Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii nami niweze kuchangia taarifa mbili za Kamati ambazo leo zimewasilishwa ndani ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na Taarifa ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Naungana na Wajumbe wa Kamati hii ya NUU kwanza kumpongeza sana Mwenyekiti wa Kamati ya NUU, Mheshimiwa Vita Rashid Mfaume Kawawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Kawawa anafanya kazi nzuri sana, ni kiongozi makini. Natuma salamu kwa wananchi wa Jimbo la Namtumbo kwamba, tunatamani Mheshimiwa Kawawa aendelee kuwepo ndani ya Bunge lako Tukufu. Sisi tunamwamini sana Mheshimiwa Vita Kawawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salamu hizo kwa wananchi wa Jimbo la Namtumbo, naomba sasa pia nitumie nafasi hii kuvipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, nikianza na Ofisi ya DGIS, IGP, CGP, CGF pia CDF kwa kazi nzuri ambazo wanafanya kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa letu limekuwa na utulivu mkubwa sana, na haya mambo hayatokei kwa bahati mbaya. Tumekuwa na mikutano mingi sana hapa nchini ambayo imekuwa na wageni wengi mbalimbali kutoka Afrika na nje ya Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na mkutano mkubwa sana mwaka 2003 ambao ni mkutano wa Kilimo na Chakula, ulikuwa na wageni zaidi ya 3,000, hakuna mtu hata mmoja aliyeondoka hapa akiwa na hali mbaya ya kiusalama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na Mkutano mkubwa sana wa Nishati mwaka huu ambao ni Energy Summit Mission 300 ya mwaka huu. Tumekuwa na wageni wengi na Marais wengi wa Afrika; na wageni wetu wote wameondoka salama Tanzania, kwa sababu ya kazi nzuri ya vyombo vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumekuwa na Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi zaidi ya 5,000 katika Mkoa wa Dodoma, waliokuja kwa kishindo kumpitisha Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa Urais. Tumeshuhudia Dodoma imekuwa shwari, hakuna aliyepoteza simu wala shati, wameondoka salama. Hongera sana vyombo vya ulinzi na usalama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kazi nzuri ya kuimarisha diplomasia ya Kimataifa. Yamesemwa mambo mengi hapa, na wahenga wanasema, mwenye macho haambiwi tazama. Watoto wa mjini pia wanasema kama huwezi kusoma, angalia picha; kama huwezi kuangalia picha, basi unaweza ukanusa hata ukasikia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama takwimu na heshima ya nchi ambayo sasa dunia wanaitazama, hakuna mashaka kama Mheshimiwa Rais amejenga diplomasia kubwa sana duniani kwa ajili ya Taifa letu. Wale ambao pengine hawafuatilii, ukitazama kwenye sekta ya utalii, kwa mfano kutoka mwaka 2021 Mheshimiwa Rais, amefanikiwa kuongeza watalii kutoka Mataifa mbalimbali, kutoka 922,000 mpaka 2,140,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii maana yake nini? Ni kwamba diplomasia yetu inazidi kuimarika na Taifa letu linazidi kuwa na taswira nzuri duniani. Mheshimiwa Rais, hongera sana kwa kazi nzuri ambayo unaifanya kwa ajili ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitumie nafasi hii kusema kwamba, kwa wakati huu ambao tunaelekea kwenye uchaguzi na wakati huu ambao nchi yetu itakwenda kuwa na masuala mbalimbali ya kuongeza ulinzi na usalama katika ukanda huu wa Maziwa Makuu, tumeona hapa ndani vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vimeongezewa magari mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitazama Askari wetu sasa hivi huko barabarani wanayo magari mazuri, wanakaa kwa amani na hii ni kuongeza ulinzi wa raia na mali zao. Mheshimiwa Rais hongera, lakini pia Mawaziri wote; Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wetu wa Ulinzi na Jeshi la Kujeta Taifa, Waziri wa Mambo ya Nje, hongereni sana kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa kazi mbalimbali za Wizara hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye hii Sekta ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama, nitumie nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais, kwani wananchi wangu wa Kata ya Mtwango, Kata ya Kichiwa, Kata ya Igongolo, Ikuna na Ninga walikuwa na kero ya Kituo cha Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazo taarifa njema kwamba Mheshimiwa Rais, ametupatia zaidi ya shilingi milioni 250 kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi pale Mtwango, ahsante sana Mheshimiwa Rais. Sasa kata hizi zitakuwa na usalama mwingi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba niingie kwenye Sekta ya Kilimo kwa maana ya Biashara na Viwanda, Kilimo na Mifugo. Hapa pia namshukuru sana Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, Kaka yangu, ahsante sana kwa taarifa nzuri. Nasi wananchi, hasa wakulima wa chai, mmetutendea haki sana, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijikite kwenye ukurasa wa 81 kwenye Taarifa ya Kamati hii ya Biashara na Viwanda, Kilimo na Mifugo. Kuhusu tasnia ya chai nchini, kwanza naunga mkono kwamba zao la chai hapa nchini kama ambavyo taarifa imesema, limeenda likidorora siku hadi siku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu zipo kazi na juhudi nzuri ambazo Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amezifanya, na ninaungana kabisa na kauli ya Mheshimiwa Dkt. Chaya, aliyesema kama Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe is very strategic, very innovative, very focused, nami naongeza kusema kuwa Mheshimiwa Bashe is very bold, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, sifa zote hizi unastahili na amefanya kazi nzuri. Kule Lupembe alitoa maelekezo kwamba wananchi wa AMCOS ya Lwafi na Ikami waende kwa sehemu ya kiwanda cha kule Kabambe. Nataka nitoe taarifa kwa Mheshimiwa Waziri Bashe, kwamba wananchi wale sasa wameshaingizwa rasmi kwenye huu mradi na wanaanza kupata pembejeo na mafunzo ya ugani. Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, Mheshimiwa Waziri, alitoa maelekezo ya msingi sana kwamba kile kiwanda cha wananchi wa Lupembe kirejeshwe kwa wakulima wa Lupembe. Uamuzi ule ulienda vizuri, uhakiki ukafanyika, lakini mpaka leo kile kiwanda hatujajua nini kimekwamisha kurejeshwa rasmi kwa wananchi wa Lupembe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Lupembe wamenituma kwamba, pamoja na kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Waziri anaifanya, kwa sababu kila alikoenda kwenye zao la korosho, kwenye zao la pamba umetatua na changamoto zile, na zimeenda zikiisha, wanaomba baada ya Bunge hili afike Lupembe kuona kazi nzuri ambayo ameanza kuifanya aikamilishe, chai ipate soko zuri hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wale watu wa kampuni ya LIPTON au NOSCI ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa wakulima wa chai Lupembe, licha kwamba chai sasa hivi inachukuliwa kwa mgao ndani ya wiki mara mbili mbili, hawa ni wadau muhimu sana. Mwaka 2024 wamesaidia kulipia wakulima certificate ya Kilimo ili wakauze mazao yao ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tena zipo kata kadhaa, kata kama ya Lupembe, Matembwe, na Ukalawa. Hawa wote watahitaji tena kufanyiwa certification kwa ajili ya mazao yao. Naiomba Serikali, kwa sababu huyu ni mdau, anasaidia wakulima, apewe ushirikiano akomboe wananchi wa Lupembe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sifa alizonazo na uwezo alionao, wananchi wa Lupembe wanachuma chai, lakini wanaelekea kukata tamaa. Tusipochukua hatua, zao hili linaweza kwenda kufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono kwamba vile viwanda kama vya Ikanga, Kiwanda cha Kibena ambacho DL ameshindwa kukiendesha, Serikali ichukue hatua viwanda hivi, vichukuliwe wapate wawekezaji wengine ili wawasaidie wakulima wetu wa chai Mkoa wa Njombe na nchi yetu kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, Mheshimiwa Waziri nashukuru sana, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)