Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika hii hoja ambayo imewasilishwa na Wenyeviti wa Kamati hapo mbele. Awali ya yote ningependa kutumia nafasi hii kuendelea kuipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna wanavyofanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. Kwenye Kamati tulijadili mambo mengi mengine yameweza kuingia katika taarifa lakini mambo mengine hayakuweza kuingia lakini niseme tu kuna baadhi ya mambo ningependa kuyaongelea kama sehemu ya kukazia au kutoa ushauri kwa Bunge letu ili mnapokuwa mnatoa maelekezo kwa Serikali yaweze kufanyiwa kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona katika taarifa suala la wastaafu kulazimika kupewa nyaraka zenye namba ya malipo kwa ajili ya kulipa madeni ya waajiri wao ili wapate mafao limeonekana na ni ukweli kwamba hata ningekuwa ni mimi kama hiyo ndiyo fursa ya kuweza kunifanya nipate mafao yangu ningeweza kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ombi maalum kwa Bunge lako Tukufu kuielekeza mifuko ambayo ilibainika watumishi wao walitoa namba za malipo kwa watumishi wastaafu wakaenda kulipa, zile fedha zirejeshwe. Pia, ningeomba Bunge lako Tukufu litusaidie kutoa maelekezo kwa Serikali iwe ni marufuku na mwiko kwa mtumishi yeyote kushindwa kulipwa mafao yake eti kwa sababu wao walishindwa kufuatilia michango yao kwa waajiri wao. Kwa hiyo, hilo nilitamani kama Bunge tuweze kulichukua na kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujielekeza pia kwenye programu ya kukuza ujuzi nchini. Tunaipongeza Serikali kwa hatua iliyofikia ya kufanya jitihada ya kuendelea kuwajengea vijana wetu ujuzi mbalimbali. Tulifanya ziara tuliwaona vijana, tuliwakuta ni vijana wenye furaha, lakini ilionekana kwamba katika lengo la Serikali lilikuwa ni kuwafikia vijana 136 kwa mwaka. Mpaka sasa hivi Serikali inafikia vijana 12,000 tu ambao ni sawasawa na 8.82% tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nina maombi kuwaelekeza Serikali kuwa na lengo na dhamira ya dhati, ya kuhakikisha wanafikia hili lengo la vijana 136,000 na kama haiwezekani basi angalau wafike 50%. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa na changamoto wakati wa mafunzo kwamba ule muda wanaopewa vijana, muda hautoshi kwa hiyo, kuna baadhi ya vitu unakuta hawafundishwi wanapokuwa kwenye hayo mafunzo na vyeti wakati mwingine unakuta hawapatiwi kwa sababu hawajafuzu ile course ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba Bunge lako Tukufu lisaidie kuielekeza Serikali kwamba wanapokuwa wanatoa mafunzo haya wazingatie muda maalum wa yale mafunzo. Pia, watusaidie kuwapatia wale vijana vifaa ambavyo wataenda kuanzia kazi baada ya pale. Haina maana watu vijana wanapatiwa mafunzo, halafu baada ya hapo wanakuwa wanarudi nyumbani kukaa hawajapewa mkopo, hawajapewa vifaa na vitu kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, kumekuwepo na hizi programu mbalimbali kwenye Wizara tofauti za kukuza ujuzi kwa vijana. Mfano tunafahamu Kilimo wana programu ya BBT, lakini Wizara ya Mifugo pia ina namna inavyoendelea kukuza vipaji vya vijana, lakini tunaona kwenye Michezo, TAMISEMI wana programu ambazo zinasaidia kukuza ujuzi kwa vijana. Hakuna bodi ambayo imewekwa kwa ajili ya kuratibu hizi programu zote.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kupitia Bunge lako hili Tukufu, Serikali iweze kuiwezesha hii Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye upande wa ajira, kazi, vijana na wenye ulemavu waweze kuwa na uratibu ili tuwe na namna nzuri ya kupata data za vijana ambao wajengewa uwezo. wasipokuwa na uratibu madhubuti kwa ajili ya hawa vijana tutakuwa tunafanya kama marudio, kijana huyo huyo anaenda kujengewa uwezo huku, anaenda kujengewa uwezo huku kitu ambacho kinakuwa siyo kizuri kwa masilahi ya Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia kwenye suala la mikopo, tunafahamu dhamira ya Serikali kuanzisha mifuko ya mikopo kwenye Wizara mbalimbali kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu ilikuwa ni nia njema kabisa lakini kumekuwa na mtiririko au mwendelezo wa kupanga bajeti ambayo itatolewa kwenye hii mifuko ya mikopo, lakini haiendi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kwenye hii Wizara ya Maendeleo ya Jamii tunaona shilingi bilioni moja ilikuwa imetengwa, kwamba iwe inatolewa kila mwaka kwenye mfuko wa vijana, the same applied lakini hizi fedha haziendi almost six years mpaka saa hizi hawajapatiwa hizo fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta ile mifuko inadumaa haina fedha lakini na kwa ile fedha ambayo ipo ambayo inakuwa revolved, yaani ile fedha ambayo ilitolewa awali ambayo inatakiwa iwe revolved fedha nyingi zipo kwenye halmashauri hawarejeshi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba kupitia Bunge lako hili Tukufu kama sehemu ya Maazimio ya Bunge, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI azielekeze halmashauri zake kuhakikisha zinatoa hizo fedha kwenye hiyo mifuko yaani zirejeshwe hizo fedha badala ya fedha hizo za Wizara kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa pia kuongelea suala la benki ambazo zinaenda kwa wananchi kuwafungulia akaunti kwa lazima kwa kigezo kwamba watawapatia mikopo. Imekuwa ni changamoto, watu wanafunguliwa akaunti halafu katika kufunguliwa akaunti wanaahidiwa mikopo, mikopo hawapewi fedha zao za kufungulia akaunti zinaenda na wakati mwingine zinapotelea huko huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kesi hii ambayo kwa kweli haituweki vizuri kwa wananchi wetu, Serikali yetu inaonekana ina watu wababaishaji ambao hawawezi ku-control hizi benki kuchukua hizo fedha kwa wananchi. Ninajaribu tu ku-imagine ukiongelea wananchi laki tano wakachangishwa shilingi 10,000 kufungua akaunti ni almost shilingi bilioni tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hili pia ninataka kuomba Serikali ielekeze benki zote ambazo walienda kufungua akaunti kwa kigezo kwamba watatoa mikopo wapeleke fedha kwa wananchi. Mbaya zaidi wanatutumia wanasiasa tufanye hamasa kwa wananchi wetu kitu ambacho kinatuweka kwenye hali ngumu ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba pia niweze kuchangia kwenye upande wa afya kidogo. Tumekuwa na utaratibu wa kwamba rufaa zote zinazotolewa kwenye nchi yetu uelekeo ni India. Ninatamani kufahamu kwamba, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha sasa tunaongeza nchi za kutoa rufaa, kama tutakuwa na wagonjwa ambao wamezidiwa? Hawezekani kila kesi ni India, kwa nini kusiwe na nchi nyingine mbadala, ambazo nazo tunaweza tukafanya nazo kazi kwa upande wa afya?

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninashukuru sana kwa kupewa nafasi na ninaunga mkono hoja. (Makofi)