Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami nichangie hotuba ya Waziri wa Mipango pamoja na Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anazoendelea kufanya kwenye Taifa letu. Tumejiridhisha na kuona namna ambavyo Mheshimiwa Rais anavyoendelea kufanya kazi kubwa katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili na Waheshimiwa Naibu Mawaziri kwa kazi kubwa wanazofanya na kwa bajeti ambazo wameleta hapa nzuri na ambazo zinaleta taswira kwa nchi yetu katika mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo matatu ambayo nataka nichangie. Jambo la kwanza ni kukubaliana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kurudisha wharfage kukusanywa na TPA. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuliona hili. Suala hili lilichangiwa sana katika Wizara ya Uchukuzi, kwa kweli linaenda kuleta tija. Kama bandari watafanya ukarabati inavyotakiwa kwa kupitia fedha hizi za wharfage, zitaenda kusaidia sana katika suala zima la ukusanyaji wa kodi zitokanazo na bandari kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024, TRA ilikusanya kodi zitokanazo na bandari kwa maana ya kodi za forodha kiasi cha shilingi trilioni tisa. Tuna imani kwamba sasa zinaenda kuongezeka kwa sababu miundombinu ya bandari itaenda kuimarika. Napongeza sana kwa hatua hii, ni hatua njema ambayo inaleta taswira ya makusanyo mazuri katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili ambalo nataka kuchangia ni eneo hili ambalo limelizungumzia matumizi ya mfumo wa malipo kidigitali. Mfumo huu ni mzuri sana. Mfumo wa TIPS ambao umetengenezwa na watu wetu wa BoT ni mfumo ambao utatusaidia sana nchi yetu katika ukusanyaji wa mapato ya TRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nieleze kidogo nini faida ya mfumo huu? Mfumo huu utaenda kutusaidia hasa katika kujua miamala ya kibiashara iliyofanyika kwa mfanyabiashara, pia inaenda kuleta uwazi mkubwa wa miamala yote inayofanyika kwa wafanyabiashara na watumiaji wa mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme jambo moja ambalo sasa inatakiwa tujielekeze kwa matumizi ya mfumo huu ili kupunguza matumizi ya malipo kwa kutumia cash. Nchi zilizoendelea ni zile ambazo nimeondokana na mfumo wa kulipa kwa kutumia cash, kwa sababu mfumo huu kwa kulipa kwa kutumia cash una mambo mengi hasa katika ukwepaji wa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi wanakwepa kodi kwa kutumia mufumo huu wa malipo kwa kutumia cash kwa sababu mtu anapewa cash, harekodi popote biashara imemalizika, amepata chake, hamna sehemu alipolipa; lakini kwa mfumo huu ambao Mheshimiwa Waziri amekuja nao wa kupunguza malipo yoyoye kwa kutumia cash, kwa kweli itaenda kusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasemekana kwa takwimu kwamba kwa sasa hivi malipo kwa kutumia mfumo huu ni 20% tu malipo yanayofanyika. Bado tuna safari ndefu, naomba sana Mheshimiwa Waziri asimamie hili, tuwasaidie wafanyabiashara kupata mashine za PoS kwa ajili ya malipo ya kutumia mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri wafanyabiashara wajiunge na mfumo huu ili kusudi waweze kusaidiwa na kufanya malipo yatokanayo na mfumo huu yaende vizuri. Mfumo huu unaweza ku-discourage watumiaji kama hatutaweka misingi mizuri ya makato ya miamala. Mfano, nikupe jambo moja hapa na ungenisikiliza ingekuwa vizuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikupe mfano wa jambo moja hapa. Ukitoa fedha kutoka kwenye mabenki, kwa benki zetu za kibiashara ukatoa kuja kuleta kwenye mtandao wa simu, mfano M-PESA kiasi cha shilingi 100,000 ukileta kwenye mtandao wa simu, kwa maana ya