Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Siha
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe kwa kutuongoza, lakini nilishukuru Bunge lako Tukufu kwa mambo makubwa ambayo amekuwa akitushauri. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Mwenyekiti wetu wa Kamati kwa kweli na Kamati yetu imekuwa ikituongoza vizuri sana sisi Wizara ya Afya. Niwashukuru pia Viongozi wote wanaotuongoza ndani ya hili Bunge, lakini pia na Chief Whip wetu jinsi ambavyo anatupangilia vizuri katika kucheza mechi ndani ya hili Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliombe Bunge lako kwa sababu ya muda waniazime tafakuri ya kina kwa muda mfupi ili nitumie maneno machache, lakini ili wote kwa pamoja tuweze kumwelewa aina ya Mheshimiwa Rais ambaye tunaye sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaye Mheshimiwa Rais ambaye hafikirii tu kutatua matatizo madogo madogo yanayoibuka ndani ya nchi yetu na matatizo ambayo yanaonekana na watu katika ulimwengu wa damu na nyama, lakini Mheshimiwa Rais huyu anaifikiria Tanzania ya miaka 100 ijayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais huyu anajua kwa nini siri ya tofauti ya Mataifa yenye nguvu na Mataifa maskini; siri ni nini? Mheshimiwa Rais huyu anajua kwamba siri siyo uwepo wa rasilimali na ukubwa wa nchi na mambo mengine, lakini siri ya Mataifa hayo ni uwepo wa watu wenye akili iliyopitiliza upeo wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Rais huyu amejua kwamba leo tupo kwenye dunia ambayo tunazungumzia artificial intelligence ambayo sasa inaanza kupitiliza hata ule uwezo wa akili ya kawaida wa binadamu na Mheshimiwa Rais huyu anajua leo artificial intelligence tunayoiona leo ni suluhu wa mambo mengi inaenda kuunganishwa na quantum computing.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakapounganisha hayo mambo mawili tutakuta tunahitaji binadamu wenye uwezo wa kufikiri kwa namna ya ajabu sana ili na sisi tuweze ku-compete na Mataifa mengine. Mheshimiwa Rais huyu ndiyo maana aliposimama hapa kwa mara ya kwanza alipofika eneo la mama na mtoto alirudia na kuongea kwa pozi ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuishia hapo aliweka resources. Leo ndiyo maana unaona dunia ipo Tanzania siku hii ya leo ikimpa Mheshimiwa Rais wetu nishani kwenye kushusha vifo vya akinamama kuliko ilivyotegemea kutoka 556 mpaka 104 yaani mwaka juzi na ilitegemewa ni mwaka huu. Leo dunia ipo na Gate Foundation na Goalkeepers wapo hapa Tanzania. Hawapo hivyo; matokeo haya yametokana na nini? Yametokana na resources aliyoingiza kwenye huduma ya mama na mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuingiza resources lengo siyo kuokoa vifo vya akinamama na watoto, ndiyo maana unamwona amesaini mkataba na wakuu wa mikoa wa lishe. Mheshimiwa Rais wetu pamoja na kuhudumia huduma ya mama na mtoto anajua ili upate Taifa la watu wenye akili unaanza kumwangalia mtoto toka akiwa tumboni kwa mama yake akiwa ana miaka zero.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake unaingiza resources kuanzia hapo, unaingiza lishe kwenye mama, unaingiza huduma zote ndiyo pale unapokwenda akazaliwa mtoto mwenye ubongo uliojengeka vizuri ambao una uwezo wa kuelewa mambo yaliyopitiliza upeo wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake chakula na mambo mengine huduma zote ndiyo zinatengeneza wiring ya ubongo. Usipotengeneza namna hiyo unakuwa na watu ambao wana ubongo lakini ubongo huo umeme GB chache tu zikiingizwa unaanza kupata moto, lakini ukiwa na ubongo uliojengwa vizuri wenye wiring ya kutosha hata upige GB kubwa kiasi gani una uwezo wa kupokea na kuchakata.