Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kusema mawili matatu kwenye bajeti hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kabisa, nachukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Amekuwa ni Rais ambaye amewatazama Watanzania katika hali zao na kuwahudumia kama ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, nachukua nafasi hii kumshukuru na kuwashukuru wasaidizi wake, Makamu na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa namna ambavyo wanamsaidia Mheshimiwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan katika kulitumikia Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba ifahamike mpaka dakika ya sasa kwamba, tunaposimama kama Wabunge wa Mkoa wa Kigoma bado mahitaji yetu hayajatekelezwa na ndiyo maana tunasimama kwanza, kukumbusha; na pili, kuieleza Serikali yetu sikivu ili iweze kufahamu namna gani watu wa Kigoma tuna uhitaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mikoa yote ya Tanzania mpaka dakika hii tunayozungumza mikoa yote imeshaunganishwa kwa lami, imebaki Kigoma peke yake na sehemu iliyobaki ni ndogo sana ambayo nasimama leo kumwomba sana kaka yangu Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kuona namna ambavyo atatutoa katika hii dhahama Watu wa Kigoma ili nasi tuweze kuingia kwenye record ya kuweza kuwa miongoni mwa mikoa iliyounganishwa kwa lami kama ilivyo mikoa mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti...
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Makanika, kuna Taarifa.
TAARIFA
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Taarifa mchangiaji, anachangia vizuri sana, lakini siyo kweli kwamba nchi yote imeunganishwa, ila bado Mkoa wa Kigoma tu. Sisi wa Lindi na Morogoro bado hatujaunganishwa kwa kiwango cha lami.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Makanika.
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendelea na hoja yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kigoma tuna barabara hii ya Uvinza ambayo barabara hii ilikuwa inatokea...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Makanika, Kanuni za Kudumu za Bunge, Kanuni ya 77 inakutaka useme au unaipokea au hupokei taarifa.
MHE. ASSA N. MAKANIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Serikali nayo iweze kumwona. Nimesikia taarifa yake na nimeipokea. Serikali iweze kuona umuhimu wa kumwezesha naye pia ili na mkoa wake uweze kuunganishwa kwa lami ikiwa ni mahitaji ya Watanzania wa maeneo mbalimbali, lakini ni sisi Kigoma na maeneo aliyotaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Barabara hii ya Uvinza ambayo imeanzia Tabora. Barabara hii kipande cha Tabora sasa kimekamilika kwa lami lakini ukija kipande kinachoiunganisha Kigoma kutokea Tabora bado kilometa 51 mpaka sasa. Kwa kweli tunaiomba Serikali ya Mama yetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iweze kuona namna bora ambayo itatuwezesha sisi watu wa Kigoma tuingie kwenye uchaguzi kipande hiki kikiwa kimekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba, ukiangalia barabara hii na mkandarasi aliyepo, bado anasuasua na tunaomba kwa kweli Serikali iweze kutia mkazo sana fedha zipelekwe na mkandarasi yule aweze kulipwa ili kipande hiki kiweze kuendelea kwa haraka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, tuna barabara ambayo tumeishaieleza Serikali, kutokea Mwandiga inakwenda mpaka Kata ya Mwamgongo na baadaye inaelekea kwenye Soko la Kimataifa la kule Kagunga. Barabara hii imekuwa ni changamoto sana, ambapo toka nimeingia Bungeni nimeipigia kelele sana ya kwamba watu wa Ukanda wa Ziwa na wao. Ni wakati mwafaka sasa Serikali iweze kuona namna bora ipeleke miundombinu hii ya barabara ili iweze kufika katika kata hizo zaidi ya nne ambazo bado hazijafunguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekaa sana na Mheshimiwa Waziri Bashungwa. Tumekwenda Wizarani kwake, tumezungumza naye sana kama Wabunge wa Mkoa wa Kigoma, naomba