Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami pia nawashukuru Mawaziri wote wawili na wasaidizi wao na pia namshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya uchangiaji kwenye bajeti hii, naomba nianze na yale ya jimboni. Namshukuru Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, tulikuwa na shida kubwa ya chumba cha kusaidia mashine za uchujaji damu. Tumepewa takribani shilingi milioni 196, najua ujenzi mzima wa kile chumba unahitaji shilingi milioni 400. Ninaamini tumeanza huko mbele ya safari Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, umelisikia hilo utaona namna ya kutusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa kwa maana ya kuboresha uchumi wa Mkoa wa Katavi ni suala zima la Gridi ya Taifa (umeme wa msongo mkubwa). Sijaiona ikisomeka hapo, lakini naamini mpango mkubwa wa kuhakikisha Mpanda tunafikishiwa umeme wa Gridi ya Taifa utatusaidia katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani kuendelea kushauri, furaha ya kuwa na vitu vingi wakati mwingine inaweza ikakufikishia sehemu ukashindwa kujua uanze na kipi. Kama nchi, Mwenyezi Mungu ameturuzuku tuna vitu vingi sana, kuanzia madini, misitu, bahari, ardhi yenye rutuba, watu ambao pia hata suala la amani na utulivu ni kati ya vitu ambavyo Mwenyezi Mungu ameturuzuku. Hasa kutokana na hayo tunajikuta wakati mwingine tunapata shida, vitu ni vingi, hujui uanze na kipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kauli yangu ni nini? Ni vizuri tukaja na vipaumbele, tuwe na vipaumbele vichache. Tukianza na hivyo tutafika mahali. Sisemi kwamba mengine tuache, lakini tu-concentrate kwenye maeneo machache ambayo hayo yanaweza yakatusaidia kututoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuongea hapa ndani, bahati nzuri ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu yupo hapa, kwamba tukizungumzia habari ya kuiunganisha nchi hii kwa mtandao wa maji (Gridi ya maji ya Taifa), tafsiri yake ni nini? Tunapozungumzia vyanzo vingine vya mapato kwa suala tu la kuunganisha nchi kwa mtandao wa maji, naijua jitihada ya Serikali katika maeneo hayo, kuunganisha kwa kutokea Ziwa Victoria, tunazungumzia habari ya kuunganisha kutokea Ziwa Tanganyika, kuunganisha vyanzo vyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukija na hiyo Gridi ya Taifa maana yake hapo kwa maana ya uchumi kilimo kitakua, kwa maana ya uchumi utalii utaongezeka na ufugaji halikadhalika. Kwa hiyo, hili suala la Gridi ya Taifa kati ya vipaumbele nilikuwa naomba sana tusisahau jambo hili. Pia, tuna maeneo mengine ambayo nashangaa Watanzania wenzangu Kiswahili kama Kiswahili ni bidhaa. Hebu tuipeleke huko duniani, kwani ni chanzo kikubwa cha mapato, na ni fursa ametupa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, ukifika mahali ambapo Kiswahili kinatoka Tanzania hapa, lakini ukienda baadhi ya nchi huko walimu wakuu katika vyuo mbalimbali unakuta ni watu wa nchi nyingine. Kwa nini tusitumie fursa hii? Kwa nini nalisema hilo? Tukikipeleka Kiswahili duniani, fedha watakayopata watu wetu huko wataturudishia nchini. Tukifanye Kiswahili kuwa bidhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo nilikuwa naongelea habari ya hiyo mipango, yaani kwa maana ya kuwa na vipaumbele. Nije kwenye suala la mipango fungamanishi. Kwanza siku zote mimi ni kinara wa masuala ya idadi ya watu kwa maana ya hapa Bungeni ni Mwenyekiti wa Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu. Naomba niendelee kusisitiza kwa maana ya mipango. Sikatai idadi ya watu, lakini ukiwa na idadi ya watu ambao huwezi kuwadhibiti, tatizo langu ndiyo linakuja hapo. Unapokuwa na midomo mingi ya kulisha kuliko wazalishaji, tatizo linakuja hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana mipango yetu iende huko, kwa sababu sasa hivi ukijaribu kuangalia na huko duniani nimeshiriki makongamano mbalimbali, dunia inaogopa kutokana na suala la ongezeko la watu, na bahati mbaya zaidi wakiiangalia Afrika na ukiangalia Afrika utarudi hata Tanzania. Leo turudi kwenye idadi ya Watanzania tuliopo, wazalishaji ni wangapi? Unapokuwa na midomo mingi ya kulisha kuliko midomo mingi ya kuzalisha, tatizo lipo hapo. Kwa hiyo, nasema