Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kupata nafasi hii kuchangia taarifa ya Kamati zetu hizi mbili ambazo zimewasilishwa hii leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda nichukue nafasi hii kutoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ambayo anaifanya. Pia napenda kuchukua nafasi hii nimpongeze kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi kuwa mgombea wa kuipeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi wa mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza katika safari moja na Mheshimiwa Rais. Vilevile sitasahau kumpongeza Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti, ndugu yetu Mheshimiwa Wasira naye kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi kwa vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama. Vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama vinafanya kazi kubwa ya kulinda nchi yetu, tunaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile nimpongeze Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuitunza amani ya nchi yetu Tanzania, pamoja na kujitahidi kuhakikisha kwamba majirani zetu nao wanakuwa na amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni anaendelea kupambana kuhakikisha kwamba amani ya Congo inapatikana kwa kuitisha mikutano na viongozi wenzake ili hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iweze kuimarika. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nilipongeze Jeshi letu la Polisi kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kwa kweli nchi imetulia, watu na mali zao wametulia kwa sababu Jeshi letu linafanya kazi usiku na mchana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto nyingi ambazo zimejitokeza, changamoto za vifaa ni ukweli usiopingika, Polisi wanafanya kazi kubwa, lakini vifaa ni vichache. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali walitupie macho Jeshi la Polisi kwa ajili ya vifaa vitakavyowawezesha kufanya kazi zao kwa weledi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi linajitahidi, linakusanya fedha za tuzo na tozo, tunaona vituo vya Polisi vinajengwa, kwa kweli wanajitahidi sana, lazima tuwape maua yao. Ni kazi nzuri ambayo wanaifanyia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi katika hali ya usalama. Jeshi la Polisi na hasa usalama wa barabarani, ni kweli ajali nyingi za barabarani zimeendelea kupungua siku hadi siku kutokana na kazi kubwa ambayo Jeshi la Polisi linaifanya, lakini bado Serikali ina jukumu kubwa sana la kulisaidia jeshi hili kupata vifaa kuachana na Habari ya traffic ambao wengi wanakaa barabarani na hatimaye wanapata kashifa nyingi kwa ajili ya kuchukua chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watafute vifaa, kwa mfano sasa hivi kuna changamoto kubwa barabarani huko, watu wana-overtake ovyo, lakini kama wangekuwa na camera sehemu zote za barabara ingesaidia sana Polisi hawa kupata nafuu katika ufanyaji wa kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka kuligusia ni bodaboda. Unatambua kuwa zaidi ya 60% katika nchi yetu usafiri wa bodaboda unategemewa sana na watu, lakini bodaboda hawa wanaishi katika mazingira ambayo siyo sahihi. Bodaboda hawa hawatambuliki. Tunaiomba Serikali ianzishe mfumo maalumu sasa hivi wa kuwatambua bodaboda kwa ajili ya usalama wao pamoja na usalama wa abiria ambao wanawachukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii bodaboda anaweza akatokea kituoni hajulikani, akafika pale akafanya jambo lolote la kihalifu, akawaponza bodaboda wenzake, wakaingia katika matatatizo kwa sababu tu hakuna utambuzi sahihi katika hivi vituo vya bodaboda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Jeshi la Polisi pamoja na Serikali ihakikishe kwamba bodaboda wanapata utambuzi ili waweze kufanya kazi zao vizuri kwa sababu ni watu ambao ni wengi sana katika nchi yetu, wanatusaidia sana sisi wengine katika suala zima la usafiri mijini pamoja vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala moja ambalo amezungumzia mjumbe mwenzangu kuhusu deni ambalo SUMA JKT wanadai. Mheshimiwa Mjumbe mwenzagu aliyepita alizungumza kwamba SUMA JKT wanadai zaidi ya shilingi bilioni 40 katika taasisi mbalimbali, katika Mawizara. Hebu Taasisi na Wizara zilipe SUMA JKT hizi shilingi bilioni 40 ili mipango yao iweze kuendelea vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika taarifa yao, SUMA JKT wamekwama kuanzisha kiwanda cha kutengeneza madawa, kutengeneza vifaatiba pamoja na kutengeneza mbolea kwa sababu tu hawana fedha. Kama wangelipwa hizi shilingi bilioni 40, mimi nafikiri kiwanda hiki kingeanzishwa vilevile na vijana wetu wengi wangepata ajira katika hii taasisi yetu ya SUMA JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli naomba niwasihi sana, Serikali pamoja na Wizara wajitahidi hata katika bajeti ya mwaka ujao, walipe hizi fedha ili SUMA JKT iweze kuwaajiri vijana wetu waweze kupata kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii pia kulipongeza Jeshi letu la Zimamoto kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Kama unavyojua, Jeshi hili bado lina tatizo la vifaa, lakini juzi juzi, mnakumbuka Dar es Salaam umetokea moto, baada ya kupatikana gari refu la kuzima moto juu ya magorofa, Jeshi la Zimamoto limeweza kudhibiti moto ambao ungeweza kuharibu gorofa zima lile. Kwa hiyo, tunaomba vifaa hivi viweze kununuliwa kwa wingi ili jeshi letu liweze kufanya kazi zake kwa weledi zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa, tunaambiwa kuna karibu vituo vya Zimamoto 157 nchini bado havina vifaa vya kutosha. Kwa hiyo tunaiomba Serikali iangalie kwa umakini, kutokana na vifaa hivi vya Jeshi la Zimamoto, wawape vifaa madhubuti ili waweze kuzima moto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana wanakamati wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na Mwenyekiti kwa taarifa nzuri, na niwapongeze sana Mwenyekiti wa Kamati ya Kilimo, Biashara na Viwanda kwa taarifa yao nzuri. Kazi ni nzuri ambayo wanaifanya Wenyeviti wetu pamoja na Wajumbe wa hizi Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nakushukuru sana, naomba kuwasilisha. (Makofi)