Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Makete
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Jambo la kwanza naomba niunge mkono hoja ya Kamati hii, hoja ambayo imekusudia kuboresha sana maeneo ya Sekta ya Afya. Jambo la pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa tuzo, ya kushusha vifo vya watoto kutoka 556 hadi 104, ambayo majira haya ya mchana, saa sita, anakabidhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuzo ya Bill Gate Goalkeepers Award ni kitu kikubwa kwa Taifa letu. Kwa kweli, sisi tunaona kwa macho kuimarika kwa Sekta ya Afya nchini kumepunguza sana vifo vya watoto kwa hiyo, tuna kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais na Chama Cha Mapinduzi kwa sababu, hili lilikuwa ni mkakati wake wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia mambo mawili; la kwanza, ni kuhusu bima ya afya kwa wote, lakini nitachangia kuhusu MSD. Mwenyekiti wa Kamati amezungumza na nimpongeze Mheshimiwa Kingu kwa kusoma vizuri hotuba yake na tumemwelewa vizuri. Kama mdau ninapenda pia, kuipongeza Kamati hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bima ya afya kwanza nianze kwa kumpongeza Dkt. Irene Isaka, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Bima ya Afya, madam huyu ambaye ni mchumi kwa kweli, tumeona mabadiliko kwenye ukusanyaji wa mapato wa mfuko huu. Ambapo unaona mapato sasa yamekuwa kutoka ukusanyaji wa shilingi bilioni 696 yameenda shilingi bilioni 756. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii inaleta tafsiri ya kwamba, watendaji na wasaidizi wa Mheshimiwa Rais ambao amekuwa akiwaamini kwenye nafasi zao wanafanya kazi vizuri sana. Lazima tumpongeze Dkt. Irene Isaka popote alipo, chapa kazi na sisi kama Wabunge tutakuunga mkono na tutaendelea kumuunga mkono kwa sababu, tunaona mabadiliko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni akinamama wanaonesha kwamba, wanaweza wakiaminiwa na wameaminika kwa kweli, wanafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kuboresha suala la bima ya afya, Kamati imezungumza suala la kuimarisha mifumo. Moja kati ya changamoto kubwa ambayo tunaipata ni mifumo kutokusomana. Kitendo cha mifumo kutokusomana kunafanya mfuko uingie shoti au hasara kwenye mambo mengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG anaripoti anasema mwaka 2020 hadi mwaka 2022 Serikali au Mfuko wa Bima ulilipa shilingi bilioni 14 kinyume na utaratibu kutokana na kupewa taarifa fake kutokana na kwamba, mifumo ilikuwa haisomani kwenye vituo vya kutoa huduma kwenye eneo la bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Maazimio ya Kamati aliyoyasema kwamba, lazima mifumo ya afya isomane na naliunga mkono hilo kwa sababu, imekuwa ndiyo kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba, mifumo yote nchi hii ni lazima isomane, ili kuondoa upotevu wa mapato na kuondoa hasara ambazo zimekuwa zikijitokeza kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili ni muhimu sana kwa sababu, pia, tunaenda kwenye bima ya afya kwa wote, ili mfuko huu uwe imara. Ni lazima ukusanyaji wa mapato uwe imara, lakini ni lazima malipo yanayolipwa yawe ni malipo sahihi, siyo ya udanganyifu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, CAG amekuwa akiripoti mara kwa mara kwamba, unakuta bima ni ya mwanaume halafu inasomeka kule imetumika na mwanamke, ni kwa sababu ya kutokusomeka kwa mifumo. Kwa hiyo, niiombe sana Serikali tuunge mkono jitihada za mifumo kusomana kwenye eneo la bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, nimpongeze Dkt. Irene Isaka kwamba, vituo vya kutolea huduma vimeongezeka kutoka 9,186 hadi 14,000. Hili ni jambo kubwa kwamba, tunaendelea kumsogelea Mtanzania, kwa ajili ya kuweza kumtolea na kumpatia huduma ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge hili linastahili kujipongeza. Kwenye Bunge la Bajeti lililopita Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Afya, alisimama hapa akaainisha vyanzo vya kuweza ku-support Mfuko wa Bima ya Afya kwa watu wasiojiweza.