Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi hii nami nitoe mawili matatu kwenye hotuba ya Serikali. Mara nyingi huwa mnatuambia kwamba Serikali ni Sikivu, itasikia, pengine ngoja tuendelee kuongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaongelea Bajeti ya 2024/2025. Kuongezeka kwa bajeti au kuongezeka kwa fedha, Taarifa ya Kamati inasema kwamba, ongezeko hilo linatokana na mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, sehemu kubwa ya bajeti yetu itakwenda kwenye kulipa deni la Taifa, wote tumesoma na tumeona sehemu kubwa tena itaenda kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, sehemu nyingie itaenda kwenye Maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, hela nyingine itaenda kwenye ajira mpya na ulipaji wa hati za madai. Eneo lingine linaenda kugharamia Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050. Kwa hiyo, hiyo ni sura ndogo ya gharama ya bajeti tunayoiongelea hapa. Kwa nini nasema hapa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha kubwa ambazo tumekuwa tukizipanga Bungeni zinaenda kwenye gharama za matumizi ya kawaida. Ukiangalia hata bajeti tuliyonayo ni kama iliyopita, fedha nyingi zinaenda kwenye recurrent. Zinaenda kwenye matumizi ya kununua hiki, kufanya hili, lakini siyo fedha za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawezaje kuondoka tukawa na maendeleo bila kuwa tunapanga bajeti kwa ajili ya fedha za maendeleo? Hilo ni swali ambalo nataka niwaulize wanaomwakilisha Mheshimiwa Rais humu ndani; Waziri wa Fedha, Waziri wa Mipango na Wasaidizi wao, tunawezaje kufikia maendeleo kama kila bajeti tutakuwa tunaongelea spending? Kwa nini nasema hapa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na bajeti ambayo katika 100%, 68% inaenda kwenye matumizi ya kawaida na 32% inaenda kwenye matumizi ya maendeleo. Lazima tuangalie ni wapi tunaweza kwenda kujibana, ili 32% iwe ya matumizi ya kawaida na 68% ije kwenye matumizi ya maendeleo. Hapo ndiyo tunaweza ku-archive tunachokitaka, otherwise tutakuwa tunakuja kuongelea mikopo ya riba nafuu na mambo kadha wa kadha ambayo hayapendezi kwenye masikio ya walio wengi. Nikaanza kupitia nione ni kwa nini Serikali imekuwa inatumia fedha nyingi sana? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikachukuwa mfano wa kitu kidogo tu, ununuzi wa magari. Kumekuwa na ununuzi mkubwa sana wa magari kwenye halmashauri. Nikachukuwa bajeti kadha wa kadha, Serikali imekuwa inaongelea nini katika ununuzi wa magari? Nikachukuwa bajeti. Mfano, Hotuba ya Bajeti ya TAMISEMI ya mwaka 2019/2020 ilieleza, Serikali imepanga kununua magari 54 ya shilingi bilioni 4.48; hiyo ni 2019/2020. Tukaja mwaka 2020/2021, ikasema Serikali imetenga shilingi bilioni 29.83, kwa ajili ya magari 234 na hapa akataja magari 16 yataenda kwenye mikoa na magari 184 yataenda kwenye Halmashauri. Hiyo ni hotuba ya mwaka 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaitafuta Hotuba ya mwaka 2021/2022. Wakasema shilingi bilioni 2.8 zitaenda kununua magari nane, kwa ajili ya Wakuu wa Mikoa na Tawala. Tukatoka hapo nikaingia kwenye bajeti iliyofuata mwaka 2022/2023, Hotuba ya Kamati ya Bajeti ikaongelea kwamba, Serikali ilitumia au ilipanga na kutumia zaidi ya shilingi bilioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa magari na wao kwenye ushauri wao wakaeleza kwamba, ni lazima Serikali iangalie haya matumizi ya magari. Nikachukuwa moja ya script ya Hotuba ya Wizara ya TAMISEMI juu ya gharama zenyewe za magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa magari ya viongozi kwa ngazi ya Mkoa, Wilaya na Halmashauri kwa Mwaka 2020/2021; Mkoa wa Katavi gari moja la RAS shilingi milioni 300, Mlibwebwe DC gari moja shilingi milioni 220. Hotuba inaenda mpaka pale chini. Nataka niulize, tunaweza kwenda wapi na ununuzi wa magari ya namna hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lingine ni kwamba, kwa kiwango gani haya magari ambayo yamekuwa yananunuliwa kwenye halmashauri, halmashauri yenyewe ina mapato