sana mtani wangu aweze kuangalia namna bora ambayo ataweza kuzifungua hizi kata nne ili ziweze kupata miundombinu hii ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na muda, naomba niseme juu ya hali ya biashara katika Mkoa wetu wa Kigoma na nchi ya jirani ambayo sisi watu wa Kigoma tunategemea biashara hii kuweza kukua kwa haraka kwa sababu ndiyo uchumi mkubwa wa Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za Benki ya Dunia za mwaka 2009 zinaonesha bidhaa ambazo zimepita katika mpaka wa Kigoma zenye thamani ya dola bilioni 600 zimepita katika mpaka wetu wa Kigoma lakini ukichukulia mipaka hii mingine, mpaka wa Tanga, Arusha, Holili na kwenda mpaka Namanga, thamani ya fedha zilizopita pale ni thamani ya dola bilioni 500. Ukiangalia mpaka wa Kigoma peke yake umeweza kuipiku hii mipaka yote mingine kutoka mwaka 2019. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hali ya Bandari ile ya Kigoma imekuwa ni kavu sana. Ukiangalia, ni meli moja tu ndiyo utaikuta pale inashusha, lakini ukienda upande wa pili utakuta meli nyingi zinachanganya kupakia na kushusha mizigo kwa ajili ya kuelekea katika maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababisha wafanyabiashara wa huko Karema, Lubumbashi hata Kabwe nchini Congo, hivi sasa wanakwenda kupita nchi ya Burundi kwenda kufanya biashara zao nchi ya Burundi na wengine sasa wanaingia nchini Uganda na sababu kubwa peke yake ni urasimu ambao unaendelea katika Bandari yetu ya pale Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri anaweza akalitazama hili. Hawa wafanyabiashara wanaokimbilia Mombasa wanakwenda Burundi, wanakwenda mpaka nchini Rwanda walikuwa wanapitisha mizigo mingi katika Bandari ya Kigoma, lakini hivi sasa wamekimbia. Jambo ni dogo tu; zipo Sheria ya Vipimo ambayo imeweza kuumiza uchumi wa Mkoa wetu wa Kigoma kwa kiwango kikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo sheria ya vipimo inaitwa Sheria ya Vipimo vya Habatani inaweza ikatazamwa kwa umakini zaidi kwa sababu inachepusha biashara nyingi ambazo zinakwenda kwenye hizo nchi ambazo nimezitaja na Sheria hii ya Habatani inachukua tu sura mbili; sura ya kwanza ni Sheria ya Kipimo ambayo inapima kwa uzito na kwa ukubwa. Hii kwa ukubwa, kitaalam ndiyo CBM ambayo hivi sasa, hii sheria imeweka mandatory ya sheria au kiwango cha kodi yoyote inayotozwa inaamuliwa na Afisa wa pale bandari, jambo ambalo linatoa mianya mikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wa hizi nchi wanakimbia bandari yetu kwa sababu kumekuwa na urasimu mkubwa. Kwa hiyo, na hilo Mheshimiwa Waziri na Bunge tuweze kuona namna hii sheria itaweza kubadilishwa hatimaye tuweze kukomboa uchumi huu wa Kigoma na Bandari yetu ya Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja kwa sababu ni bajeti ambayo inabeba mambo yote yanayohusu wananchi. Tumeweza kuzungumza juu ya jambo la Ziwa. Kwa kweli hali ya kufunga Ziwa tunaona kwamba imeweza kuumiza uchumi mkubwa wa wavuvi wengi katika Mkoa wetu wa Kigoma. Sasa hii imesababisha hali ambayo uchumi wa watu wetu umezorota kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano tu mdogo, hivi sasa kumekuwa na vizimba ambavyo vimeletwa huko Kigoma, lakini vizimba 29 vimejengwa katika Jimbo la Kigoma Mjini na kwenda kule ziwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia katika Jimbo la Kigoma Kaskazini hakuna hata kizimba kimoja, na hali hii ambayo imeweza kuwaingiza wananchi wengi kwenye hali ya dimbwi la umaskini kwa sababu ziwa limefungwa, lakini ukilinganisha mkataba ule wa kufunga ziwa ulikuwa ni wa zaidi ya nchi tatu mpaka nne. Hali hii tunaomba sana Serikali iweze kutazama namna bora ili tuweze kuangalia kwa sababu wananchi waliumizwa. Wananchi walikuwa na mikopo ambao wametoa kwenye mabenki lakini ziwa limefungwa na hali ya uchumi wao umezorota.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya machache hayo, nakushukuru na ninaunga mkono bajeti hii. (Makofi)