Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Abdallah Jafari Chaurembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbagala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami kutoa mchango wangu katika Wizara hizi mbili ambazo zipo mbele yetu leo. Kwanza, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametuwezesha leo kuwepo hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mambo makubwa ambayo ameyafanya kwenye nchi hii katika nyanja ya elimu, reli, barabara, umeme, maji na mambo mengi ambayo yalikuwa kero, na kwa kweli yameenda kutatulika kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita sana katika mipango yetu ya maendeleo ambayo inabidi iendane na Sensa ya Watu na Makazi. Maendeleo ambayo tunapanga ni vyema yakaendana na sensa ambayo tumetoka kutoa taarifa zake hivi karibuni. Taarifa za sensa zinaonesha idadi ya watu kuanzia kwenye mitaa mpaka Taifa, kwa hiyo, na maendeleo nayo yaendane na idadi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tufike mahali tuone kwa idadi hii ya watu waliokuwepo katika kila Mkoa, je, miundombinu ya elimu iliyokuwepo inaendana na idadi ya watu? Kama haiendani na idadi ya watu, je, Serikali tunakuja na mpango gani? Hapa namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, kwa kiasi fulani amejitahidi sana iwe fedha za vyanzo au vyovyote, lakini tumeona namna ambavyo shule zimekuja nyingi katika maeneo yetu. Kwa hiyo, inaonesha ni jinsi gani Sensa ya Watu na Makazi imesababisha kupata maendeleo katika nyanja hii ya elimu msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo nataka nijikite sana kwenye barabara kwa sababu nafahamu tulikuwa na Wizara ya TAMISEMI, tumejadili barabara na Wizara ya Miundombinu kwa maana ya Ujenzi tumejadili mambo ya TANROADS. Haya yote tuliyoyajadili, anayefanya mambo yaende ni Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia bajeti, Wizara hizi mbili zinaweka mipango yake katika maandishi, lakini ukweli tunahitaji fedha kutoka katika Wizara ya Fedha. Hoja yangu ya msingi ni kwamba, hebu tuangalie idadi ya watu waliokuwepo Mkoa wa Dar es Salaam, idadi ya watu waliopo katika Majimbo ya Mbagala na Ukonga na kiasi cha kilometa za barabara za TANROADS na TARURA tulizopangiwa, zipo sawa kulingana na ukubwa wa barabara zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha endapo hawataleta fedha kwa ajili ya kujenga kilometa tano mpaka sita, kwa kweli watakuwa hawajatutendea haki Mkoa wa Dar es Salaam, na majimbo haya niliyoyasema. Siasa ya Dar es Salaam kwa sasa ni barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua takwimu ya barabara za TANROADS zinazohitajika Dar es Salaam nzima haziwezi kufika kilometa 100. Sasa msipotupa barabara zote zilizowekwa kwenye bajeti za Dar es Salaam, mjue hamjatutendea haki. Tumepitisha bajeti kubwa ya Kilimo na mambo mengine, ni nzuri, lakini Dar es Salaam kilimo chetu sisi ni kwenye barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Kokoto mpaka Kongowe, Mheshimiwa Ndulane ameizungumzia, unaweza ukajiuliza, Mheshimiwa Ndulane sio Mbunge wa Dar es Salaam, kwa nini ameizungumza? Ni kwa sababu, ndiyo lango la kutokea kwao kuingia Dar es Salaam. Ukitaka kutoka Dar es Salaam kwenda Kusini, lazima upite barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo imewekwa kwenye bajeti zaidi ya miaka mitano, lakini utekelezaji haupo. Wizara inayotoa fedha ni Wizara ya Fedha, hebu waoneeni huruma, chukueni takwimu, ni wananchi wangapi wamekufa katika barabara ile katika kipindi kifupi? Juzi tu wananchi watano wamekufa, gari limeshindwa kupanda, limerudi nyuma limeua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalieni kwa jicho la huruma. Barabara ile hai-save watu wa Dar es Salaam tu wala watu wa Mbagala, inawa-save watu wa Mikoa ya Kusini, Pwani na maeneo mengine. Hebu wekeni fedha safari hii. Wananchi wa pale wamethaminiwa nyumba zao zaidi ya miaka 10, hawajengi, hawaongezi kitu, na hatuwalipi fedha zao. Naomba sana Wizara ya Fedha tuwalipe fedha zao, tupanue ile barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Dar es Salaam sasa hivi ni Jimbo la Mbagala lenye foleni ya bodaboda. Mpaka bodaboda sasa hivi zinaenda kwa foleni kwa maana barabara zote zimejaa na zimefurika kwa msongamano. Wizara ya Fedha hizo kilometa chache za barabara tunazopangiwa, hebu toeni fedha ziende zikatengenezwe. Leo barabara inayotoka Rangi Tatu kwenda Mbande imekuwa ni changamoto kubwa, watu wanatembea kwa miguu, bodaboda zinakaa foleni, barabara zimezidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ni matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi. Mheshimiwa Kitila wewe upo katika Wizara ya Mipango, unapoona idadi ya watu ni kubwa elekeza mipango yako katika maeneo hayo. La sivyo, maeneo hayo hayataweza kupata maendeleo kwa kuwa kuna msongamano mkubwa wa watu na mipango iliyopangwa haiendani na wingi wa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunamshukuru sana Waziri wetu wa Ardhi, Mheshimiwa Jerry Silaa, ameenda kutatua migogoro ya ardhi, lakini nataka nimwambie kwa Dar es Salaam na kwa idadi ya sensa ya watu na makazi tunamwelewa, tunamheshimu na wananchi hatutavamia viwanja vya mtu, lakini kwa taasisi za Serikali ambazo wana viwanja na hawajengi, kwa population ile tukajenge wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hapa muda mrefu, Waziri wa Mipango upo, NSSF wana mipango yao ambayo haitekelezeki. Sisi hatuna maeneo ya kwenda, wananchi waende wapi?

