Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Awali ya yote kwanza nitoe shukurani kwa Serikali katika taarifa yao nimeona hapa kwamba wametujengea bwalo la chakula katika Chuo chetu cha Ruaha, sisi Iringa tunakiita CBTI.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa inaendelea kusema kwamba litakamilika Mei, nipende tu kutoa taarifa kwamba limeshakamilika tayari na wanafunzi wetu wa Chuo kile cha Maendeleo ya Jamii wanakwenda field. Kwa hiyo, watakaporudi mwezi Aprili wataanza rasmi kutumia, ninawapongeza sana kwa hilo lakini pia niwashukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa chuo kile sasa kinachukua wanafunzi wengi, bado tuna tatizo na changamoto kubwa sana ya usafiri. Kwa hiyo, Wizara mnaweza mkaona namna ambavyo mnaweza mkatusaidia na kusema ukweli nimshukuru sana Mkuu wa Chuo kwa sababu amefanya kazi kubwa ya kusimamia lile bwalo kisasa kabisa na niwapongeze walimu wote wa Chuo chetu kile cha Ruaha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno haya niipongeze pia Kamati kwa mchango wao wa mwisho kuona umuhimu wa elimu ya afya ya akili na kusisitiza Serikali ichukue hatua madhubuti kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa afya ya akili nchini, ninawashukuru sana. Pamoja na pongezi bado kuna taarifa maendeleo ya jamii na nilichangia kwenye Bunge lililopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna shida ya kupeleka fedha za mikopo kwa wafanyabiashara wadogowadogo ambazo zilikuwa zimetengwa karibu shilingi bilioni 22.9, lakini pia kuna fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya machinga shilingi bilioni 18.8. Kwa masikitiko makubwa sana tulichangia kwa uchungu kwamba fedha hizi ziende kwa wale wafanyabiashara wadogo zikawasaidie.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo makubwa sana Serikali imefanya na hapa kuna vitu vikubwa sana Kamati zimesoma inabidi vifanyike. Bado tunaendelea kufanya extension kubwa sana kwenye masuala ya afya na tunaendelea kulalamika kila siku kwamba tunatakiwa tuongeze vifaatiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbali sana katika maazimio ambayo ametoka kusoma Mwenyekiti wa Kamati, moja ya maazimio wametoa kwa ajili ya maambukizi makubwa ya VVU kwa vijana wetu wa miaka 15 mpaka 24 maazimio yao wanasema tutoe elimu ya kutosha kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeambiwa tuna matatizo makubwa matatu kwenye utapiamlo, kuzidi sana au kupungua sana. Zaidi ya kutoa elimu, Bunge lako Tukufu linaona kuna umuhimu wa kuwezesha jamii na ndio maana tukapendekeza hapa Serikali ichukue initiatives kuhakikisha kwamba tunapeleka mikopo kwa vijana wetu ili wapate kazi za kufanya, kwa sababu tunapoongelea utapiamlo pamoja na kwamba tutaongelea kwa Watoto, lakini ule mwingine hata sisi watu wazima.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana unaambiwa hata ukiwa tu na kitambi ni utapiamlo, umekula umezidisha au ukipunguza chakula na yenyewe pia ni utapiamlo. Leo hii vijana wetu walio wengi au tulio wengi tunakula chakula kilichopo, hatuli chakula kwa mahitaji ya mwili unaotaka, lakini hii yote ndiyo inapelekea utapiamlo. Hii inasababishwa na hali ya uchumi kuwa duni au umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongea hapa kuhusu watoto wachanga, watoto wachanga wanaopokuwa katika mazingira ya uchanga tunategemea wazazi au mama awe naye karibu mtoto mchanga. Mtoto anapokuwa kwenye level ya primary school mpaka sekondari O’ level tunategemea atakuwepo chini ya uangalizi wa wazazi, lakini anapotoka hapo anapokuwa nje kwenye society anategemea sisi jamii nyingine na Serikali iingie kwa kina kuhakikisha tunawaangalia hawa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa vijana wengi wapo mitaani wamejiajiri ndiyo tunasema ni machinga, ndiyo tunasema wafanyabiashara wadogo na walio wengi ni wa kiume. Wale wengi walio wa kike tunashukuru Serikali imeonesha namna ambavyo wamefanya uwezeshaji wa uchumi kwa wanawake na mpango walionao kuendelea kuwawezesha wanawake. Hizi fedha shilingi bilioni 18 ni kitu gani kwenda kuwawezesha vijana wetu ili watupunguzie utapiamlo kwenye hii nchi. Shilingi bilioni 22 ni kitu gani twende tukawawezeshe vijana wetu ili tuendelee kuwa na kizazi bora kwenye hii nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana sasa hivi siyo tu wanakula kilichopo, wameamua tu kunywa pombe kujizima data. Tuna vijana wanakunywa pombe mpaka unajiuliza niongee na nitoe wito kwenye Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Serikali ina dhamana ya kuwalea watoto hawa, hebu