idadi ya watu siyo tatizo, ikitumika vizuri ni fursa, lakini isipotumika vizuri tatizo naliona linaanzia hapo. Kwa misingi hiyo, naomba suala la idadi ya watu tuliangalie vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru suala la kuboresha nidhamu ya matumizi ya fedha, lakini pia kuboresha kitengo cha ufuatiliaji na tathmini na nilikuwa naomba watu hao wapatiwe rasilimali fedha na idadi ya watumishi iongezwe eneo hilo. Tunapozungumzia sekta za uzalishaji na huduma za jamii, usalama wa chakula, amani, usalama na umoja ni jambo la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia suala lingine ambalo niliwahi kuongelea hapa suala la mapinduzi ya nne ya viwanda. Kwa maana leo hii sisi kama nchi bila kujikita huko ambako kunagusa akili bandia, wengine wanaita akili mnemba (Artificial Intelligence) shida ipo. Majuzi hapa mnaona kuna hiki kitu wanaita optic fibre, ilipata shida, tulipata tabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo watu wetu katika suala zima la mipango, tusipojikita huko ambapo dunia ndiyo ipo huko tutapata tabu. Nilipokuwa nikifuatilia tunaambiwa hakuna namna, tutafanya bila kubadilishana namna tunavyoweza kuishi, kwa maana ya mapinduzi ya nne ya viwanda. Pia, hapa tulipofika sasa hivi dunia tunaingiliana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo bila ya kwenda huko sisi kama sisi hatuwezi tukabaki peke yetu. Narudia kutoa mfano, tulipata shida ya hiyo optic fibre na watu tuliparaganyika mahospitali, benki, viwanja vya ndege, wote tuliliona. Kwa hiyo, wakati tukizungumzia tunatokaje hapa, tusiache na sisi kujikita huko kwa sababu hatupo peke yetu, lazima tuchanganyike na dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye eneo la madini. Madini kwa ujumla wake nilifurahi kusikia kwamba sekta ya madini iliongezeka kwa kiasi hiki, kutoka dola bilioni 3.12 mwaka 2021 hadi dola 3.55 mwaka 2023. Rai yangu ni kwamba, ili madini yaweze kututoa, tunatakiwa tuangalie hoja za msingi. Tatizo ni nini? Niliwahi kuzungumza hapa suala la tozo. Mbali ya tozo, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri, uende mbali zaidi. Ikiwa tunaambiwa leseni zilizopo... (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapufi, hiyo figure nadhani hujaitamka sawasawa, labda irejee vizuri, toka bilioni tatu point ngapi mpaka bilioni ngapi?
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, bilioni 3.12 kwa maana ya mwaka 2021 hadi dola bilioni 3.55 mwaka 2023. Kwa hiyo, point yangu hapa nilichokuwa naomba sana tusiache kwenda kwenye intelijensia ya uchumi. Kwenye eneo hilo la madini tukumbuke hatupo peke yetu, kuna watu wengine wanachimba pia, tusaidie kwenda huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna baadhi ya vitu hapa na inatakiwa watu wa mipango mtuambie, nimekuta huko kwenye vyombo vya habari tunaambiwa, kwa mfano eneo la matangazo tu na watu tunashindwa kuelewa matangazo yanaweza yakawa ni biashara. Leo baadhi ya nchi, ndege yao wameiandika Ngorongoro Crater. Mtu unajiuliza, hivi wamefanya kwa kubahatisha au kuna kitu wana-aim at? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani tunatakiwa kwa maana ya intelijensia ya uchumi twende huko. Yawezekana fedha ile ambayo ilitakiwa ije nchini kwa kuandika tu, watu wakatengeneza fedha. Sasa Watanzania tunasemaje katika maeneo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunapata shida baadhi ya nchi huko duniani wanaendelea kufikiri kwamba Mlima Kilimanjaro upo kwao, na Watanzania tunakalia hizo fursa. Tunatakiwa tutoke kwa maana ya dunia ya sasa hivi. Ndiyo maana nasema hatuwezi tukakwepa hii awamu ya nne ya maendeleo ya viwanda kwa maana, kama wenzetu wanafanya matangazo, wanajaribu kuishawishi dunia na sisi kwa maana ya uchumi mpana tufike huko, huko hakukwepeki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kwa kumalizia, nilikuwa naomba mipango mizuri ambayo imefanyika na mama yetu kwa maana ya kuboresha sekta nzima ya afya, hivyo vifaatiba vilivyoongezeka tutoke kwenye eneo hilo, tufanye eneo la afya pia kuwa ni eneo ambalo tunaweza tukafanya utalii wa tiba na hiyo ikawa ni sehemu ya kupata mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)