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya nakusikiliza, Taarifa. (Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jerry Silaa, Waziri wa Ardhi.

TAARIFA

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Chaurembo kwa mchango wake mzuri, lakini naomba kumpa taarifa fupi kwamba, kwa namna yoyote uvamizi wa ardhi ni suala ambalo halikubaliki. Kwa hiyo, namwomba sana kama kiongozi na mwakilishi wa wananchi, pamoja na ongezeko la watu Dar es Salaam anaweza kuwasilisha na Serikali tumesikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutatengeneza mpango mzuri wa matumizi ya ardhi, lakini ni vyema tukaheshimu maeneo yanayomilikiwa na watu binafsi, maeneo ya umma na maeneo ya Taasisi za Umma bila kuyavamia kwa sababu ni maeneo yetu sisi wote Watanzania.

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Abdallah Jafar Chaurembo unaipokea Taarifa?

MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa nimeipokea, lakini hiyo hiyo Sheria ya Ardhi inaeleza, naye ni msomi mzuri, Mwanasheria, kwamba eneo lisipofanyiwa kazi kwa muda mrefu na mwananchi akaingia pale, tumia sheria hiyohiyo kumfanya mwananchi awepo. Hakuna Sheria isiyokuwa na mbadala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NSSF wana zaidi ya miaka 20 hawaendelezi maeneo. Wananchi wa Malela, Mwapemba wameendeleza. Tunao mpango, tulizungumza nao, tulikaa tukakubaliana kwamba kwa kuwa NSSF maeneo yale wanataka kuuza, wananchi wapo tayari, wawakatie, wayathaminishe, wawauzie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwananchi ametafuta hela kwa tabu, amejenga nyumba yake kwa tabu, leo hii nyumba imekamilika, NSSF wapo kazini wanavunja majumba ya watu. Sawa, tunakubali ni sheria, lakini wale watu wamekaa pale ndani ya muda gani? Kwa nini hatuwezi kukaa tukakubaliana kama kulipa mimi nikachukua kiinua mgongo changu nikawalipia wananchi wangu wakaendelea kukaa kuliko kuvunjiwa nyumba zao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hapa hifadhi, wananchi wamevamia maeneo mengine, Serikali imekaa imeangalia namna bora ya matumizi ya ardhi, wameruhusiwa. Kwa nini isiwe Mbagala?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali katika hili, Mheshimiwa Jenista, Mheshimiwa Jerry Silaa na Waziri wa Mipango, hao wamepanga mipango, wameshindwa kuitekeleza. Naomba tutengeneze utaratibu badala ya kuwavunjia wananchi, basi wananchi wale warasimishwe. Tupo tayari kulipa kuliko kuvunja nyumba zao. Chonde chonde, siwezi kuruka sarakasi, lakini nitakachoweza kufanya, nitawasomea Ahlul-Badr. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)