za Maswa na utalii wa Serengeti ya Kusini. Barabara hii imeahidiwa kwenye ukurasa wa 78 wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na sote tunajua tupo hapa kumsaidia Mheshimiwa Rais. Naomba sana, sana, sana viongozi wangu Sumve ni barabara na siasa za Sumve ni barabara. Sasa na ninyi mpo hapo kutekeleza hilo. Wakati wa kitubio mtubu, kama mliwahi kutudanganya mwende mkatujengee barabara yote siyo kipande, yote na sisi tuanze kukanyaga lami maisha yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naahidi kama nitathibitishiwa kwamba sidanganywi tena, nitaunga mkono bajeti hii. (Makofi)