Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MISSION 300 ULIOFANYIKA DAR ES SALAAM TAREHE 27 - 28 JANUARI, 2025 NA KUHUDHURIWA NA WAKUU WA NCHI 21 ZA AFRIKA

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

AZIMIO LA BUNGE LA KUMPONGEZA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA MISSION 300 ULIOFANYIKA DAR ES SALAAM TAREHE 27 - 28 JANUARI, 2025 NA KUHUDHURIWA NA WAKUU WA NCHI 21 ZA AFRIKA

NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa nafasi hii, lakini nakushukuru pia kwa upendeleo. Siyo kawaida mchangiaji wa kawaida kuja kusemea hapa. Nakushukuru sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nami vilevile nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa neema na uzima wa kukutana hapa leo, na kwa kweli nimshukuru sana na kumpongeza sana mtoa hoja ambaye ameleta hoja hii ya pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa sababu ya Mkutano huu ambao umefanyika hapa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, ni Mkutano ambao ulikuwa ni mkubwa sana na kwa kweli kila mahali na kila sehemu ambapo wakati tunafanya kazi ya kufanya maandalizi, tulikuwa tunaona mazingira ambayo yatakuwa magumu. Moja, watu waliotaka kushiriki kwenye ule mkutano, idadi yao ilikuwa kubwa sana, matokeo yake tumeshindwa hata tu kulaza watu Dar es Salaam, ikabidi wengine wanatokea Zanzibar kuja kwenye mkutano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka kuwa delegation ya Tanzania peke yake, ambaye ndiye mwenyeji, tulikuwa tumepanga kuwa na watu 497 wakiwemo na Waheshimiwa Wabunge na baadhi ya viongozi, lakini kutokana na mwitikio mkubwa ilishuka kutoka 497 hadi watu 90. Benki ya Dunia ilikuwa imeleta watu karibu 120, ilishuka mpaka watu 26 walioweza kupata nafasi. AfDB walikuwa na watu zaidi ya 180 na wao ilishuka mpaka watu 47 ambao tungeweza kuwaweka ukumbini na Rockefeller waliweza kupata nafasi tano tu.

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi ni kwamba mkutano ulipata mwitikio mkubwa sana na kwa sababu hiyo, ninawashukuru sana na ninakushukuru wewe kwa kuwa na jambo hili.

