Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi niweze kuchangia na kunipatia nafasi kuwa wa kwanza kuchangia taarifa za hizi Kamati mbili; ya Ardhi pamoja na Maji.

Mheshimiwa Spika, kabla sijasema chochote, kwanza nitumie nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati sana kwa Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi kwa kutujaalia afya pamoja na uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hili tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa sisi Wabunge kuwa na afya na uzima, lakini ziada ni kwako Mwenyezi Mungu kuendelea kukupatia afya njema pamoja na uzima na kuendelea kutusimamia sisi Waheshimiwa Wabunge katika muda wote ambao tupo hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ziada nitoe pongezi zangu kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Kibamba kwa Viongozi wetu watatu wa Kitaifa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu wetu Maalum kuwa wagombea kwenye nafasi zao kwa uchaguzi wa 2025/2030, hasa kwa Dkt. Balozi Emmanuel John Nchimbi kuteuliwa na Chama chetu kuwa Mgombea wa nafasi ya Makamu wa Rais. Hawa wengine wanaendelea na nafasi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama Mjumbe wa ule Mkutano Maalum, ninaamini nilitenda haki kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Kibamba kuwachagua wote hawa watatu kwa kura ya Ndiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi zangu hizo, nizungumzie maeneo mawili; la maji na hilo la ardhi. Hili la maji, moja kubwa ni mafanikio makubwa ambayo yamepatikana katika kipindi chote hiki cha miaka minne na miezi kama mitatu ya Chama chetu katika Ilani ya Uchaguzi ya 2020/2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba mimi kama Mbunge wa Jimbo la Kibamba ninaendelea kutoa shukrani zangu za dhati sana kwa jemedari wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Awamu ya Sita pamoja na viongozi wote wa Wizara wakiongozwa na mdogo wangu Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso, kwa kufanya kazi nzuri sana kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, katika muda wote nikisimama humu mwanzoni, nimekuwa nikisema kidogo kwa ukali juu ya changamoto kubwa ya maji ambayo toka ninaingia ilikuwa chini ya 40% au 30%, lakini leo ni ukweli tumeshafika zaidi ya 85%. Shukrani zangu hizi zipo wazi tu kwamba wananchi walio wengi sasa wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, miradi mitatu mikubwa ya Wizara hii imeweza kuifanya kwenye Jimbo la Kibamba mikubwa kabisa. Mradi wa Tegeta A, tenki la ujazo wa lita 5,500,000. Ndani ya ujenzi wa takribani matenki makubwa matatu kwenye Mradi wa Changanyike - Bagamoyo, mradi ambao umetumia zaidi ya shilingi bilioni 64 za Benki ya Dunia. Kwa hiyo, sisi wananchi wa Jimbo la Kibamba eneo la Tegeta A, Goba na Goba nzima na viunga vyake sehemu kubwa wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tenki la pili, ni pale Mshikamano. Nimekuwepo humu, ndani ya mwaka 2021, fedha zile za UVIKO Mheshimiwa Rais, akatoa shilingi bilioni 4.8; Shilingi bilioni 2.5 fedha za ndani na shilingi bilioni 2.4 fedha za UVIKO kujenga lile tenki kubwa la ujazo wa lita 6,000,000 pale Mbezi. Leo wananchi wengi wanapata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni ukweli kwamba sasa hivi Mheshimiwa Rais anatekeleza mradi wa shilingi bilioni 42 chini ya Benki ya Dunia pale Pangulo ambao utawasaidia wananchi wengi wa Dar es Salaam ya Kusini ambao kwangu ni kule Mpakani, Msingwa, maeneo ya King’azi A na B, maeneo ya Kipera, Kwembe na maeneo mengine ya Malamba Mawili, Msigani. Sasa tenki limekamilika.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, juzi nilimwona kule na akatutaja Wabunge wahusika kwenye mradi ule na sasa wanaenda kwenye usambazaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na miradi niliyoisema hii, au mafanikio yetu ya Serikali yetu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwenye sekta ya maji, tunakubali changamoto bado ipo na changamoto kubwa ni usambazaji wa maji kwa muda mrefu kwenye haya matenki ambayo yametimia. Wananchi wanashaanga tu bado, kwa nini, hawayaoni wakati matenki yana maji.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuwaomba, yapo maeneo yamepelekwa mabomba, lakini hawajazamisha ndani. Yatoke maelekezo kwa sababu mabomba yale yanaibiwa, na wananchi wanashindwa kuelewa, hasa maeneo ya Mbezi, Torino, Kwa Mvungi, CCM ya Zamani Mpiji Magoe na maeneo machache mengine sehemu ya Jimbo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nawaomba sana Wizara itoe maelekezo mabomba ambayo wameyaleta jimboni yazamishwe ndani ili wananchi waone kweli yameletwa kwa ajili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia changamoto nyingine ambayo nataka wananchi wajue, ni kwamba leo tunatumia chanzo cha Ruvu Juu. Ruvu Juu ndiyo inalisha Dar es Salaam na upande wetu huo Ruvu Chini inalisha upande wa Jimbo la Kawe na maeneo ya mjini. Ni ukweli chanzo kile ni toka tunapata uhuru. Wananchi lazima wajue chanzo hakijawahi kubadilika, chanzo ni kile kile, na leo tunatengeneza tu vihifadhia maji. Kwa hiyo, nyakati kame ni kweli lazima tutakutana na upungufu wa uzalishaji wa maji kwenye vyanzo vyetu vikuu.

