Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

nakushukuru sana kuniruhusu nichangie hoja hii iliyopo mezani kwetu leo, inayohusu Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwaka 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie maeneo ninayodhani ni muhimu, lakini pia, naona kwamba, yanahusu ushauri wa Bunge kwa Serikali. Nayo ni Shirika letu la OSHA au Mamlaka ya OSHA ambayo yanasimamia usalama na afya mahali pa kazi na pia, SDL ule mfuko wa kuendeleza ujuzi wa wafanyakazi na vilevile kuendeleza ujuzi wa vijana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA). OSHA ilipoanzishwa na Sheria Na.5 ya Mwaka 2003, ilikuwa na malengo na makusudio mahususi kusimamia usalama wa afya mahali pa kazi hivyo, kupunguza ajali na magonjwa ya waajiriwa au vifo mahali pa kazi. Aidha, matokeo ya usimamizi huo wa OSHA ungeongeza tija na uzalishaji wa mali na hatimaye kukuza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, OSHA ina changamoto moja sasa kwamba, Sera ile ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya Mwaka 2010 imepitwa na wakati, imekuwa nje ya Miongozo na Kanuni za ILO. Hili ni Shirika la Kazi Duniani ambalo limesimamia ajira na shughuli za ajira na kusimamia waajiri, wafanyakazi, vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri. Makao yake Makuu ya hili Shirika yapo Geneva na kila mwaka Tanzania inawakilishwa kule na waajiri, yenyewe kama Serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kwenda kule Geneva tunaridhia kanuni na miongozo hii, lakini OSHA ili ifanye kazi vizuri ni lazima iwe na tija. Tija hii itatokana na sera ya usalama na afya mahali pa kazi endapo itaboreshwa, lakini pia, OSHA inakabiliwa na matatizo makubwa sana. Moja, ni upungufu wa kupanuka katika maeneo mengine ya nchi yetu, ipo sehemu chache sana. Vilevile, OSHA ina upungufu wa wafanyakazi na majengo maeneo ya kufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu programu ya kukuza ujuzi na utumishi nchini, mpango umeanzishwa. Mpango mahususi ni muhimu na ulifikiwa kwa makubaliano kati ya waajiri wa sekta binafsi na Serikali, ikiwa ni sehemu kubwa ya kuboresha mazingira ya biashara nchini (easy of doing business).

Mheshimiwa Naibu Spika, programu hii ikisimamiwa vizuri na kufaulu itapunguza ajira zisizo na lazima kwa wageni na pia, itatibu suala la waajiri kutafuta watumishi nje ya nchi na hivyo, kupunguza fursa kwa vijana wetu kuajiriwa hapa nchini. Waajiriwa wa kigeni wana gharama kubwa sana na hivyo, kuongeza gharama za wafanyakazi na waajiri.

Mheshimiwa Naibu Spika, programu hii inagharamiwa na waajiri, waajiri wanatozwa tozo ya asilimia 3.5 kwa kila mwajiriwa na tozo hii inatengeneza hela ambazo zinatakiwa ziende sasa kwa ajili ya Skills Development Levy, ambayo hii kodi kwa makubaliano ya Serikali na waajiri theluthi moja ya SDL itumike katika program ya kukuza waajiri, ujuzi na theluthi moja nyingine iende kwa ajili ya kukuza mikopo ya elimu ya juu. Nini kinatokea?

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ilipewa na takwimu za kusikitisha kwamba fedha hii haitoki Hazina licha ya kulipiwa na waajiri. Idadi ya watarajiwa waliotakiwa kufundishwa au kupewa ujuzi huu imeshuka kutoka vijana 42,000 mpaka leo 12,000 kwa mwaka na sababu ilikuwa hela haipatikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa maendeleo ulilenga kufundisha au kutoa ujuzi kwa watu au vijana 681,000 kupitia ujuzi ndani ya miaka mitano. Sasa vijana 136 kwa mwaka, lakini sasa hivi vijana wachache wapatao 12,000 tu wanapatikana. Hii ni upungufu mkubwa kuliko ambavyo ilikusudiwa na matokeo yake tunapoteza fursa ya vijana kusoma na kupewa ujuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe kwamba Mfuko huu ulikusudia pia kufundisha wafanyakazi ambao wapo kazini wakapate ujuzi, lakini mapungufu haya yanaonekana wazi wazi kwamba waajiri bado wanachukua wafanyakazi kutoka nje ya nchi kwa kisingizio kwamba waliopo hapa nchini hawana ujuzi ni muhimu Serikali ikaongeza hela kwenye Mfuko huu ili uweze kutimiza wajibu wake kama ambavyo imekusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninatoa pongezi kubwa sana kwa viongozi wa Wizara zangu zote mbili, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Dorothy Gwajima, Makatibu Wakuu wote na wasaidizi wao lakini hongera kubwa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuweka nia ya kuendeleza ujuzi kwa vijana wote ili waweze kupata kazi hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya haya machache, naunga mkono. (Makofi)