madogo, lakini unaipelekea gari la shilingi milioni 300; kuna gari la Mkuu wa Mkoa, kuna gari la Mkuu wa Wilaya, kuna gari la RAS, na uongozi mwingine mnaoujua. Ni kwa kiwango gani sasa tunaweza kuangalia value for money unapopeleka magari ya zaidi ya shilingi milioni 800 kwenye halmashauri moja? Value for money tunayoipata ni kiasi gani? Ni fedha kiasi gani halmashauri zina-collect ili kutuwezesha sisi kuona thamani ya kuwapelekea magari haya yote? Ni kwa nini tunapeleka hayo magari? Wananchi kwenye halmashauri husika, ukifanya sensa, wanatumia magari ya aina gani? Ni kwa nini wao watumie mashangingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nipate jibu la ni kwa nini tunatumia magari ya namna ile, tukikumbuka kwamba, hayo mashangingi tunayanunua kila siku latest, tunapeleka ajira Japan, tunapeleka fedha Japan, tunapeleka kila kitu Japan? Unapokuwa na nchi inayokuwa ina-think of spending zaidi ya kuwaza kutengeneza fedha na kutengeneza maendeleo ya watu wake then tujue kwamba, hapa kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Mawaziri wetu, hebu tusaidieni namna tunavyoweza kubana matumizi katika matumizi ya fedha. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali imeeleza utaratibu mbovu ambao umekuwa ukitumika ku-dispose hayo magari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, gari hata likipata ajali ndogo, likiegeshwa kwenye gereji, halitoki mpaka miaka minne na value yake inashuka. Gari mmenunua shilingi milioni 300, baada ya miaka miwili limepata ajali ya kawaida, anakuja kuuziwa mtumishi chini kwa chini zaidi ya shilingi milioni 10. Tumeona hayo na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali ameeleza hayo. Hiyo ndiyo namna tunayoweza kuisaidia hii Serikali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kuja hapa tunaongea mlolongo wa namna ya kutafuta fedha. Tunataka kutafuta fedha zipi kama hatuwezi kutunza hizi chache tulizonazo? Naomba hilo tuliangalie upya na utaratibu wa kwenye Halmashauri, tunapeleka gari baada ya muda gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kamati ya Bajeti na Wabunge wamewahi kushauri kwamba, tunapokwenda sasa tuwaze kuwakopesha hao watumishi magari badala ya kuwapa magari ya Serikali. Wamekuwa hawana custodian ya yale magari kwa sababu ya ajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tukaenda mbali zaidi, nataka hapa niongelee pendekezo ambalo analileta Mheshimiwa Waziri, nadhani ni Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura Na. 220. Humu Bungeni tulikuwa tunajadili namna ambavyo tunaweza kusaidia magari ya Serikali badala ya kutumia diesel na petrol ambayo inakuwa imported na it is very expensive, twende kwenye gesi asilia tunayozalisha hapa nchini. Leo naona trend imebadilika na badala yake Wizara inakuja na tozo ya shilingi 382 kwenye kilo moja ya gesi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hiyo haikubaliki. Siyo tu kwa kuwa friendly kwa mazingira, lakini haikubaliki kwa mpango wa kuendelea kuchukua fedha, kuendelea kununua dola. Tunavyoendelea kuweka matumizi ya kuongeza kutumia dola tuna-encourage fedha kuzidi kuishiwa nguvu, kukosa fedha na kuendelea kuwa dependant. Kwa hiyo, hayo mambo siyaafiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hayo tu, naongezea hapo. Mnakuja na Sheria ya Sukari, Sura Na. 251, kuwezesha NFRA kununua sukari ghafi. Hiyo haikubaliki kokote, na haiwezekani. Tunataka kuua viwanda vya sukari tulivyonavyo hapa! Tunataka kuhamisha ajira za Watanzania wenzetu! Tunataka mashamba makubwa ambayo yameanzishwa leo yafanye kazi gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala yake hizi dola mnazotaka kuzipeleka nje, vikopesheni hivi viwanda viweze kuzalisha vya kutosha tutengeneze ajira za watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana, kama tunaweza kuwa na thinking ya namna ile, hii ni ya kuliumiza Taifa. Badala ya kuwaza kuhamisha fedha, tuanze kurudisha fedha hizi ziwasaidie wananchi wetu, tuweze kurudisha fedha, ili tuweze