Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nami nakushukuru sana kwa kupata fursa hii adhimu ya kuchangia katika azimio hili muhimu sana la kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa ku-host mkutano mkubwa sana wa kidunia katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuileta Afrika na dunia nchini Tanzania. Tumesikia hapa kwamba Mkutano huu umehudhuriwa na Wakuu wa Nchi zaidi ya 20, lakini umehudhuriwa na Wajumbe zaidi ya 2,000 kutoka duniani kote. Dunia ilikuwa hapa katika siku hizi mbili na nilifuatilia. Tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu, Mawaziri wote na Naibu Mawaziri, lakini na Wizara ya Nishati kwa kuratibu vizuri mkutano huu. Wageni wetu wamekuja na wameuona ukarimu wa Kitanzania. Yale ambayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyaonesha kwenye Royal Tour, wameyaona na nina uhakika wamerudi kwenda kuyasema mazuri ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika maazimio haya au Azimio la Dar es Salaam, mambo makuu matatu yamewekwa. La kwanza, kuhakikisha kwamba kufikia mwaka 2030 Waafrika milioni 300 watapata access ya uhakika ya umeme; la pili, ni kuhakikisha umeme huu unapatikana kwa gharamna ndogo; na la tatu, ni kuhakikisha Afrika inakuwa kinara wa matumizi ya nishati safi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maazimio haya yanakwenda kumgusa moja kwa moja Mtanzania wa chini. Mkutano huu umekuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu, tunapozungumzia mapinduzi katika Sekta ya Nishati, tunazungumzia mapinduzi ya viwanda, tunazungumzia uwekezaji mkubwa ndani ya nchi yetu, tunazungumzia mapinduzi makubwa katika uzalishaji wa chakula, tunazungumzia maendeleo vijijini, tunazungumzia maendeleo ya miundombinu, tunazungumzia mapinduzi ya biashara za kimtandao na mapinduzi ya elimu ya kimtandao, tunamzungumzia Mtanzania wa kawaida, na tunazungumzia kwa ukubwa zaidi suala la ajira kwa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, amezungumza vizuri sana kaka yangu Mheshimiwa Kingu, kwamba Bara la Afrika ndilo bara changa kuliko yote katika dunia hii sasa hivi. Kwa vile watu wengi zaidi ndani ya Afrika ni vijana, ninukuu, World Bank Group imesema kwamba, “maazimio haya yatakuwa ndiyo cornerstone ya kuanza kutatua tatizo la ajira kwa kundi kubwa na linaloongezeka la vijana Afrika.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukizungumzia mapinduzi ya viwanda, hakuna nchi duniani iliyoendelea pasipokuwa na maendeleo makubwa kwenye viwanda na hakutakuwa na viwanda bila kuwa na nishati ya kueleweka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza sasa, wakati Mheshimiwa Dkt. Adesina anafunga au anatoa wasilisho lake la mwisho alisema; “Ajenda hii siyo mpya katika Bara la Afrika, imekuwa inajadiliwa mara nyingi, lakini utendaji wake umekuwa mdogo. Sasa maazimio haya ya Dar es Salaam yawe ndiyo mwanzo wa utendaji wa uhakika wa utekelezaji wa ajenda hii.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa wakati wengine wanafikiria kuanza kutenda, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alishaanza kutenda, ameshatenda na anaendelea kutenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, duniani kote, nchi zote zilizoendelea zina mchango mkubwa wa viongozi wenye maono ya kesho na unavyozungumza, wakati wengine wanawaza kuanza kutembea au kuanza kufikiri, Mheshimiwa Dkt. Samia ana mawazo ya kesho na alikwishafikiri.
Mheshimiwa Spika, tunavyozungumza hivi sasa, Bwawa la Mwalimu Nyerere liko 98%, kumekuwa na kongamano la kuanza kutumia umeme wa jotoardhi ambalo lilifanyika mwaka 2024 mwezi Oktoba na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akatoa commitment kwamba mwaka huu wa 2025 umeme wa jotoardhi utaanza kutumika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapozungumza sasa hivi, mikataba mingi sana ya kuanza kutumia gesi asilia imesainiwa. Wakati watu wanazungumzia ajenda ya kuanza kutoa nishati yenye gharama nafuu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa ruzuku kwenye gesi au nishati safi, 20% kwa walioko Dar es Salaam na 50% kwa mikoa yote. Kwa maana ya kwamba, mama aliyekuwa nyumbani, ambaye alikuwa anakwenda kujaza mtungi wa gesi kwa shilingi 20,000 mpaka 25,000, sasa hivi anakwenda kujaza kwa 10,000 mpaka shilingi 12,000. Nani kama Mheshimiwa Dkt. Samia? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunavyozungumza sasa hivi, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa mitungi ya gesi zaidi ya 420,000 kwenda kwa akina mama ku-champion ajenda hii ya nishati safi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunavyozungumza sasa hivi kuna Mradi wa Liganga na Mchuchuma. Mfupa uliokuwa umeshamshinda fisi, leo hii Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameuweka vizuri, wananchi wamelipwa fidia na mkataba ule mtauona hapa Bungeni na mambo yamekwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, amezungumza vizuri Mheshimiwa Hasunga, leo hii hapa ni kama ndoto. Tuna treni ya umeme inayotumia umeme wetu wenyewe na hapa tunapozungumza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa commitment kwamba nchi yetu itahakikisha inaunganisha nchi zote za jirani katika gridi yetu ya Taifa ili tuanze kuwauzia umeme. Nchi yetu imepiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati wengine wanawaza kuanza, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshaitangazia dunia kwamba Tanzania inakuja, they better watch out. Tunampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi niseme, Kitabu cha Luka Sura ya 19:40 inasema; “Wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.” Sisi tumeamua kusema, tunasema kwa sababu tuna kila sababu ya kusema, lakini tutahakikisha kwamba sisi vijana wake Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan tuko nyuma yake kumuunga mkono, lakini kubwa zaidi mcheza kwao hutunzwa.
Mheshimiwa Spika, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi wametuonesha, lakini yale yalikuwa ni maono ya Wana-CCM wote zaidi ya milioni 12 katika nchi hii kwamba bado tuna imani kwamba nchi yetu chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iko katika mikono salama, kesho yetu ni bora. Tunaamini kwamba mapinduzi makubwa yatakayofanyika katika nchi hii mpaka ifikapo mwaka 2030 itakuwa mbali sana katika uchumi wa Afrika na dunia kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)