Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza ninapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema. Ninakupongeza wewe kwa kuendesha Bunge hili Tukufu. Pia, ninapenda kuipongeza Kamati na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametoa hoja zao katika Kamati hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Kamati kwa ushirikiano ambao wanatupa katika Wizara yetu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Tumepokea ushauri wao na tunatekeleza vizuri kwa ushirikiano wanaotupa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru pia,Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na upeo na kuona kuunda Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii. Sasa wananchi wameweza kuona umuhimu wa wizara hii na wananchi wengi wanakuja kutatuliwa changamoto zao za kimaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wametoa hoja mbalimbali ambazo zinawahusu wananchi. Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara yetu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum tunafanya nao kazi vizuri na tuko karibu nao; na sasa hivi tayari utaratibu kuhusu mikopo ya wafanyabiashara wadogo wadogo umeshakamilika, fedha zimeanza kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upendo kwa wananchi wa Tanzania tayari Mheshimiwa Rais ametoa fedha shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kushirikiana na Maafisa wetu wa Maendeleo ya Jamii walioko katika halmashauri zote nchini Tanzania kuhakikisha wananchi wanakwenda NMB na kuchukua vitambulisho vya kielektroniki ili kuhakikisha wanapata mikopo hiyo na kuweza kujiwezesha wenyewe kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeongeza bajeti ya vyuo vyote vya maendeleo ya jamii. Hadi sasa Mheshimiwa Rais ametuwekea fedha za ujenzi, fedha za hostel na fedha ambazo zitasaidia vibali vya ajira ili kuhakikisha kwamba vyuo vyetu vinaendelea vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, shilingi bilioni 12.665 zimewekwa kwa ajili ya kuendesha vyuo hivi. Hii ni fursa nzuri kwa wananchi wetu kuhakikisha wanapata elimu hii ya maendeleo ya jamii ili waweze kujiwezesha wenyewe na pia kuleta maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge hapa, kutorejeshwa fedha tulizozitoa za WDF ambazo tumewapa wananchi mikopo hiyo. Sasa hivi tumeshaunda Kamati ambayo itawawezesha kukusanya fedha hizi na kurejesha na kuwapatia wananchi wengine, ili kuhakikisha fedha hizi zinatoa msaada na wananchi wengine kupokea mikopo kama hii kutoka WDF. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuwezesha na kutuunganisha na mataifa mbalimbali. Hivi karibuni Mheshimiwa Rais ametuunganisha na tumeingia mkataba na Benki ya Dunia kwa zaidi ya shilingi bilioni 248 tumefunga nazo mkataba. Fedha hizi ni kwa ajili ya kuwakopesha wananchi wadogo wadogo hasa wanawake kwa riba nafuu ili kuhakikisha wanawake wetu wanaweza kujiendesha kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake kwa maono yake na upeo wake ambao analenga kwa wananchi wa Tanzania kuhakikisha wanapata fursa wanazozihitaji katika maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu ya mikopo kwa wananchi wote kupitia vyombo vya habari mbalimbali ambavyo vitawafikia wananchi hadi vijijini ili kuhakikisha kuwa wanapata fursa hizi nzuri za mikopo midogo midogo ili waweze kujiwezesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, nia na madhumuni ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wote wanapata fedha hizi na kuondokana na umaskini, matatizo na changamoto zote za maisha ambazo zinawakabili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muda ni mdogo sana. Kutokana na mambo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wamechangia na maelekezo ambayo wametupa, Serikali tutazifanyia kazi hoja zote na maazimio yote ya Kamati ambayo yametolewa hapa na kushirikiana vizuri kuhakikisha Serikali hii inakwenda vizuri kama Mheshimiwa Rais anavyotuelekeza sisi wasaidizi wake kuhakikisha wananchi wote wanakuwa salama na amani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa michango yote ya Kamati na ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wanaotupa. Sisi tuko tayari, mlango yetu Wizara ya Maendeleo ya Jamii iko wazi kuhakikisha tunashirikiana pamoja na wananchi wote. Ahsanteni sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)