kutengeneza uchumi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tuangalie bajeti tuliyonayo leo. Hii bajeti yetu pamoja na mambo mengine, hapa Taarifa ya Kamati imeeleza hivi, kwanza ukopaji wa mikopo ya masharti, tunaita concession loans, umeongezeka kwa 48% kutoka kwenye ile tuliyokuwanayo. Ina maana mikopo imeongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, ukiangalia mapato tuliyonayo TRA inachoweza ku-collect, mapato yasiyokuwa ya kikodi, lakini pia na Halmashauri tunaweza kuitegemeza bajeti yetu kwa 70% tu. Kwa hiyo, unaona kwamba sisi ni production for consumption with diversity. Tunazalisha, tunatumia na tuna-diversify. Sasa hili ni Taifa la namna gani jamani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha tunazoweza ku-collect hatuendi kulipa wakandarasi kwa wakati, tunaenda kulipa riba. Hapa Taarifa ya Kamati imeeleza vizuri sana, fedha mamilioni na mabilioni ambayo wakandarasi wanadai tunaenda kulipa riba kwenye miradi ya maji, tunaenda kulipa riba kwenye miradi ya barabara. Taarifa ya Kamati imeeleza vizuri ni kwa nini tunaingia kwenye commitment ya mikataba wakati hatujapata fedha? Kwamba, Maafisa Masuuli wana-incur commitment za spending wakati hawana fedha, ukifika wakati certificate zimefikia ku-mature wanapaswa kulipa, hawalipi. Ni kwa nini tunaenda hivi na ni kwa nini tunafanya hivi? Tunaiongezea Serikali mzigo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila siku tunabanana hapa kwa ajili ya spending, kwa ajili ya kulipana mishahara, kwa ajili ya fedha kupotea na mambo mengine kama hayo. Mimi nashauri sana, lakini unaona tumekuwa tukiongea humu ndani kuwa na bajeti ambazo zinakuwa na mrengo wa kijinsia. Ni kwa kiwango gani bajeti zinakuwa zipo sensitive kwa wanawake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nieleze wazi. Bajeti ya Wizara ya Maji imeshuka na inavyoshuka wanaoathirika kwa kiwango kikubwa ni wanawake ambao wao ndio wanachota maji wakati wanaume hawapo, wanabaki nyumbani wanahangaika. Naomba Mheshimiwa Waziri hili mliangalie upya na halikubaliki. Hiyo ndiyo namna pekee tunayoweza kuongelea bajeti ambazo zipo sensitive, lakini zinawagusa wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uchache, naenda kwenye Jimbo la Kyerwa. Tuna changamoto kadha wa kadha. Changamoto ya kwanza ni barabara na hata asubuhi nimeeleza changamoto ya barabara. Sisi tuna barabara mbili tu; barabara ya kutoka Bugene – Nkwenda, unakuja Kaisho unakuja kutokea Murongo, lakini hiyo barabara unatoka Murongo unakuja Businde, unakuja kutokea Omgakorongo. Hizo ndizo barabara mbili tulizonazo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi barabara zetu hazitengenezwi tangu mkoloni. Mmetuahidi kilometa 50 za Nkwenda, lakini imekuwa ni ngonjera kila siku. Ninachosikitika sasa wakati Mbunge mmoja amesema hapa kwamba, wengine barabara zilibanduka, sisi hata hiyo ya kubanduka, watoto hawajawahi kuiona lami. Siyo sahihi. Sisi ni walipa kodi, tunastahili lami. Serikali mmeahidi kilometa 50 za lami nami sina uhakika kama naweza kuunga mkono hii bajeti iwapo sisikii chochote kuhusu kuanza kwa hiyo lami. Siyo hiyo tu ya kilometa 50, lakini pia, kulipa fidia kwa wananchi wa Mgakorongo kuja kutokea mpaka Mrongo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hiyo tu, nimeongelea changamoto ya vitambulisho vya NIDA. Naongea kwa uchungu sana, Wilaya zetu za mpakani ikiwemo Kyerwa, kumekuwa na changamoto ya kubambikiziana kwamba, wewe sio raia. Ukionekana unajitambua, unaweza kujisimamia, upo kwenye siasa, unaambiwa wewe sio raia. Wanakunyima kitambulisho, wanaanza kukubambika kwamba, sio raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba uwepo mkakati maalum wa kuja kuandikisha vitambulisho, kama nilivyosema juzi na badala yake tuwe na Maafisa Uhamiaji wanaotufahamu. Mnatuletea watu kutoka wapi, wanaanza kusema huyu ana pua ndefu, huyu fupi na wale hawajui watu wa huko kwetu wanafananaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, muda wangu siyo rafiki. (Makofi)