Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MISSION 300 ULIOFANYIKA DAR ES SALAAM TAREHE 27 - 28 JANUARI, 2025 NA KUHUDHURIWA NA WAKUU WA NCHI 21 ZA AFRIKA

Hon. Shamsi Vuai Nahodha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MISSION 300 ULIOFANYIKA DAR ES SALAAM TAREHE 27 - 28 JANUARI, 2025 NA KUHUDHURIWA NA WAKUU WA NCHI 21 ZA AFRIKA

MHE. SHAMSI VUAI NAHODHA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na kwa unyenyekevu mkubwa naomba kusimama mbele yenu kwa minajili ya kutoa mchango wangu kuhusu Azimio la Kumuunga Mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufanikisha Mkutano huu Mkuu kwa kuzungumzia masuala ya nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze maelezo yangu kwa kunukuu maneno mazuri sana ya msomi mmoja na mwandishi wa vitabu mwenye ulemavu wa macho ambaye anaitwa Helen Keller. Aliulizwa na Waandishi wa Habari, ni jambo gani linamsikitisha sana hapa duniani? Alisema anasikitishwa anapowaona watu wenye macho kamili, lakini hawana ndoto katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ndoto zake za kuwakutanisha viongozi wenzake wapatao 21 kutoka maeneo mbalimbali ya Bara la Afrika ili kuzungumzia mustakabali wa nishati hasa katika maeneo ya vijiji Kusini mwa Jangwa la Sahara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtakumbuka kwamba nchi yetu kwa miaka mingi sana imekuwa ikitegemewa kutoa mwongozo katika masuala ya kisiasa, maendeleo na uchumi katika Bara la Afrika. Tulifanya hivyo kwa ukombozi wa Kusini mwa Afrika, tukafanya hivyo katika kutetea utamaduni wa Afrika na sasa nashukuru kwamba Mheshimiwa Rais Dkt. Samia anauendeleza utamaduni huo wa kutetea masuala ya msingi ya mahitaji ya binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, namshukuru kwa kuturudisha huko. Tunapokuwa na mambo ya msingi, tunapokuwa na matatizo ya msingi ndani na nje ya Bara la Afrika, sauti ya Tanzania, msimamo wa Tanzania umekuwa ukihitajika sana katika kuwapa faraja hasa wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaambiwa kuna watu wapatao zaidi ya milioni 300 katika Bara la Afrika, hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wanahitaji nishati, lakini kwa bahati mbaya sana hawana nishati hiyo muhimu. Matokeo yake ni nini? Wapo Waafrika wenzetu wamepoteza maisha kutokana na matumizi mabaya ya nishati hiyo. Kwa msingi huo, basi tuna kila sababu ya kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu kwa kutoa ukombozi kwa watu hawa niliowataja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bara la Afrika lina vyanzo vingi sana vya nishati, kama vile upepo, jua, mawimbi ya bahari, gesi asilia, lakini bado matumizi ya nishati salama katika Bara la Afrika yako chini sana. Kwa msingi huo, naviomba vyuo vikuu vya Tanzania viendeleze mafunzo na utafiti wa teknolojia ya matumizi ya nishati ya upepo, maji ya bahari, gesi asilia, biogas na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naviomba vyuo vikuu vya Tanzania vitengeneze majiko sanifu ili tupunguze uagizaji wa majiko haya kutoka nje. Mwalimu alitufundisha kujenga Taifa linalojitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo basi, ninayo kila sababu ya kuunga mkono hoja na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)