Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. FATMA H. TOUFIQ – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA USTAWI NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuhitimisha hoja yetu. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia ni Waheshimiwa Wabunge sita, lakini pia Waheshimiwa Mawaziri ambao wamechangia ni Waheshimiwa Mawaziri wawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchache labda niwabainishe hao Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia ni Mheshimiwa Msambatavangu, Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mheshimiwa Almas Maige, Mheshimiwa Riziki Lulida, Mheshimiwa Kimei pamoja na Mheshimiwa Miraji Mtaturu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja zilizojitokeza zaidi ni kwamba fedha za machinga kutotolewa kwa muda mrefu na kasi ndogo na pia katika uandikishaji unaosuasua kwa hawa wamachinga. Kwa hiyo kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri wanaendelea kulifanyia kazi na yale maoni ya Kamati tuliyoyatoa wataendelea kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili ilikuwa ni kuhusiana na mikopo ya Mfuko wa Wanawake (WDF) kwamba fedha hizi zinatakiwa zirejeshwe kwa wakati kwani kuna baadhi ya halmashauri zilikopeshwa fedha hizi. Kwa hiyo inabidi zile halmashauri ambazo zimechukua hizi fedha zirudishe ili kusudi kwa sababu ule Mfuko ni revolving ili kusudi wanufaika wengine waweze kupata. Ni budi sasa Wizara ya Maendeleo ya Jamii pamoja na TAMISEMI washirikiane kuhakikisha kwamba fedha hizi zinarudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine iliyojitokeza ni kwamba kwenye suala zima la usimamizi kwenye ile program ya ufanisi wa kukuza ujuzi kwamba katika program ile ambapo inaonyesha kabisa kwamba inabidi Watanzania wengi zaidi waweze kupata fursa hii. Inaonekana napo bado kwenye kukuza ule ujuzi Watanzania wengi hawashiriki. Imeshauriwa kwamba walau ifikie hata 50% ili kusudi Watanzania au wale vijana wanaokuza ujuzi waweze kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo ni kwamba imeshauriwa hawa vijana wanaomaliza kupata yale mafunzo katika kukuza ujuzi waweze kupewa vitendea kazi. Hata hivyo, wameenda mbali zaidi kwamba kwenye hili suala la kukuza ujuzi kwa sababu program hii pia inataka wale wawekezaji wanaokuja hapa nchini waweze kutoa ujuzi kwa wale vijana wa hapa kwetu ili tuweze kupunguza kuleta ma-expatriate au kuleta wataalam kutoka nje. Hii nayo imezungumziwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaomba Serikali ifanyie kazi kwa kuhakikisha kwamba Watanzania wengi na kwa wakati wanapata mafunzo haya ili mwisho wa siku sasa wale vijana waweze kuajirika hapa badala ya kutegemea wale wawekezaji kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limejitokeza ni kwamba waajiriwa na wastaafu kulipwa fdha za michango ya waajiri wao. Yaani kwamba wale wastaafu wanapokuwa wamefikia wakati wa kustaafu, kuna baadhi ya michango yao inakuwa haijaenda kule kwa hiyo kuna baadhi ya wastaafu ilibidi walipe zile fedha ili kusudi waweze kupata zile fedha zao za kustaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo tumelizungumza sana na bahati nzuri Sheria kabisa tumeshaipitisha. Kwa hiyo kuanzia sasa hivi ina maana kwamba mifuko yote hii haitafuatilia iwapo kama mwajiri hajapeleka michango basi wale wanufaika watatakiwa walipwe mafao yao na wakishalipwa mafao yao itabidi sasa mifuko ndiyo iendelee kufuatilia katika hizi halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo limejitokeza ni kwamba inabidi kuwepo na data za kutosha kwa wale wote waliojengewa uwezo kwenye hili suala la kukuza ujuzi. Kwa upande wa OSHA kwamba sera ya usalama na afya mahali pa kazi inatakiwa irejewe upya kwa sababu inaonekana kwamba imepitwa na wakati. Kwa hiyo hii pia imezungumzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba kwenye suala la mifuko wamezungumzia ufanisi wa Mifuko. Ninapenda kusema kwamba, nadhani Serikali ilipofanya revision ya kuona kwamba Mifuko hii fedha zipelekwe benki ili kusudi ziwe salama zaidi baada ya kuonekana kwamba kulikuwa na mianya, niendelee tu kuwashauri Waheshimiwa Wabunge turidhiane na masuala ya Serikali kuona kwamba fedha hizi zipitie benki ili kusudi wanufaika wengi waweze kupata hasa wale wanaostahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri ambao wamechangia hoja. Pia, kwa namna ya kipekee nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha kwamba ustawi na maendeleo ya Watanzania yanapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.