tuangalie hizi pombe tunazoruhusu na hapa ninafikiri ni suala mtambuka, Wizara nyingi zinaingia: ipo Viwanda na Biashara, ninajua kuna vijana na kutakuwa na Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu Mheshimiwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, awakusanye wenzake wakae waone namna gani wana-rescue hili kundi la vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtu akiwa amelewa atakumbukaje hata ukimwelimisha kwamba anatakiwa atumie zana hizi kufanya mapenzi asipate maambukizi. Leo hii kuna vipombe vinanywewa mpaka alcohol 40, 30 watoto wanakunywa. Nimekwenda kwenye ziara siku moja, ninafanya mkutano nikapata kero kutoka kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, akinamama hata wale wengine wanaouza pombe vilabuni nao wamekuwa wakemia, kwenye zile pombe kuna vitu wanaongeza. Sisi wengine tumekuwa tulikuwa tunaona bibi zetu, babu zetu wanakunywa ulanzi mpaka wanafariki hawajawahi kupata matatizo ya figo, hawajawahi ungua maini, hawajawahi ungua nini maisha yanaendelea, lakini vijana wa leo umri huo huo wa miaka 15 mpaka 24 akinywa pombe tu mfululizo miezi miwili ameshakufa, ameungua ukimwangalia haeleweki akili imekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba tuone Wizara wana taratibu gani pamoja na kutoa elimu. Naomba niongeze azimio lingine, azimio lingine liwe ni pamoja na kupambana na vile vitu vyote vinavyochochea kufanya ngono zembe ikiwepo ulevi uliokithiri. Tusitoe tu elimu ili kuwakinga hawa; lakini pamoja na kupambana na vitu kama hivi ambavyo vinachochea ngono zembe lazima pia tupambane kuhakikisha kwamba tunawawezesha kiuchumi watoke huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo unaleta hoja tu kwamba hizi shilingi bilioni 22 zilizotakiwa zipelekwe kwa wafanyabiashara wadogo wadogo hazikwenda eti kwa sababu taasisi inayotakiwa kukopesha haikutokea kwa muda, kwa hiyo fedha hazikupelekwa kweli? Serikali imekosa taasisi ya kwenda kukopesha vijana wetu kuwasaidia wapate hiyo mikopo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi bilioni 18 zimeombwa, kibali hakikuombwa sijui zimevuka mwaka. Hizo shilingi bilioni 22 ni kiasi gani cha hela ambacho tunashindwa kusema tutoe tu hata sadaka wala haifiki hata fungu la kumi la mapato ya nchi yetu kwa ajili ya ku-rescue vijana wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayaongea haya leo ukienda huko mitaani kama Waheshimiwa Wabunge huwa tunahudhuria misiba na labda haijafanyika analysis sasa hivi vijana wetu wanafariki sana. Wana matatizo ya figo wengi, wana shida za kupumua (mapafu) wengi lakini cha msingi hapa vijana hawa uwezeshaji wao kiuchumi bado ni duni.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ni vijana ambao tumewekeza kwa kiasi kikubwa kuwajengea shule za kata, kujenga vyuo vikuu, kujenga vyuo vya kati, tumewajengea hizo hospitali wanazaliwa vizuri, wanakwenda hospitali za wilaya wanazaliwa vizuri, baada ya kutoka pale wanakwenda kuishia kwenye kitu kidogo tu pombe. Yaani dozi wanayopewa vijana hawa ya pombe haiendani na uzito wao. Anakwenda kutumia alcohol 30 wakati yeye mwenyewe ukiangalia uzito wake 50, kilo 50, kilo 60 wana-faint. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jamii yetu ni nani atakayeilinda kama siyo sisi viongozi tuliopewa dhama tukaamua kuingia? Sisi tutengeneze sheria na utaratibu. Sasa nimekwenda kwenye ziara wale akinamama wanaopika pombe na wanaouza pombe wanalalamika kwamba wanaojumua pombe hawawalipi, wale wajumua pombe ninawauliza, wanasema madamu walevi wenyewe ndiyo kama unavyowaona wamechoka, hawana kitu tunawakopesha tu hawatulipi.
Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hawa ndiyo akinamama waliokopa hela huko hazirudi kwenye Mfuko wa WFP sijui huko hazirudi na hawa huku wanakunywa wanajiua, baada ya kujiua wanataka mashine za dialysis kwenye kila kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hawa ndio wanaokwenda kuzaa au wanaoa wanawapa ujauzito mabinti wale watoto wanazaliwa kutokana na masuala ya ulevi wanakwenda kuzaliwa kabla ya umri tunapata watoto njiti wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaanza kuhangaika hapa na surfactant ya kuwasaidia watoto kwa gharama kubwa, lakini kumbe solution ilikuwa ni kuwa-rescue hawa wazazi ili mwendelezo wa hilo tatizo usiendelee tuwe tumejiokoa kwenye mambo mengine...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninawapongeza Kamati kwa hoja nzito ambazo wamezitoa na tunaomba maazimio yao yafanyiwe kazi. Ninaomba Wizara ikae iangalie suala la ulevi uliokithiri. Ahsante.