Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuunga mkono hoja ya kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa ambayo ameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini tunampongeza? Tunampongeza kwa sababu kwanza katika historia ya Tanzania, mkutano wa aina hii na mkubwa katika eneo la nishati haujawahi kutokea toka tupate Uhuru. Haijawahi! Kama tumewahi kupata mkutano mkubwa kama huu ni kwenye maeneo mengine, lakini kwenye upande wa nishati ni mkutano wa kwanza katika historia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu kwanza siyo tu anapongezwa, anapongezwa kutokana na kazi ambazo amezifanya, zimeonekana na zimeleta matunda. Katika ujenzi wa Bwawa la Nyerere watu wengi waliamini kwamba lile bwawa halitaweza kukamilika, lakini amelisimamia mpaka limekamilika na sasa hivi Tanzania inasifika kuwa na umeme mwingi ambao hatuna hata mahali pa kuupeleka na sasa tunauuza nchi za nje. Hii ni kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ameonesha maono makubwa, uzalendo, uadilifu, umahiri na kusimamia masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa katika nchi yetu. Kwa namna alivyofanya kazi, ndiyo maana tunayo kila sababu ya kusimama na kumpongeza na kumtia moyo ili aendelee katika kuleta maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya kuandaa mkutano huu, ni mkutano mkubwa wa watu wengi zaidi ya 2,600 kwenye mkutano, wakuu wa nchi zaidi ya 21 kuja kwenye nchi yetu; maana yake nini? Maana yake tumepata fedha nyingi za kigeni, tumepata uchumi mzuri, lakini zaidi ya hapo, unatokana na msimamo wake wa kusimamia nishati safi kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika ajenda ambazo amekuwa akizisimamia na ambazo tumeona Tanzania toka miaka nenda rudi, ilikuwa inasimamia ajenda mbalimbali na tunafanikiwa. Hii ndiyo ishara kwamba Tanzania ina viongozi wakubwa, waadilifu, wenye maono na wanaotakiwa kuheshimika katika dunia hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, leo hii katika hili lililofanyika ni ishara kwamba tunaweza tukawa champion wa kuiunganisha Afrika yote tukawa kitu kimoja. Tukiunganisha Afrika na jinsi ambavyo Mheshimiwa Rais amesimamia nishati safi, maana yake nini? Maana yake itatusaidia kupunguza umaskini wa Watanzania. Kwa sababu umeme ukipatikana na nishati safi ikipatikana kila mahali, umaskini wa Tanzania utapungua, pia uchumi wa nchi za Afrika utapungua, na zaidi ya hapo ajira mbalimbali zitakuwa zimetengenezwa. Kikubwa zaidi, amelinda afya za akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, afya za akina mama zitalindwa vizuri sana, ndiyo maana ameendelea na hiyo kwamba tulinde afya kwa kutumia nishati safi kwa kila mmoja. Kwa kufanya hivyo, tuna kila sababu ya kumpongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, amesimamia ujenzi wa SGR ambayo imeleta mabadiliko makubwa sana. Tulikuwa tunaona magari yote yalikuwa yanatumia mafuta ya kigeni, mitambo mingi ilikuwa inatumia hiyo, SGR sasa inatumia umeme unaozalishwa hapa hapa nchini na sasa ni mabadiliko makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukienda tena tukaanza kutumia nishati kwenye kupikia na kila mahali, maana yake fedha za kigeni zitakuwa zimepona na tutazielekeza katika maeneo mengine. Kwa hiyo, hiyo ni kazi kubwa ambayo ameileta na mabadiliko makubwa katika usafirishaji hapa nchini na kuleta maendeleo kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina imani kwa kazi hii, kwa uzalendo huu, kwa uadilifu huu na mambo ambayo anaendelea kuyasimamia, ndiyo maana sisi Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi tulipokutana Dodoma, tukasema huyu huyu anatosha tena atuongoze kwa miaka mingine mitano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nawaomba Watanzania, wananchi na Wabunge wenzangu, tumuunge mkono ili maendeleo makubwa ya nchi hii yapatikane na vijana wa nchi hii wapate ajira kutokana na ajenda hizi kubwa ambazo zimetokana na kufanikiwa kwa mkutano huu ambao umeandaliwa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Naibu wake na Baraza zima kwa kazi kubwa mliyoifanya katika kufanikisha mkutano huu. Tuendelee kumuunga mkono ili tuweze kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)