Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Jeremiah Mrimi Amsabi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. JEREMIAH M. AMSABI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri ambayo yeye pamoja na Serikali wametekeleza katika Jimbo la Serengeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka hii mitatu iliyopita, Jimbo la Serengeti limepata miradi mikubwa sana ya maji, barabara, elimu, afya na kadhalika. Kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa pamoja na Serikali yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia kwa kuiongoza vizuri nchi yetu katika kuelekea kujenga uchumi mkubwa pamoja na kuondoa umaskini. Katika kuzingatia dhana kubwa kabisa ya ushindani wa uchumi katika mataifa mbalimbali yanayotuzunguka na mataifa mengine pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Wizara hii ya Fedha pamoja na Wizara ya Mipango kwa kazi ya uwasilishaji wa Mpango ule wa Taifa wa Maendeleo pamoja na bajeti ambayo kwa kiasi kikubwa imeonesha kulipeleka Taifa katika kujenga uchumi na kuondoa umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, ninazishauri Wizara hizi mbili kwamba ni vema zikazingatia pia mambo haya makubwa manne tunapoendelea ku-focus kuipeleka nchi yetu katika kujenga uchumi na kuondoa umaskini, kwa sababu Taifa lolote lile ukiangalia wachumi wakubwa duniani wakiwemo akina John Keynes, akina Adam Smith wanasema, Taifa lolote duniani ambalo linataka kukua katika uchumi lazima lizingatie mambo manne. Jambo la kwanza ni lazima lijenge uchumi ambao unategemea sana kilimo pamoja na viwanda, kwa maana ya kwamba lazima tujenge uwezo mkubwa wa uzalishaji katika kilimo na katika viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima Taifa hilo lihakikishe linajenga kwa kiasi kikubwa miundombinu bora na ya kisasa ambayo inagusa maeneo ya mawasiliano na usafirishaji hasa kuelekea katika maeneo yote yenye uzalishaji wa mali. Jambo la tatu ni lazima Taifa lijielekeze katika kujenga uwezo mkubwa wa kiteknolojia na jambo la nne ni lazima Taifa hilo lijielekeze sana katika kujenga rasilimali watu wenye ujuzi mkubwa na ambayo ina nidhamu ya kazi na inayojituma katika kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii pamoja na mpango wetu wa maendeleo, naomba kugusa maeneo mawili tu katika hayo manne, nikianza na eneo hili la ujenzi wa miundombinu bora ya kisasa na inayogusa maeneo ya mawasiliano na usafirishaji katika maeneo yetu tunayoyategemea katika uchumi mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu maeneo yetu tunayoyategemea sana katika uchumi hayajafikiwa vizuri na miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano. Tumejaribu kwa kiasi fulani, naipongeza Serikali imefanya, lakini bado yapo maeneo ambayo ni vema yaweze kuzingatiwa kwa haraka kwa sababu tunajipotezea wenyewe uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uchumi wa mazingira ya ushindani uliopo duniani unapotaka kujenga uchumi ni lazima uchukue mali kutoka kwa mataifa mengine, lazima uchukue fedha kutoka kwa mataifa mengine. Ili uchukue fedha zao na mali zao lazima yale maeneo ya muhimu katika uzalishaji yafikike, lazima mawasiliano yawepo. Huko nyuma kipaumbele chetu katika ujenzi wa miundombinu kilikuwa zaidi katika kuhakikisha kwamba tunaunganisha maeneo ya kiutawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuona haja ya uwepo wa Tume ya Mipango. Leo maeneo yetu yenye uzalishaji mkubwa yapo mengi, lakini nitaje moja ambalo nalifahamu zaidi. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni jambo ambalo lipo wazi, imeendelea kutuingizia pesa nyingi sana. Sasa mataifa ili waje na kuleta pesa, lazima eneo hili lifikike, lakini mpaka leo barabara ile ya kutoka kule Musoma Makutano ambayo inatuunganisha kutoka Kenya inafika Makutano, inapita Butiama – Sanzate – Nata mpaka kule Mugumu na kuunganisha na Hifadhi ya Serengeti haijawahi kukamilika kwa muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naiomba Serikali, jinsi tunavyochelewa kuiunganisha hifadhi hii, watalii wanavyopata shida kufika eneo hili, tunaendelea kujichelewesha katika kujenga uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na Barabara, imekuwepo ajenda ya muda mrefu ya kujenga uwanja wa ndege mkubwa katika eneo hili, lengo kubwa ilikuwa kuona kwamba watalii wanafika eneo hili kwa urahisi na kwa muda mfupi ili tuweze kukusanya pesa hizi za mataifa. Kwa muda mrefu zimeundwa timu nyingi sana huko nyuma. Imewahi kuundwa timu ya kwanza miaka kati ya mwaka 2010 – 2015 haikufika mahali popote. Ikaja timu nyingine ya pili 2017 – 2019, wakaja Maliasili nao wakaunda timu lakini hakuna kilichoendelea, wakaenda watu mpaka nje ya nchi wakazunguka hakuna kitu kilichofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeundwa tena timu nyingine ya nne tarehe 16 Mei, 2024 ipo barua inayoonesha tena timu nyingine ya nne, barua yenye Kumbukumbu Na. CAD.26/3180/1C/117. Barua hii ime-circulate kenye ma-group mengi sana ya mitandao hii ya kijamii, sasa tumejiuliza kwa nini timu nyingi ziundwe? Lazima kuwepo commitment ya fedha. Mimi niishauri sana Wizara, tunahitaji kuingia kwenye kufanya commitment na siyo kutengeneza mipango mingi, siyo kutengeneza timu nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotaka kujenga viwanja, kujenga barabara mbalimbali ndani ya nchi yetu, hatukuunda timu nyingi hivi. Tena tumefanya miradi mikubwa sana bila uwepo wa timu nyingi hizi. Pia ukiangalia wenzetu katika mambo tofauti tofauti hawakuwa na mikakati na mipango mingi ya namna hii. Nitolee mfano tu nchi ya Malawi. Malawi wana eneo dogo kuliko sisi kama kilomita za mraba 200,000 hivi. Sisi ni zaidi ya 940, lakini wana export chai mara 10 zaidi yetu. Sisi tumekuwa na mipango mingi, mikakati mingi ya kitaifa kuhusu kilimo, lakini hatukuwahi kuwazidi watu hawa. Kwa nini? Ni kwa sababu tumekosa commitment ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Wizara hii ya Fedha pamoja na Wizara ya Mipango waone sasa umuhimu wa ku-prioritize maeneo ambayo yanaweza kutuletea uchumi mkubwa ambayo mataifa yanaweza kuja na kuleta fedha. Tujenge miundombinu ikamilike na tukusanye fedha tuweze kuondoa umaskini. Tusipofanya kazi hii tunaendelea kujichelewesha, tunaendelea kufanya Taifa hili kubaki kwenye makusanyo madogo na kutojipatia maendeleo ambayo Watanzania wanakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)