Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Kwanza kabisa naipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, vilevile na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna walivyoboresha kwa kiwango kikubwa sekta ya afya. Ninampongeza Waziri wa Afya Mheshimiwa Jenista Mhagama, Naibu Waziri Dkt. Mollel, pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri mnayoifanya katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Masuala ya UKIMWI na Wajumbe wote kwa taarifa nzuri pia ninampongeza sana Mwenyekiti kwa jinsi anavyoiongoza ile Kamati katika kuishauri Serikali na kwa usomaji mzuri wa taarifa yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeimarisha huduma za afya kwa kiwango kikubwa sana ndani ya Tanzania kama tulivyosikia, katika kipindi kifupi imeweza kuongeza vituo vya kutolea afya zaidi ya 1,368, lakini hospitali ambazo sasa zinatoa huduma ya dharura zimepanda kutoka saba zilivyokuwa mwaka 2020 na sasa hivi mwaka 2024 ni 116.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kwenye hospitali zetu za rufaa za mkoa tuna ultrasound zimewekwa, digital x-ray zipo na sasa hivi watu wanafanyiwa dialysis huko mkoani, hawatakiwi kwenda mpaka kwenye kanda. Ukienda kwenye hospitali za taifa kuna cath lab na kuna angio suite.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Afrika nzima kuna nchi tano tu ndizo zenye PET scan. PET scan ni mashine ambayo inaweza ikatambua magonjwa kama saratani hata kama ndiyo imeanza tu. Nchi hizo tano ni Egypt, Ethiopia, South Africa, Kenya na Tanzania tumo. Kwa hiyo, tuna sababu zote za kumpongeza mama yetu kwa jinsi anavyoendelea kuboresha sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa huduma za kibingwa na kibobezi na hivyo vifaa vingi vizuri vya kisasa sasa kumeleta ukuaji wa utalii tiba. Hadi mwaka 2024, tumepata wagonjwa zaidi ya 7,843 kutoka nchi za nje ambao wamevutiwa, sasa na badala ya kwenda India na mahali pengine wanakuja Tanzania kutafuta matibabu. Ahsante sana Wizara ya Afya kwa kazi nzuri na ahsante sana Mheshimiwa Rais kwa kuboresha Sekta ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera unakumbwa na magonjwa yanayoambukiza pamoja na ya mlipuko mara kwa mara. Kiasi ambacho hata nchi jirani wakisikia kwamba kuna kaugonjwa kama Ebola kametokea au Marburg, basi unakuta watu wanaanza kuwa na wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaendelea kuomba kama ambavyo tunaendelea kuomba kila siku, kwamba, kwenye mpaka kati ya Burundi na Tanzania pale Kabanga, kwenye mpaka wa Rwanda na Tanzania pale Rusumo, kwenye mpaka wa Kyerwa na Uganda pale Morongo, tujengewe isolation centers ili kusudi wale wasafiri wanaokuwa wametoka kwenye nchi za jirani wakiwa wanaingia Tanzania wakishukiwa, waweze kuwa isolated pale pale ili kusudi wasiingie Tanzania na kuweza kusambaza magonjwa kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali walituahidi kutujengea hospitali kubwa ya kisasa ambayo itawachukua wale waliokuwa isolated kwamba inawezekana wana haya magonjwa ili waweze kupimwa vizuri na kupata tiba inayofaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba mchakato unaanza lakini tunauliza, ujenzi wa hospitali hiyo unaanza lini? Kwa sababu kwa kila mwaka ni lazima kuna kamlipuko fulani Mkoani Kagera. Kwa hiyo, tunaomba Serikali walione hili, watenge fedha za kutosha ili hii hospitali kubwa ya kisasa ijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, historia imeandikwa na Watanzania tutamkumbuka Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha uanzishwaji wa bima ya afya kwa wote. Bunge lako Tukufu lilipitisha Muswada wa Sheria hii tarehe Mosi Novemba, 2023 na Mheshimiwa Rais akawa amesaini ikawa sheria tarehe Mosi Disemba, 2023. Sasa hivi kanuni ziko tayari na sheria hii imeanza kufanya kazi tangu tarehe 13 Septemba, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, Bima hii na kitita cha huduma muhimu. Ukishakichukua kitita hiki unatibiwa wewe, mwenzi wako na wategemezi wengine wanne, yaani watu sita. Sina uhakika kama Watanzania wanajua kwamba kwenye bima hii nzuri, bima ya afya kwa wote kuna kitita kizuri kama hicho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kitita hiki watu walifikiri kwa sababu ni kitita ambacho kila mtu ni lazima akipate, kwamba labda huduma zitaishia kwenye zahanati. Kitita hiki kufuatana na kanuni zilizopo kinakuruhusu kutibiwa tangu kwenye ngazi ya zahanati na kama ugonjwa wako unahitaji kwenda mpaka hata kwenye Hospitali ya Taifa kama Muhimbili, unaweza kupelekwa kule kwa njia ya rufaa. Kwa hiyo, ni kitita kizuri sana. Tuwahamasishe watu waweze kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili bima hii iweze kufanikiwa ni lazima kuwe na utaratibu wa kuwatambua watu ambao hawana uwezo. Ndiyo, Serikali wanasema kwamba watatumia TASAF, Ofisi ya Takwimu na watatumia TAMISEMI, lakini ni lazima ule utaratibu utakaotumika kumtambua yule fulani kwenye kijiji kwamba huyu ndiye hana uwezo, uainishwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu zaidi ya 26% ya Watanzania wanatambuliwa kwamba ni maskini. Hatuwezi kuwabeba wote kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, ni lazima kuwe na vigezo vya kumtambua yule ambaye hana uwezo kabisa wa kuanza kumhudumia. La siyo hivyo, huu Mfuko utaelemewa na utashindwa kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili Mfuko huu au Bima ya Afya iweze kufanya kazi, vilevile Serikali ni lazima itambue vyanzo ambavyo ni endelevu. Ninajua hapa Serikali ilikuja na vyanzo ambavyo nimevitaja, lakini kwa sababu masikini ni wengi Tanzania, tunaomba Serikali iendelee kutafuta vyanzo vingine vingi zaidi ambavyo ni endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, kila mapato yanayotokana na chanzo fulani, waainishe kinagaubaga kwamba ni asilimia ngapi kutoka kwenye chanzo hicho inaenda kwenye bima ya afya, siyo kutaja tu. Vilevile, hizo hela zikishaingia mle ziweze kulindwa, ziwe ringfenced na ziweze kufanya kazi ya kuwahudumia wale watu ambao hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu, ugonjwa haupigi hodi. Ugonjwa unaweza ukamshambulia mtu yeyote wakati ukiwa huna hata senti tano. Kwa hiyo, ndiyo maana ninaomba Wizara ya Afya, NHIF na Waheshimiwa Wabunge wenzangu tukiwa kwenye mikutano yetu tuendelee kuwahamasisha watu wajue kwamba mkombozi wetu ni hii bima ya afya kwa wote. Tuingie ili kusudi sisi na wapendwa wetu tuendelee kutibiwa kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, UKIMWI umewatesa Watanzania wengi kwa muda mrefu. Hadi leo tuna Watanzania zaidi ya 1,700,000 ambao wanaishi na UKIMWI na wengi kati yao wako kwenye matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs). Kati ya hao, 63% ya hao wenye UKIMWI ni wanawake; na ukiangalia kwenye hayo maambukizi mapya 28% ya wenye maambukizi mapya ni vijana ambao wako kati ya miaka 15 mpaka 24…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa
muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante…

MHE. BENARDETA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaona kwamba bado tuna tatizo lakini takwimu zinaonesha…