Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kwanza nami nitangulie kwa kushukuru kupata fursa hii, lakini niseme tu kwa heshima na furaha kubwa, nimesimama leo nikiungana na Rais wa Benki ya Dunia Bwana Ajay Banga, pamoja na Rais wa Benki ya Afrika Dkt. Adesina, wadau wote wa Sekta ya Nishati pamoja na wananchi wote wa Tanzania, kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa aliyonayo katika Sekta ya Nishati, Diplomasia na Uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba, siyo mara ya kwanza Wakuu wa Nchi kuja kwenye Taifa letu. Tunayo rekodi. Ukiangalia mwaka 1999 wakati wa msiba wa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere, walikuja Wakuu wa Mataifa 19. Siyo hivyo tu, tukiangalia mwaka 2019 kwenye Mkutano wa SADC walikuja Wakuu wa Mataifa 15. Hii ya sasa imevunja rekodi kwa kupokea Viongozi Wakuu wa Mataifa 35. Hiyo idadi iliyotajwa pale 21 hao ni Marais, lakini kuna Makamu wa Marais, Mawaziri Wakuu, Naibu Mawaziri Wakuu ambayo inaleta idadi ya karibu 35. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba mkutano huu umefanyika kwa kuzingatia mambo mengi sana. Haiwezekani mkutano huu ukafanyika, haya mambo hayatokei tu. Tunajua kazi kubwa iliyofanyika kwenye kuimarisha diplomasia ya Taifa hili. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa mstari wa mbele kuimarisha diplomasia.
Mheshimiwa Spika, tuna rekodi, amekuwa akialikwa kwenye mikutano mikubwa ambayo inajadili masuala mazima ya kiuchumi na mahusiano na Mataifa mengine. Mfano tu Novemba, 2024 amehudhuria Mkutano wa Mataifa Tajiri 20 (G.20). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameshiriki Mkutano unaoitwa FOCAC. Mkutano huu yeye ndio aliyeteuliwa kuwa Msemaji wa Bara la Afrika. Fikiria Afrika ina Marais wangapi? Ina Marais wangapi? Lakini Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akateuliwa kuwa Msemaji wa Marais wote katika Bara la Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya mambo hayatokei hivi hivi jamani. Ni hivi, niseme nisiseme? Niseme nisiseme? (Makofi)
WABUNGE FULANI: Semaaa!
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ni hivi, kwa haya yanayofanyika na kwa hiki kilichofanyika, Mkutano Mkuu na mengine yote, haya mambo yamehalalisha maamuzi ya Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi yaliyofanyika mwaka huu na mimi naungana kwa 100% na maamuzi waliyofanya Wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limesababisha mataifa haya kushiriki Mkutano huu bila kuwa na tatizo lolote ni suala la amani na utulivu katika Taifa hili. Nitumie fursa hii kuvipongeza sana vyombo vya ulinzi na usalama wa Taifa hili. Ninavyofahamu, hakuna nchi yoyote inayoweza kuleta kiongozi wake wa kitaifa bila vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuhakikisha anakokwenda ni salama kiasi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa tafsiri hii ni kwamba vyombo hivi vimejihakikishia kwamba nchi ya Tanzania ni nchi ya amani. Nami naomba kupitia Bunge lako Tukufu, Jeshi la Ulinzi na Usalama kwenye suala la amani wasi-compromise na mtu yeyote. Tunawaona wenzetu wa Mataifa mengine wanavyoteseka, tunawaona wamama, watoto na wazee wanavyoangamia. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, jambo hili lisingefanyika kama ukuaji wa uchumi wa Taifa letu ungekuwa unasuasua, lakini watu hawa watakuwa walijihakikishia kwamba mpaka kufika hapa ni lazima kuna facilities za kutosha. Huwezi kuita Mataifa mengine yakaja kwenye nchi yako ukiwa una umeme wa kusuasua. Huwezi kuita Wakuu wa Mataifa mengine ukiwa unajua huna usafiri wa uhakika na ninyi ni mashuhuda, tuna ndege za kutosha na airport ya kisasa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukizungumzia umeme, ndiyo usiseme. Leo tunazungumzia nchi yetu ina Megawati 3,404. Ukiangalia wakati tunapata Uhuru tulikuwa tuna Megawati 21 peke yake. Mama Samia amechukua nchi hii ikiwa ina Megawati 2,100. Sasa kuna ongezeko la Megawati 1,300 zilizoletwa na mama huyu. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, mafanikio ya mkutano huu ni makubwa sana. Najua kwa sababu ya muda na wenzangu wameshayasema, sitaki kuyarudia, lakini kwa kifupi tumeona kwamba kufika mwaka 2,030 ajenda kubwa ambayo mama alizungumza wakati wa hotuba yake, ndoto yake ni kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vilivyobaki 30,000 vipate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna jambo moja la msingi sana kwa watu wote ambao wanapenda kusoma vitu na kufanya references wanaweza wakanielewa vizuri zaidi. Mataifa yote kwa sasa Afrika na kwingineko watakapokuwa wanazungumzia masuala ya umeme watafanya reference ya Energy Summit 300; 2025 Tanzania. Nchi hii itasikika kote duniani kwenye sekta ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia, napata furaha sana nami kama mtoto wa kike, amesema vizuri sana dada yangu Mheshimiwa Shonza pale, Rais huyu ametutengenezea mazingira ambayo kila mwanamke wa nchi hii Tanzania anapata precedence ya kuamini kwamba anaweza akawa lolote katika Taifa hili. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, nami naomba nitumie jukwaa hili la Bunge kutaka kumhakikishia Mheshimiwa Rais ya kwamba wanawake wote wa Tanzania hii tunamuunga mkono, tunampenda na tunamwombea kwa Mwenyezi Mungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huwa wanasema kwamba mchawi wa mwanamke ni mwanamke mwenzie, siyo kweli. Wanawake walioko humu ndani wananielewa, uongo, kweli! Sisi tunapendana. Tutashirikiana na Rais wetu mwaka 2025 huu atashinda kwa kishindo. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Spika, tunajua 70% ya wapigakura katika Taifa hili ni wanawake. Kwa hiyo, naomba niendelee kumtia moyo Mheshimiwa Rais na naunga mkono sana Azimio hili ambalo limeletwa hapa mbele ya Bunge lako Tukufu. Nakushukuru sana. (Makofi/Vigelegele)