Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kilwa Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuzungumza jioni ya leo. Kwanza nitangulie kuishukuru Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa namna ambavyo imetuunga mkono sisi wa Wilaya ya Kilwa baada ya kupatwa na janga la mafuriko yaliyosababishwa na mvua za El-Nino ambazo zilianza mwezi Oktoba hadi mwezi Mei na Kimbunga Hidaya ambacho kilitokea tarehe 3 hadi 5 mwezi Mei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kimbunga hiki na mafuriko haya yaliacha athari kubwa ambapo kaya takribani 2,096 ziliathirika, wakazi 8,397 waliathirika na kadhia hii, nyumba zaidi ya 1,160 zilizolewa na mafuriko na hekta 28,000 za mashamba ziliharibiwa na mafuriko. Kwa hiyo, napenda kutoa pongezi na shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo aliweza kuidhinisha pesa nyingi zikaweza kutumika kwenda kutusaidia kupunguza athari na kuondoa athari za janga hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Innocent Bashungwa kwa kazi nzuri ambayo amefanya ya kurejesha mawasiliano ya barabara kuu na barabara za mikoa. Mheshimiwa Jenista Mhagama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mheshimiwa Hussein Bashe, ambaye ametuahidi kutuletea miche 66,625 ya minazi na pia namshukuru Mheshimiwa RC wa Mkoa wa Lindi Mheshimiwa Zainab Telack kwa kutekeleza majukumu yake vizuri wakati wa janga hili, Mheshimiwa Mohamed Abdallah Nyundo DC wa Wilaya ya Kilwa, DED Wilaya ya Kilwa Bi. Hanan Bafagih, pia Mheshimiwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilwa Said Timami; sisi Wabunge kwa umoja wetu ambao tulishirikiana na mamlaka zote za Serikali, Mheshimiwa Rajabu Ngatanda, Diwani Kata ya Tingi, Mheshimiwa Said Manjonjo, Diwani Kata ya Somanga na Mzee wetu Shaweji Kimbwembwe au almaarufu Mzee wa Jogoo ambaye kwa hakika alikuwepo katika kila eneo ambapo mafuriko haya yalisababisha athari mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, napenda kuishukuru Taasisi ya AUWA (Asili ya Wamatumbi na Uzalendo Wao), Jeshi la Zimamoto na Uokozi, TANROADS, TAWA, Kanisa la AICC, Kanisa la EPCT, Taasisi ya Bin Shomari, Blue Springs ya Ujerumani, MSD, BAKWATA, Benki ya NMB, TRA, UNICEF pamoja na Umoja wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kilwa Masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa shukrani hizo za dhati nawatakia kila la heri wale wote ambao walitusaidia na Mwenyezi Mungu awarejeshee pale ambapo walitoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupongeza na kuunga mkono bajeti hii, nampongeza Mheshimiwa Waziri rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu, ambaye alikuwa anasimamia utoaji wa mafungu. Nimemsikia katika hotuba yake ukurasa wa 155, amezungumzia suala la kutengeneza ule mfuko wa kusaidia athari za maafa mbalimbali, kwa kweli hapa amecheza kama Azizi Ki. Hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa hizo fedha zilizopangwa kukusanywa, zikusanywe kweli kweli ili linapotokea janga kama hili, basi tuweze kulishughulikia mara tu changamoto inapojitokeza. Hii itasaidia kurejesha mawasiliano na miundombinu mbalimbali kama ilivyotokea mwaka huu kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kushukuru na kupongeza hotuba ya bajeti kwa kuongeza malipo ya kikokotoo kwa wastaafu wetu, katika ukurasa wa 102 hadi 103. Kwa kweli hili ni jambo jema ambalo lilileta mgogoro mkubwa sana katika jamii na kwa kweli sasa tunaenda kupata mwarubaini katika jambo hili, isipokuwa nilikuwa nina angalizo eneo moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi kufanyika uhakiki wa Watumishi wetu waliostaafu, na mara zote uhakiki unafanyikia mikoani. Naomba jukumu hili sasa lipelekwe kwenye ngazi ya Tarafa kwa sababu tunafahamu hawa watumishi wanaokwenda kuhakiki hawa watumishi wastaafu wana vifaa, wana magari na kadhalika. Tofauti na hawa watumishi ambao wamekuwa wengi ni wazee, hawana nguvu ya kifedha ya kutosha ya kuweza kusafiri kwenda mikoani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, sitarajii Mwalimu wangu Swaleh Mweru anaishi Nandete leo umtembeze zaidi ya kilomita 300 kufuata haki zake au kufuata uhakiki. Kuna Mwalimu Said Ngomba yupo kule Mtende na kuna Mwalimu Emiliana Mandai yupo kule Kipatimu wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 300 kufuata haki zao au kufuata huo uhakiki. Kwa hiyo, naomba Serikali irekebishe hili ili kuboresha mambo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuzungumzia suala la mifumo. Mifumo yetu imekuwa sumbufu sana katika malipo. Licha ya bajeti ambayo tuliipitisha mwaka 2023 na mwaka 2022, utekelezaji wake umekuwa mgumu hasa kwenye kipengele cha malipo. Kwa mfano, kule kwenye Halmashauri yetu ya Wilaya ya Kilwa, mpaka leo fedha za Mfuko wa Jimbo shilingi milioni 68 hazijaenda kwa walengwa. Tulitenga shilingi milioni 20 kati ya shilingi milioni 68 za Mfuko wa Jimbo ziende zikarekebishe huduma ya visima kule Kibata, imeshindikana mpaka wakati huu, mifumo inasumbua; Mfumo wa MUSE unasumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hela za MSD ambazo zilipangwa kununua madawa na vifaatiba, zimekwama, nazo ni shilingi milioni 780, lakini kuna fedha za mapato ya ndani cha kushangaza. Shilingi milioni 53 tulipanga zikaanze kujenga Zahanati ya Njinjo ambayo iliathiriwa na mafuriko ya mwaka 2020, zimeshindikana mpaka wakati huu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri, basi afanye jitihada angalau inapofika wiki ijayo, tuone fedha hizo zimefika na siku zijazo katika utekelezaji wa bajeti ya shilingi bilioni 49 tuone fedha zikifika, zinaenda kutumika moja kwa moja ili kuongeza ufanisi na tija katika miradi ambayo tumelenga kuitekeleza kama ambavyo imepangwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, alitueleza hapa mwaka 2023, tungejengewa kilomita 72 kwa kiwango cha lami kati ya kilomita 230 za barabara za Nangurukuru -Liwale lakini sijasikia hata wakati akiwasilisha hoja za Wizara yake. Naomba atupe maelezo, watu kule tumeshawaambia lami inakuja (joka jeusi linakuja), lakini mpaka leo hatujaona juhudi zozote. Tunaomba maelezo huu mradi unatekelezwa lini na taratibu za zabuni zipoje na kadhalika. Pia, katika mradi wa barabara nne pale kutoka Mbagala Rangi Tatu kwenda Kongowe nao ningeomba mtusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kuipongeza Serikali, tumeshatekeleza miradi mingi na leo hii nimepata taarifa kuwa jumla ya shilingi milioni 560 zitaingia muda wowote kwenda kutekeleza Mradi wa Shule ya Sekondari Mt. Kimwaga, Kata ya Kipatimu. Naipongeza Serikali. VETA inaendelea kujengwa mwaka huu 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mara ya kwanza Serikali imetenga bajeti kubwa kwa Taasisi ya TARURA pengine kuzidi hata ile ya TANROADS. Kwa hiyo, imeonesha namna gani kule vijijini ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mazao kumewekewa mkazo wa kuboresha barabara zake ili mazao yaweze kusafirishwa kupelekwa sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada yakusema hayo, nasema naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)