laini, benki inakukata shilingi 6,000 kwa shilingi 100,000 lakini ukienda kulipa kwa mfanyabiashara kwa matumizi ya manunuzi ya bidhaa kwa kutumia Lipa Namba kwa kiasi cha shilingi 100,000 utakatwa shilingi 2,000. Unaiona laki moja umekatwa shilingi 8,000. Sasa kwa wananchi wetu wa kawaida, shilingi 8,000 ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza wananchi wa Busega leo kwenda kufanya transaction ya shilingi 100,000 kwa kununua bidhaa alipe shilingi 8,000 hatakubali. Ataona ni bora achukue bodaboda alipe shilingi 1,000 akachukue Shilingi 100,000 kwenye ATM halafu akaenda akafanya manunuzi. Hapo tutakuwa bado hatujasaidia nchi katika suala zima la kutumia mfumo huu. Ili mfumo huu utumike vizuri, anza kwanza na haya matatizo ambayo yanaweza kuwasababisha wananchi kuwa demoralized kwenye suala zima la kutumia mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekupa mfano hapa wa shilingi 100,000 namna inavyokatwa kwenda kwa mlaji wa mwisho huyu uliyemlipa kwa kutumia Lipa Namba, kama angekatwa makato ya kawaida mfano Shilingi 100,000 nikitoa hapa kuja kwangu kwenye M-PESA wakakata shilingi 2,000 badala ya shilingi 6,000 mimi inani-encourage kutumia mitandao ya simu kufanya manunuzi lakini kama tukifanya hivyo maana yake haya manunuzi ambayo tunasema tunaenda kununua kwa cash kodi yake haitafahamika.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa

MWENYEKITI: Mheshimiwa Simon kuna taarifa.

TAARIFA

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana kwa asilimia mia moja na anachokizungumza Mheshimiwa Simon.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni incentives tu zinaweza zikaisaidia Serikali kutoka kwenye huu mfumo wa kutumia cash kwenda kwenye cashless. Hata kwenye EFD Mheshimiwa Waziri tungeshauri shusheni VAT kwa mtu ambaye analipa kwa cashless economy kwa maana kwa mfumo kuliko mtu anayelipa kwa cash hii itasaidia Watanzania wengi kushawishika kutumia fedha au kulipa fedha kupitia kwenye mfumo na hatimaye Serikali ikaiona fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shusheni VAT angalau mfikishe kutoka 18% kwenda 16% ili iweze kusaidia Watanzania wengi. Ahsante.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Simon unapokea taarifa ya Mheshimiwa Festo Sanga?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea taarifa kutoka kwa mtu bingwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini maana yake, mfano sasa hivi nikitoka hapa niende ATM nikachukue shilingi 100,000 wanakata shilingi 2,000, lakini nikitoa shilingi 100,000 hiyo hiyo kuja kwenye M-PESA nakatwa shilingi 6,000. Huoni hili ni tatizo kubwa. Sasa tutamshawishi vipi Mtanzania atumie miamala kupitia simu badala ya kutumia cash?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukikata kumsaidia Mtanzania ni lazima kwanza tuanze na benki za kibiashara waweze kupata faida kidogo ambazo amezungumzia incentives zile ili tuweze kwenda kwenye mfumo. Huu mfumo unasaidia eneo lipi? Hata wale ambao tunapiga kelele wanakwepa kutoa EFD, mfumo utamwonesha kwamba wewe mfumo unasema sales zako ni shilingi bilioni 200, mbona EFD zinaonyesha shilingi bilioni 100? Hukutoa risiti huku kwa sababu mfumo hauwezi kudanganya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tulione hili tuweze kuwasaidia Watanzania na tuisaidie nchi. Tunapoteza kodi na walipakodi wameshajua muda mwingine mnaziangalia account zao. Kwa hiyo, kuna wafanyabiashara wengine wanakuwa na account ya kampuni na account ya personal zote zinapokea fedha za biashara. Akikusanya pale amekusanya shilingi milioni 200, shilingi milioni 100 anapeleka kwenye kampuni; shilingi