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana utaona kwamba kuna wakati mwingine watu wanajua kupokea mdude kitu chochote kizima kizima na kumeza kizima kizima, lakini ubongo uliochakatwa ukipokea chochote unachakata, unameng’enya na unafikiria beyond mwonekano wa macho ya kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndicho Mheshimiwa Rais anataka hizo akili tuzipate Tanzania. Ndiyo maana umemsikia akishazaliwa huyo mtoto sasa mwenye huo ubongo uliojengeka kwa afya nzuri na huduma nzuri za afya na lishe nzuri inahitaji elimu bora; ndiyo maana umemwona Mheshimiwa Rais huyu amewekeza sana kwenye elimu na juzi hapa amezindua mtaala. Anazindua mtaala ambao unakuja ubongo mkubwa; huo mtaala je, una uwezo wa kusisimua huo ubongo mkubwa uweze kufikiria kwa namna ambayo unaweza kuona mambo yasiyoonekana? Ndiyo huyo Mheshimiwa Rais ambaye tunaye, anayetutayarishia Taifa la kesho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kuwaambia Waheshimiwa Wabunge tembeeni kifua mbele kwenye maeneo yote na kwenye eneo la afya na yote mliyoyasema, sisi kama afya tunayachukua. Tumeshamsikia Mheshimiwa Rais alichokisema na tunaenda kutekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa moja tu kwa kuwaambia kwamba mmesema eneo la afya kwa maana ya elimu kwenye afya na utoaji wa elimu. Naombeni Waheshimiwa Wabunge waturuhusu kuendelea kuhakikisha vichwa hivi vizuri ambavyo Mheshimiwa Rais wetu anaanza kuvitengeneza vya miaka 100 ijayo ndiyo vinaingia kwenye taaluma ya afya kwa sababu kwenye afya ukikosewa aidha umekuwa mlemavu au umekufa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sheria ukikosea una uwezo wa kukata rufaa, Mahakama nyingine ikakupa haki, lakini kwenye afya tunasababisha walemavu na mambo mengine. Ni eneo tunalohitaji tupate watu smart sana. Pia, Wabunge watakuwa wamesikia tunapokea watu sasa kutoka nje kuwatibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashindano hayo siyo ya teknolojia tu, mashindano hayo pia ni ya kupata brain nzuri zenye kuweza ku-compete na kufanya mambo kwa namna ambayo watu wengine hawawezi kufanya ndipo tunageuza Taifa letu linakuwa pool la kila mtu kuwa kimbilio lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba waendelee kutukubalia tuendelee kuhakikisha tunaweka tight measurement kuhakikisha watu wanaoingia huko kwenye kutibu watu wanakuja watu ambao tuna uhakika kwamba wana uwezo wa kufanya hayo mambo yanayohusu maisha ya binadamu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuwaambia Mheshimiwa Rais huyu alichokifanya kwenye afya pamoja na ugumu wa bajeti na mambo mengine haijatatua tu matatizo ya Watanzania kwenye eneo la afya, imetatua na matatizo ya majirani zake. Maana yake leo walikuwa Zambia, Rwanda kwingine kote Msumbiji, Comoro mnaona wakisaini mikataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, walikuwa watumie hela nyingi sana kwenda Ulaya na India leo wanakuja hapa karibu Tanzania kupata suluhu ya matatizo yao na fedha nyingine wanazibakiza nchini kwao kutatua matatizo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais huyu ni Mheshimiwa Rais ambaye anatazama beyond measure, ni Mheshimiwa Rais ambaye ameleta suluhu za Tanzania na ameleta suluhu za nje ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, waendelee kutukubalia, waendelee kutuunga mkono, waendelee kumuunga Mheshimiwa Rais wetu huyu mkono, tutembee kifua mbele kwa sababu tupo mikono salama ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na yote ambayo wametuelekeza waliyoyasema sisi kama afya tupo kifua mbele, tuna uhakika 100% yataenda kutekelezeka kwa sababu tuna jemedari wetu Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na Mungu awabariki. (Makofi)