Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja za Kamati mbili ambazo ziko mezani. Hoja ya Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI na Hoja ya Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, ambazo zimewasilishwa vizuri sana na Wenyeviti; Ndugu yangu Mheshimiwa Elibariki Kingu ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya na pia Mama yangu Fatma Toufiq kwa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa sana kwenye Sekta ya Afya. Sisi wote tunashuhudia ambavyo watu wetu wameendelea kupunguziwa mwendo wa kupata huduma za afya, lakini dawa pamoja na vifaa tiba vimekuwa vikipatikana na huduma muhimu ambazo zilikuwa hazipatikanani katika maeneo yetu sasa zinapatikana, ikiwemo mashine za MRI pamoja na ultrasound, ambayo ilikuwa inapatikana mbali kutoka kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili uweze kupata matibabu sahihi kwanza ni lazima upate vipimo. Eneo la vipimo lilikuwa ni changamoto lakini kwa sasa maeneo mengi yanakwenda vizuri, na tunampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya na dhamira yake ya kuhudumia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi tunampongeza Mheshimiwa Rais, kwamba angalau taasisi mbalimbali zinazohusika na mambo ya afya duniani zinamtambua katika jitihada zake na Serikali yake. Leo tunaambiwa anapata tuzo hii kwa ajili ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, ambalo lilikuwa ni tatizo kubwa sana. Tumetoka kwenye vifo 500 mpaka 100, maana yake ni kwamba, kazi kubwa imefanyika. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka nichangie katika maeneo machache katika kuongeza ushauri wangu kwenye Kamati hizi mbili. Kwanza, ninataka kupongeza kazi kubwa inayofanywa na MSD. MSD inafanya kazi kubwa sana; inasambaza dawa katika maeneo yetu ya vituo vya kutolea huduma. Tunaona magari yanavyozunguka katika maeneo ya vituo vyetu kwenye vijiji vyetu, kata na wilaya zetu. Kazi kubwa inafanywa na MSD katika kusambaza vifaa tiba pamoja na huduma nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo wote tunajua, na tumempongeza sana Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza kwamba changamoto kubwa ni mtaji. Wenzetu wa MSD hawana mtaji wa kutosha. Waliomba shilingi bilioni 561 lakini wamepatiwa shilingi bilioni 100 ambayo kimsingi kwenye uwekezaji ni fedha kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ombi langu, ninaomba waangaliwe, waongezewe hizi fedha. Kwa sababu wamelenga pia kwenda kuhakikisha kwamba kwenye vile viwanda vya kuzalisha dawa; kilichoko pale Keko, Dar es Salaam pamoja na kile kule cha Arusha Pharmaceutical, kimsingi ambacho ni kiwanda kizuri, kikiwezeshwa kitazalisha dawa nyingi hapa nchini na hivyo tutaondokana na kuagiza dawa kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, zile fedha za kigeni zitatumika kwa kazi nyingine. Kwa hiyo, nasi tutauza nje ya nchi na tutapata fedha za kigeni ambazo tutaweza kununulia bidhaa mbalimbali tunazohitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali ambayo pia ina shares katika Kiwanda kile cha Keko kwa 70%, kwa hiyo ni kiwanda cha Serikali; ninaomba sana wawaangalie, waweze kuwapatia fedha kwa ajili ya kufanya hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama haitoshi, tumeona wamepandisha mapato kutoka shilingi bilioni 378 hadi shilingi bilioni 553. Hili siyo jambo dogo, ni jambo kubwa. Tunawapongeza sana taasisi hii kwa kuweza kuongeza mapato na tunampongeza Mkurugenzi, Mr. Mavere pamoja na menejimenti yake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kusimamia MSD. Hongera sana, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunao wenzetu wa NHIF ambao wanasimamia suala la bima ya afya kwa wananchi. Kwenye eneo hili tumeeleza kwamba tumekuja na mfumo huu wa bima ya afya kwa wote. Ni kazi nzuri, lakini hawa wenzetu wa bima ya afya wakiwezeshwa wataweza kufanya kazi sana kwa kutumia bima ya afya kwa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba sana kwamba mifumo ya kudhibiti mapato iimarishwe kwa kusomana kama ambavyo tumeona imeelezwa kwenye Kamati. Yale wanayoyahitaji yakifanyika vizuri, vituo vikasomana, tutaondokana na watu kufanya mambo ambayo hayako sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupoteza mapato nalo linaweza likadhibitiwa vizuri na kuufanya Mfuko kuwa na uwezo wa kuwahudumia wananchi wetu na kuweza kuongeza uwezo mkubwa wa kuweza kuhudumia wananchi walio wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili tunampongeza Mkurugenzi, dada yetu Ndugu Irene pamoja na wenzake wote kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuhakikisha kwamba wanaboresha Mfuko huu. Zaidi tumeona, kwamba wamepandisha mapato kutoka shilingi bilioni 696 mpaka shilingi bilioni 756. Mifumo ikisomana vizuri tutaona namna ambavyo watapandisha zaidi kwenye eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni kwenye eneo la mikopo. Mikopo hii ilitolewa kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kujiwezesha kiuchumi. Tuliangalia Mfuko kwenye maeneo mengi, ambapo huko nyuma Mfuko haukufanya vizuri sana; lakini kwa sasa tumekuja na mfumo mpya kwenye fedha hizi. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuruhusu wananchi kwenda kukopa tena katika fedha hizi. Kwa hiyo, makundi haya ni matatu, wanawake, vijana pamoja na wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengine wamesema kwamba wamepeleka kwenye benki. Wananchi wengi hawajui vizuri mfumo wa kwenda kufuata fedha hizi. Ninaomba sana Serikali iweke mfumo rahisi ili wananchi wafikiwe na vikundi hivi viweze kuchukua zile fedha kwa ajili ya kujiwezesha kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo hili kumekuwa na kilio cha akinababa ambao nao wanatuambia kwamba, asilimia 10 mbona haziwagusi? Kwa hiyo, wazee wanalalamika kule kwenye maeneo mengi; wanasema na wao waguswe na fedha hizi kwa sababu wao pia wanatunza familia. Kwa hiyo, leo wakishazaa watoto vijana wakawaacha pale, maana yake wao wanaachwa wanakuwa kama second hand.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wazee wanasema nao waangaliwe ili Mfuko wao uweze kupatikana. Kama hatuna Mfuko wa kuwapa fedha bure, basi wapewe za mkopo ili waweze kuimarika, na kwa hakika wawe na sauti kwenye nyumba kwa sababu akinababa nao wanaona wameachwa nyuma sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaiomba Serikali nayo iende kuangalia upya. Mheshimiwa Rais anawapenda wazee, ambapo kama kweli wazee ni dawa basi wawe na uwezo wa kiuchumi ili waweze kuzisimamia familia zao, wasiwe wanyonge na waondoke kwenye unyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, ninaunga mkono hoja. Ninasema ahsante sana kwa mchango huu. (Makofi)