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunakiri hapa, tunazungumza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, wamekusanya zaidi ya shilingi bilioni 47, Bunge ni lazima tuipongeze Serikali kwa hatua hizi kwa sababu, wakati tunazungumza miezi sita iliyopita tulikuwa na shilingi sifuri, leo hii tunazungumza tuna shilingi bilioni 47 zimekusanywa, kwa ajili ya kuwezesha Mfuko wa Bima ya Afya kwa watu ambao hawajiwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni kwamba, Serikali ina nia, Serikali imekusudia kuhakikisha bima ya wote inawezekana Tanzania. Hili ni jambo la kujipongeza na Bunge ni lazima lijipongeze kwa sababu, jambo ambalo lilikuwa limelipitisha sasa linafanyika na limeanza kukusanya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kuimarisha Mfumo wa Claims Management Information System ni vyema Serikali ikalifanya hili jambo kwa uharaka sana kwa sababu, tusipofanya kwa uharaka bado tutakuwa na changamoto ya utoaji wa huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo kipo Makete na madai yanatakiwa yaende Dar es Salaam, kama mifumo haijasomana ni lazima tutaendelea kupata changamoto kwenye Mfuko wetu wa Bima ya Afya. Kwa hiyo, ninaiunga mkono Serikali na Kamati kwenye maazimio waliyotoa kwamba, kuhakikisha lazima bima yetu iweze kusomeka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwenye jambo la MSD. Tunapozungumzia MSD tunazungumzia ununuzi, uzalishaji na utunzaji wa vifaa vya afya kwa maana ya dawa na vitu vingine ambavyo vinahusika na vifaa vya afya. MSD ya kwetu Serikali inahitaji mtaji wa karibu shilingi bilioni 561, kama sikosei, kwa ajili ya kufanikisha uzalishaji, ununuzi na utunzaji wa vifaa vya afya. Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 100, tupongeze kwa jitihada hiyo ambayo ni sawasawa na 17.5%. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuikumbushe Serikali, tunapoimarisha bima ya afya kwa wote ni lazima tuimarishe na mfuko wa upatikanaji wa dawa kwa maana ya bohari. Hivi vitu viwili vikiwa imara kwenye nchi Sekta ya Afya inakuwa salama na inakuwa ni ya kuaminika. Sasa ni muhimu sana Serikali tukachukua hii initiative, tunahitaji shilingi bilioni 456, ili tuweze kuuwezesha mfuko uwe full funded na uweze kuhudumia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninayezungumza niseme wazi, ninatoka Mkoa wa Njombe ambako kimejengwa Kiwanda cha Kuzalisha Gloves na katika mahitaji makubwa ya hospitali ni gloves (examination gloves). Mkoa wetu umejengwa hicho kiwanda na tayari kimeshazalisha gloves 4,000,000, hizi ni jitihada za Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni lazima tuipongeze Serikali yetu. Badala ya kuagiza gloves kutoka nje sasa gloves zinapatikana ndani ya nchi hii, kwa ajili ya ku-support huduma ya afya kwenye Taifa letu. Kwa hiyo, ni lazima tumuunge mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna uwekezaji kwenye hii bohari, hizi fedha ambazo zinahitajika tumwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha iangalieni, bohari ikiwa imara dawa zikapatikana, ndivyo ambavyo bima ya afya kwa wote pia, itakuwa na tija kwa Watanzania, ambapo wakienda kwenye vituo vya afya watapata huduma na dawa kwa uhakika, hii inaweza ikawa imetu-support.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali kwa ujumla, waangalie Mfuko wa Bohari (MSD) uweze kupata fedha, kwa ajili ya uwekezaji. Mtaji unaohitajika ni shilingi bilioni 400 na pointi ni hela ambayo nadhani ipo ndani ya uwezo, shilingi bilioni 461 ipo ndani ya uwezo kabisa wa kui-support bohari hii iweze kuleta tija kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kabisa Mkurugenzi kwa sababu, pia na yeye ameongeza ukusanyaji wa mapato. Mkurugenzi wa bohari ameongeza ukusanyaji wa mapato kutoka shilingi bilioni 378.77 amefikia shilingi bilioni 553, siyo kiwango kidogo, siyo haba. Ni nini wanachokihitaji? Ni kwamba, tuwapatie fedha ya mtaji, ili iweze kufanya kazi ambayo imekusudiwa na Watanzania waweze kupata vifaa tiba kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niipongeze Serikali yangu kwa utekelezaji wa ilani ambao unafanyika kwenye Sekta ya Afya, hususani kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kiwango kikubwa, kama Mheshimiwa Rais ambavyo amefanya leo. Nakushukuru sana. (Makofi)