Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Kangi Alphaxard Lugola

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwibara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ALPHAXARD K. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina kila sababu ya kumpongeza Waziri Profesa Sospeter Muhongo na Naibu wake Mheshimiwa Kalemani kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha nchi yetu inapata umeme. Aidha, nawapongeza kwa usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini, nawatakia kila la kheri chapeni kazi bila wasiwasi kwani Wabunge tuko nyuma yenu kuhakikisha mnakuwa katika mazingira rafiki ya kufanya kazi. Pia nawapongeza kwa kuwasilisha bajeti nzuri yenye kuleta matumaini kwa Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali juu ya mpango wa umeme vijijini unaotekelezwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Yapo maeneo hapa nchini ambayo yana changamoto kubwa sana katika usambazaji wa umeme. Maeneo hayo ni yale ya visiwa vingi ambavyo viko katika maziwa na bahari.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwamba ili kupunguza gharama za kutumia marine cable kupeleka umeme katika visiwa, basi REA wasambaze umeme huo kwa njia ya solar (umeme jua) Jimboni kwangu nina visiwa katika Ziwa Victoria vya Nafuba, Sozia, Namuguma, Machwela, Rwiga, Buyanza, Kwigali, Bwenyi na Nyakalango.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa shughuli kubwa za kiuchumi katika visiwa hivi ni uvuvi, umeme huu utasaidia sana kuhifadhia mazao ya samaki pamoja na viwanda vidogovidogo vya kuchakata samaki na kutengenezea boti na mitumbwi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache, naunga mkono hoja. Ahsante.