Mheshimiwa Spika, naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita katika kuliona hili, kwenye long term imekuja na Bwawa la Kidunda. Sijaliona kwenye taarifa inasemwa vizuri, lakini mradi unaoendelea na upo zaidi ya 46%. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili bwawa ndiyo litakuwa ukombozi wa Morogoro na Dar es Salaam au Pwani kwa maana ya muda wote sasa kuwa na chanzo kinachotosheleza. Kwa hiyo, wananchi waendelee kuwa na subira kama walivyokuwa na subira nyakati za nyuma.

Mheshimiwa Spika, leo tumekuwa na vihifadhia maji kwenye maji machache yanayozalishwa, na tunaweza kuwapeleka walio wachache, wachache bado kweli hawayapati maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, siyo muda mrefu, hii ni awamu ya kwanza inakamilika. Mheshimiwa Mbunge Mtemvu, anamaliza, lakini ni imani yangu kwamba watanichagua tena kwa kura nyingi sana. Huu ni ukweli ambao nitaenda kukamilisha haya kwa sababu madirisha na milango ninaijua. Kwa hiyo, hilo lipo wazi na wenyewe wanaokuja wanajua, hili lipo vizuri sana kwa Mheshimiwa Mbunge Mtemvu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo jambo la pili, ni jambo la migogoro ya ardhi. Hili nimekuwa nikilisema sana hata nikichangia kwenye Wizara za kisekta, lakini ukweli migogoro mingi imetatulika. Kuna maeneo machache sana ya mipaka haijasemwa sana kwenye Kamati, lakini kuna maeneo ambayo yanaingiliana, Wilaya ya Ubungo na Wilaya ya Kinondoni. Ule ambao tulikuwa nao Kisarawe na Ubungo imetatuliwa, na nitoe pongezi sana kwa viongozi wote wa Serikali Kuu wanaokuja na kupishana, kwa maana ya Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tunayo maeneo mawili ndani ya Ubungo na Kinondoni, moja ni eneo la Mpiji Magoe na Mabwepande kwa maana ya eneo ya Kibesa na Mabwepande eneo linaitwa Mji Mpya tukamilishe huu mgogoro Wizara mtusaidie kutatua.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni kule Msumi na Mbopo mtusaidie, kuna migogoro mikubwa na watu wanaumizana kwa sababu ya kutojua GN pale inasema nini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa ambalo mara nyingi nimekuwa nikilisema hapa ni mgogoro wa Shamba la Malolo (Malolo Farm). Nimewahi kulitolea historia yake jinsi lilivyopatikana, lakini lilikuwa chini ya DDC toka mwaka 1989 na hati wanayo, lakini wananchi wengi zaidi ya 70,000 wameingia humu.

Mheshimiwa Spika, nimewahi kueleza kwa historia kubwa sana na juzi Mheshimiwa Naibu Waziri ameniambia vizuri juu ya jambo hili. Nimtakie kila la heri ndugu yangu Mheshimiwa Ndejembi, akalimalize hili jambo kwenye Wilaya zetu hizi mbili ili wananchi waendelee kupimiwa ardhi wapate hati na mambo mengine ya kujiinua kiuchumi yaweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku ya leo sina maneno mengi zaidi, niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na wateule wote wale. Sisi ni ahadi yetu kwao kwamba hatuwadai, zaidi wanatudai sisi.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Kibamba wataenda kuonyesha jinsi gani ya kurudisha fadhila kubwa kwa kura nyingi sana kwa Wagombea wote Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais na Mbunge wao, Mheshimiwa Issa Bin Jumanne Mtemvu, kwenye Jimbo la Kibamba.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi. (Makofi)