milioni 100 anapeleka kwenye account yake ya kawaida ili mkienda kuangalia account mjue mauzo yake hamtayapata yote, lakini tukitumia mfumo ambao huu umekuja nao wa TIPS ni mfumo mzuri, nauunga mkono, lakini lazima tuone vitu ambavyo vinaweza kuleta changamoto ikiwepo na gharama za miamala kama nilivyosema na kama alivyosema rafiki yangu Mheshimiwa Sanga hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, barabara ya kutoka Mwanza – Tarime kipange ya kutoa Nyanguge kwenda Lamadi, hiki kipande ni kibovu, ni kibovu sijawahi kuona. Barabara hii ni barabara ya kiuchumi, ni barabara ya kimkakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani atakavyokuja kuzungumza wakati wa bajeti yake, aseme hili, lakini tunatamani kuona barabara inatengenezwa, tunatamani kuona barabara hii inakarabatiwa kwa sababu ni barabara kuu. Tunaomba aitembelee barabara hii ili aweze kuona namna ilivyoharibika kutoka pale Nyanguge kuelekea Lamadi Jimboni kwangu tuweze kuitengeneza iweze kuleta uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Rais, tumetengeneza Daraja la Msisi, sasa ili litumike vizuri ni lazima barabara nyingine na zenyewe ziwe na ushirikiano. Kama barabara hizi hazina ushirikiano, sasa mizigo kutoka kule Tarime tunapitisha wapi kwenda Geita? Barabara hizi lazima ziwe na ushirikiano ili ziwe na matokeo chanya kwa Watanzania na tuweze kujenga uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimeona kwenye bajeti yako ukurasa wa 20, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amewapa MSD mtaji wa shilingi bilioni 100 kitu ambacho ni kizuri. Nilitamani atuambie atakapokuja hapa aseme, hizi fedha shilingi bilioni 100 alizowapa MSD ni sehemu ya deni wanalodai? Kwa sababu MSD ukisoma taarifa zao za fedha wanamdai shilingi bilioni 260. Sasa huu mtaji aliowapa, ni nje ya deni? Kama amewapa kama mtaji nitashangaa kwa sababu it was very simple. Awalipe tu deni lao shilingi bilioni 260, achane nao, basi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Mheshimiwa Waziri alitazame vizuri hapa. Kama amewapa mtaji wa shilingi bilioni 100, it is better offset kwenye deni shilingi bilioni 260, wabakiwe na deni la shilingi bilioni 160, wamalizane. Hakuna sababu za kuendelea kusema tumewapa shilingi bilioni 100 kama mtaji halafu wao huku kwenye vitabu vyao wanaendelea kudai shilingi bilioni 260. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri Serikali ichukue shilingi bilioni 260 isiwe na madeni makubwa, amalizane nao. Awape fedha zao zile shilingi bilioni 100, wakubaliane kwamba bado shilingi bilioni 160 wanawadai wamalizane ili vitabu vya Serikali, vitabu vya MSD visomane na kuleta tija na kutokuwa na madeni makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakuja hapa tunazungumzia madeni, madeni, ili tuweze kufanya vizuri zaidi, nilikuwa nafikiri Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu, basi nitashawishika aniambie hizi fedha shilingi bilioni 100 na hili deni la Shilingi bilioni 260 zimekaaje? Kama aliwapa mtaji, pia atupe mkakati ni kwa namna gani hili deni la shilingi bilioni la 260 ambalo zinadaiwa na MSD anaenda kulilipa ili wananchi wetu waendelee kupata huduma, kwa sababu fedha hizi ukienda MSD wanakwambia tunaidai Serikali, bado haijatulipa na mwisho wa siku dawa zinakosekana kwenye taasisi zetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Simon, muda umeisha.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Mheshimiwa Waziri umefanya mambo mazuri kwenye bajeti, haya ambayo nimeyazungumza natamani siku ya kuhitimisha utupe majibu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)