Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Singida Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ELIBARIKI I. KINGU – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA AFYA NA MASUALA YA UKIMWI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kukushukuru wewe binafsi kwa kutupa muda sisi Kamati ya Afya na Masuala ya UKIMWI kutoa taarifa yetu ya utekelezaji wa shughuli za Kamati kwa mwaka 2024/2025 ambayo imeishia Januari, 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, sitakuwa na mengi sana ya kusema, lakini naomba niweke kumbukumbu vizuri. Mwanzo niliteleza kwa kusema kwamba Mheshimiwa Rais tuzo anayopokea leo siyo ya kupunguza vifo vya watoto ni vifo vya kina mama kutoka vifo 556 mpaka vifo 104.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi malengo yaliyokuwa yamewekwa na WHO yalikuwa ni kufikia vifo 225 kwa hiyo Tanzania Mheshimiwa Rais wetu na Serikali wamekwenda beyond kwa hiyo hatuna sababu ya kuacha kuwapongeza katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wamechangia wachangiaji wengi. Wengi wameunga mkono mapendekezo na ushauri uliotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, wengi wameunga mapendekezo kwa mfano pendekezo la kuiomba Serikali ya kuitaka Serikali iweze kutoa mtaji wa zaidi ya shilingi bilioni 460 kwa Medical Stores Department ili kuwawezesha kufanya uwekezaji, ununuzi, uhifadhi na usambazi wa madawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, amechangia Mheshimiwa Sanga, ameshindilia kwenye hilo na Mheshimiwa Jacqueline ameshindilia kwenye hilo. Pia, amechangia Mheshimiwa Mwandabila amezungumzia masuala ya kuhakikisha kwamba tuwe na hospitali mbadala.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiona hapo kubwa ni kuiomba Serikali iendelee kufanya uwekezaji kwa hospitali zetu za ndani kwa kufanya public private partnership. Kwa mfano tulizungumza hata kwenye Kamati yetu hivi karibuni tunayo hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre ambayo tuliishauri Serikali waingie nayo ubia badala ya kwenda kuwekeza kujenga majengo mapya, wanaweza kuingia ubia wakapeleka vifaatiba, mitaji na mambo mengine shughuli zikaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hoja ya Mheshimiwa Mwandabila inaweza kuwa solved kwa kuhakikisha kwamba Serikali inaendelea kuwekeza katika hospitali zetu za ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mama Mushashu ninampongeza pia mama yangu na Mjumbe wa Kamati ametoa sifa na pongezi kwa Serikali, lakini pia ameomba Kagera wajengewe centre kwa ajili ya karantini kutokana na wingi wa milipuko ya magonjwa. Hilo jambo pia nafikiri ninaliafiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, bima ya afya kwa wote watu wameendelea kusema elimu ya umma iendelee kutolewa na Mheshimiwa Mtaturu kaka yangu amempongeza Mheshimiwa Rais na pia ameomba mtaji kwa MSD wapewe. Amewapongeza watu wa NHIF kwa kuongeza mapato, lakini amesisitiza watu wa NHIF waimarishe mifumo yao ya huduma ili kuhakikisha kwamba ubadhirifu na upotevu wa fedha za Serikali zinazopotea uweze kudhibitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikiri kwa kifupi sana pamoja na changamoto nyingi ambazo kama Kamati tunaziona zipo nikiri Serikali wanafanya kazi kubwa sana katika Sekta ya Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hata takwimu zinaonyesha; kwa mfano mpaka mwaka jana tumeweza kupata wageni kutoka nje ya nchi ambao jambo hili lilikuwa geni kwa nchi yetu, zaidi ya watu 11,332 wametoka nje ya nchi wamekuja kutibiwa Tanzania. Vifaatiba vya kisasa, tumekuwa na digital x-ray, tumekuwa na mashine za MRI, tumekuwa na mashine digital za ultra sound vitu ambavyo mwanszo vilikuwa ni hadithi kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatuna sababu ya kuendelea kuiunga mkono Serikali na pale ambapo Bunge tutapaswa kuishauri na kuona kwamba kuna mambo hayaendi vizuri hatutapepesa jicho kuiambia Serikali lakini pale itakapofanya vizuri tutaendelea kuipongeza ili kuwatia moyo waendelee kuwahudumia Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ninakushukuru sana wewe binafsi, ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru tena kwa mara ya pili, ahsante sana kwa kutupa nafasi. Baada ya kusema hayo ninatoa hoja ahsanteni sana.