Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, pia nami nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa maoni yangu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa mwenyeji wa Mkutano huu wa Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nitumnie nafasi hii kuieleza dunia juu ya umahiri mkubwa aliyonao Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan hasa katika masuala yote ya kidplomasia.
Mheshimiwa Spika, tutakubaliana tu wote kwamba halikuwa jambo rahisi kuweza kushawishi dunia nzima, kuweza kukubali kwamba Tanzania inaweza kuwa Mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Nishati wa Afrika. Ninasema hivyo kwa sababu Mkutano huo ulijumuisha wakuu wa nchi zaidi ya 20, lakini wako wakuu wa taasisi za kimataifa mbalimbali duniani zilikuja hapa Tanzania. Hiyo ni kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais wetu ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inaonesha kwamba Rais wetu mbali na mambo mengi ambayo amefanya katika nchi yetu, ameweka historia nyingine ya kuwa Rais mahiri, Rais mpambanaji, nasi kama Watanzania tuna sababu ya kuendelea kumuunga mkono Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mkutano huu umefanikiwa katika kipindi ambacho jamii nyingi sana za Afrika zilikuwa na maono hasi juu ya uongozi unaomhusu mwanamke. Walikuwa hawaamini kwamba mwanamke anaweza akafanya mambo makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amebomoa hizo kuta na ametuma salamu duniani ili dunia ijue kwamba suala la uongozi halihusiani na suala la jinsia, bali uongozi unahusiana na suala la uwezo alionao mtu. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala kama hili, fursa ya mkutano mkubwa kama huu, ni fursa ambayo nchi nyingi huwa zinatamani kwamba jambo hili lifanyike kwenye nchi yake. Kwa hiyo, sisi kama Tanzania, na kama Afrika ziko faida mbalimbali ambazo kama nchi tumezipata. Kutokana na muda, nitataja chache.
Mheshimiwa Spika, faida mojawapo, tumeweza kukuza fursa za kiuchumi na wafanyabiashara wamenufaika. Faida ya pili ni kwamba, tunafahamu Rais wetu ndiye champion mkubwa wa masuala ya utalii ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, tumetumia mkutano huu kuweza kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii. Pia, tunafahamu wafanyabiashara wamepata network na connection mbalimbali kwa ajili ya biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, faida nyingine kubwa ambazo ni za muhimu sana, tunafahamu katika Mkutano huo Rais wa World Bank ametoa pongezi kwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan na ameitaja Tanzania kuwa ndiyo kinara wa mapinduzi ya nishati vijijini. Pia, hilo limefanikiwa kutokana na kazi kubwa ambayo Mheshimiwa Rais ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii tumeona katika nchi yetu, tunayo mikoa mingi ambayo ilikuwa bado haijaingizwa kwenye gridi ya Taifa. Tunavyoongea hivi sasa Mkoa wa Kigoma umeingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Tunavyoongea hivi sasa, Mkoa wetu wa Songwe ambao kwa miaka mingi tulikuwa tuna tatizo la kukatikakatika kwa umeme, sasa hivi Mkoa wa Songwe umeingizwa kwenye gridi ya Taifa. Pia, tunavyoongea sasa hivi, tumeweza kufikisha umeme kwenye vijiji vyote ndani ya Tanzania. Sasa tunakwenda kuingia kwenye awamu nyingine ya pili ya kusambaza umeme katika vitongoji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kazi hii ni kubwa na ndiyo maana Rais wa World Bank akasema kwamba nchi nyingine za Afrika zina kila sababu ya kuiga kwa Tanzania. Hongera sana Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunafahamu kwa muda wa miaka mingi tulikuwa tunatamani kwanza tuwe na umeme ambao utatutosheleza sisi kama nchi. Pia, tulikuwa tunatamani tuwe na umeme ambao tutaweza kuuza katika nchi nyingine. Hata hivyo, kwa kasi hii ambayo Mheshimiwa Rais anayokwenda nayo na kwa mageuzi haya makubwa katika nishati ya umeme, ni wazi kwamba siku siyo nyingi tunakwenda kuanza kuuza umeme katika nchi nyingine za Afrika ikiwepo nchi ya Zambia, Comoro na Mozambique.
Mheshimiwa Spika, vilevile, sisi kama nchi ya Tanzania muda siyo mrefu tunakwenda kujitosheleza kwa umeme na ndiyo maana Mheshimiwa Rais amesema kwamba, ana ujasiri kwamba sasa vitongoji vyote ndani ya nchi yetu vinakwenda kupata umeme. Hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mengi mazuri ambayo Mheshimiwa Rais ameyafanya, tunaona kwamba muda hautoshi, sisi kama Chama cha Mapinduzi kutokana na kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifanya, ndiyo maana sisi kama Wajumbe kupitia Mkutano Mkuu tulisema kwamba hatuna dakika za kupoteza zaidi ya kupitisha jina moja la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili aweze kwenda kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Urais katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulifanya hivyo siyo kwamba yale yalikuwa ni maoni yetu Wajumbe wa Mkutano Mkuu, hapana. Sisi tulikuwa ni wawakilishi wa Wana-CCM wengi ambao tumewaacha katika mikoa yetu. Katika kuthibitisha hilo ndiyo maana umeona baada ya lile Azimio la Mkutano Mkuu, tumeona makundi makubwa ya Wana-CCM na makundi makubwa ya wananchi katika mikoa yetu wakiendelea kuunga mkono Azimio la Mkutano Mkuu na kusema kwamba Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatosha, tuweze kumpa mitano tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi na tunafahamu kwamba nchi yetu Mheshimiwa Rais Samia ameitoa mbali sana na kwa hapa alipofika ni wazi kwamba, wapinzani wana kazi ya kufanya katika uchaguzi wa mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika, wengine walitamani kwamba mambo mengi yasifanyike, lakini mambo mengi yamefanyika, walitamani Bwawa la Mwalimu Nyerere lisikamilike, lakini limekamilika; walitamani umeme usipelekwe vijijini, umepelekwa vijijini na sasa tunakwenda kupeleka umeme kwenye vitongoji; Walitamani kuona kwamba, wanawake wakiendelea kutumia nishati ambazo zinahatarisha afya zao (kuni), lakini Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshasema kwamba ifikapo mwaka 2035 wanawake wote watakuwa wanatumia nishati ambayo ni safi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kama Wabunge tunapenda tuchukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na tunasema kwamba Rais wetu anatosha kuweza kutuongoza katika miaka mitano inayofuata, ahsante sana. (Makofi)