Mheshimiwa Spika, Bunge hili ni Bunge ambalo kazi zake kubwa mbili ni kuishauri na kuisimamia Serikali na wakati wote limekuwa likizifanya hizo kazi kwa bidii kubwa. Naomba niwaambie Watanzania kuwa, kama kuna mahali ambapo shida na matatizo ya wananchi yanazungumzwa wakati wote ni kwenye nyumba hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili Bunge ukifanya jambo baya watakwambia, na vilevile ukifanya jambo zuri watakwambia. Leo ni kielelezo kuwa Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana na nzuri na ndiyo maana umeona Bunge na wote waliozungumza toka wa mwanzo (mtoa hoja) mpaka wa mwisho aliyemalizia, utaona walikuwa wanazungumza mambo mazuri, kwa ushahidi wa mambo ambayo yanaonekana, wala hayahitaji kupigiwa ramli. Unayaona moja kwa moja yametokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwani Energy Summit ilikuwa ni nini? Ni kitu gani kilichotokea? Jambo kubwa sana ambalo tumelipata ni kuwa na mipango ya kupeleka nishati kwa wananchi milioni 300 katika Bara la Afrika. Kama unavyojua, watu milioni 600 Afrika hawana umeme na kati ya yao 85% wako Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mheshimiwa Spika, sasa mpango huu ambao ulipaswa kufanyika ilipaswa apatikane mtu mmoja wa kuusimamia. Mwanzo, Tanzania wala haikufikiriwa. Nataka nieleze hapa sababu mbili tu zilizofanya mkutano huu kuja Tanzania. Sababu ya kwanza, ni kuimarika kwa diplomasia yetu na Mataifa mengine Duniani. Diplomasia hiyo haijaimarishwa na mtu mwingine, imeimarishwa na yeye mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu ya pili ni kasi kubwa ya upelekaji wa umeme kwa wananchi hasa vijijini. Benki ya Dunia walivyofanya tathmini mwaka 2024 Tanzania iliongoza na matokeo yake wakasema mahali pekee tunapoweza kupeleka mpango huu basi iwe Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, nichukue nafasi hii kuungana na Waheshimiwa Wabunge wote kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwanza kwa msukumo mkubwa alioutoa kwenye sekta ya nishati, na pili kwa mahusiano yake yeye mwenyewe binafsi aliyoyajenga na Jumuiya ya Kimataifa na watu wengine wote ambao wana utashi mwema kwa ajili ya Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya mkutano huu, kumetokea nini? Hili ni muhimu sana, watu wajue kwamba wakati ule tunapambana kutafuta fedha kwa ajili ya kusukuma miradi ya maendeleo, kuwapelekea watu umeme, kwa kweli changamoto kubwa ilikuwa ni fedha. Mkutano huu ulivyofanyika, moja, wadau wanaohusika kwa ajili ya kuweka fedha kwenye miradi ya umeme, Afrika wameongezeka, achilia mbali wale ambao tumezoea kuwasikia, Benki ya Dunia na AFDB.
Mheshimiwa Spika, leo tunavyozungumza, kumetolewa ahadi mbalimbali za watu ambao wako tayari kushirikia kwa ajili ya kupeleka fedha ili kuweza kupeleka nishati ya umeme kwa wananchi wengi zaidi hapa Barani Afrika.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano, Benki ya Dunia imeamua kutumia mpango huu ambao tunauita Energy Compact kutoa dola bilioni 22, Benki ya Maendeleo ya Afrika imeahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni 18.2; Benki ya Maendeleo ya Kiislamu imeahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni 2.7; Benki ya Maendeleo ya Asia imeahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni 1.5; Benki ya Maendeleo ya Ufaransa imeahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni moja; Mfuko wa Maendeleo wa OPEC umeahidi kutoa Dola za Kimarekani bilioni moja; na Serikali ya Ufaransa na Rais wa Ufaransa mwenyewe Macron aliomba nafasi aweze kusalimia kwenye huu mkutano na ile announcement ya pledge ya Dola za Kimarekani bilioni moja aliitoa mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi zote za Afrika zilizokuwa zimeandaa mipango hii, mwanzo zilikuwa nchi 15, lakini kulikuwa na vigezo vya kufikiwa, baada ya mchakato kuendelea zimebaki nchi 12. Nataka nikuhakikishie kwamba, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye leo Bunge lako limeamua kutoa tamko la kumpongeza, ndiyo mpango pekee ambao Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika wamesema ni mpango pekee ambao umeandaliwa vizuri na unatekelezeka.

Mheshimiwa Spika, nataka niwahakikishie kuwa sisi wasaidizi wake tutahakikisha kuwa kazi hii ya kusimamia huu mpango inafanyika kwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Spika, sasa huu mpango una jambo gani? Mtoa hoja ameeleza vizuri na ninataka tu nirudie kwa msisitizo. Mpango huu tumewekewa viashiria vitano. Kiashiria cha kwanza, ni upatikanaji wa umeme (Energy Access). Kwa sasa hali tuliyonayo access ya umeme hapa nchini ni 78.4%, miaka mitano inayokuja kwenye mpango tulisaini, tutaupeleka umeme kwa 100% kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbili, uunganishaji umeme na wateja, leo tunavyozungumza hatua tuliyonayo tumeunganisha wateja milioni 5.2. Mpango wetu ni kupeleka kwa wateja milioni 13.5. Hili nataka nilifafanue vizuri, maana mtu mwingine anaweza kusema tuko watu milioni 60, unazungumza milioni 13?

Mheshimiwa Spika, tunazungumzia wateja, kwa maana ya kwamba zile mita unazounganisha. Ukienda kwenye jeshi utakuta jeshi moja labda lina wanajeshi 2,000 lakini wanatumia mita moja. Sisi huyo tunaita ni mteja mmoja.

Mheshimiwa Spika, maana yake ni kwamba tunapeleka kwa wateja milioni 13 kwa speed ambayo kama kusingekuwa na huu mpango tungepambana tunavyoweza tusingezidi milioni 5.2 ambayo tulikuwa nayo. Kwa nishati safi ya kupikia ambako tunataka tutoke 6.9% twende 75% kwa kipindi cha miaka mitano, na mchango wa nishati jadidifu itoke 56% iliyopo twende 65%. Hili tutalifikia bila matatizo yoyote.

Mheshimiwa Spika, ninataka kutoa taarifa kwa sababu nimepata nafasi hii, kama nyongeza kwa Waheshimiwa Wabunge kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa msukumo. Lile bwawa tunalozungumzia tungeweza kuwa tumelikamilisha ifikapo mwezi Mei. Ninafurahi kusema mbele ya Bunge hili Tukufu kwamba mpaka leo asubuhi mitambo yote nane imekwisha kabidhiwa na mtambo mmoja wa tisa utakabidhiwa mwishoni mwa mwezi huu wa pili unaokuja na Mradi wa Julius Nyerere tutakuwa tumemaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ambalo ninataka nirudie tena kuwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wabunge historia itaandikwa. Ukisikia Dunia inazungumza The Dar es Salaam Declaration ni kwa sababu Mheshimiwa Rais alikubali ku-host huu mkutano.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kishoa amezungumza vizuri sana. Hii ni nyaraka ambayo watu wote na wasomi wote na kila mtu atakayekuwa anazungumza nishati Duniani na Bara la Afrika ataizungumzia. Wakuu wa nchi waliokuja; tunaweza tukazungumza wakuu wa nchi waliokuja 22, lakini ninataka niwaambie wako wakuu wa nchi ambao last minutes kwa sababu ya matatizo yaliyotokea waliahirisha lakini walituma viongozi muhimu sana na ndio maana mliona lile tamko lilisainiwa na wakuu wa nchi na wakaonesha kuwa hii ni document yetu Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza tumeingia kwenye record ya Dunia kwamba sisi tumekuwa sababu, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na tamko la Wakuu wa Nchi wa Afrika kwa nia ya kupeleka nishati ya umeme kwa watu wake. Waheshimiwa Wabunge, ninataka niwaambie kutoka kwenye sakafu ya moyo wangu na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye notes zangu aliniambia niliongeze hili, hiki mlichokifanya leo mmetenda uungwana mkubwa sana kwa Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa ninawasikiliza Waheshimiwa Wabunge, nywele zilikuwa zinanisisimka na sababu ni moja tu. Ni kawaida sana mwanadamu kuangalia mabaya kuliko mema. Ninyi mmefanya jambo kinyume chake. Kulitafuta jema ambalo Mheshimiwa Rais amelifanya na mkalisema kwa uchungu na kwa hasira kubwa kwamba ninyi mtaungana naye kusukuma mipango ya Serikali aliyonayo kwa ajili ya kupelekea umeme wananchi. Mngeweza kunyamaza, kwanza jambo lenyewe limeshafanyika wala hakuna mtu angewadai.

Mheshimiwa Spika, nyumba hii imethibitisha uungwana na ustaarabu wa kumwambia Mheshimiwa Rais, “Tuko na wewe, tunakuunga mkono, tunakutia moyo, tunakuombea, tunakutakia mema na utashi wetu kwako ni kuona Tanzania inaendelea.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali ambayo haikutarajiwa kabisa, hata kwa vyama vingine, wamesema walichofanya Chama cha Mapinduzi, kumweka mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea na Makamu wa wake Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi lilikuwa ni jambo jema.

Mheshimiwa Spika, nataka nimalizie tena kwa niaba ya wote tulio chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwenye sekta ya nishati, tutaenda kuisimamia mipango hii ili matokeo yapatikane. Mheshimiwa Rais na Bunge hili ambalo wakati wote limekuwa likitupa ushirikiano wa kuhakikisha kuwa tunapeleka umeme kwa watu wetu, tusingependa kuona haya yanabaki kuwa makaratasi, tungependa kuona yanakuwa matokeo yanayoonekana tena yasiyotetewa kwa maneno, bali yanayotetewa kwa vitendo na kuonekana hadharani bila kupigiwa debe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena kukushukuru sana kwa fursa hii, nawe mwenyewe tunakuombea kila la heri; na kwa kweli mtoa hoja tunakushukuru mno kwa kuja na hoja hii; na wale wote mliochangia tunawashukuru sana. Nimeona ulivyosema tuendelee kuchangia, Wabunge wote wakasema hayo yaliyosemwa hata tukisema tutarudia. Ni kama mimi ninarudia yale yale waliyoyasema, nisingependa kuwachosha kwa kuwashukuru.

Mheshimiwa Spika, naomba kusema, naunga mkono hoja na ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)