Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buhigwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, nami kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii. Awali ya yote, nami niungane na wachangiaji wengine ambao mmeshatangulia kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupitishwa na Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa 100% kuwa Mgombea wa Urais, hongera sana Mama.
Mheshimiwa Spika, vile vile nampongeza na mteule, Mgombea Mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi. Hakika anatosha sana. Nimpongeze na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hussein Mwinyi naye kwa kupata zaidi ya 98% ya kura kuwa mgombea wa Urais Zanzibar, hongereni sana.
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizi, sasa nawapongeza kwanza Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati yangu ya Maji na Mazingira na Mheshimiwa Makamu wake kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Sambamba na hilo, nawapongeza Wizara zote mbili ambazo tumekuwa tukishirikiana nazo tangu Januari, 2024 hadi leo Januari, 2025 nikianza na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutupa Waziri wa Maji kijana na Makamu wa Wizara ya Maji kijana Mheshimiwa Aweso na Mheshimiwa Eng. Kundo, hongereni sana. Waheshimiwa Mawaziri hawa ni wasikivu mwanzo mwisho. Hutusikiliza, hupokea maoni na haya kwa ushirikiano mzuri na Wizara ndiyo yamechangia katika utendaji wao na maendeleo yanaonekana. Mwenye macho haambiwi tazama, miradi ya maji imesambaa katika nchi nzima, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi, niende kwenye Wizara ya Makamu wa Rais inayosimamia mazingira. Tunawashukuru kwa juhudi kubwa ambayo wameifanya hasa kwenye biashara ya carbon na ndipo mchango wangu utakapojikita.
Mheshimiwa Spika, biashara ya carbon ni fursa, ni chanzo kipya cha mapato ambacho kama tukikisimamia vizuri, kinaweza kikaleta mapato makubwa sana kwa nchi yetu na katika Halmashauri zetu na katika vijiji vyetu. 32% ya nchi yetu ipo chini ya hifadhi za misitu na mbuga za Taifa. Biashara hii ni biashara ngeni, lakini inaonyesha kama tukiisimamia kwa umadhubuti kabisa, tunaweza tukapata pato kubwa sana. Mathalani tumeona mwaka 2024, halmashauri moja tu ya Tanganyika iliweza kupata zaidi ya shilingi bilioni 14. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa biashara hii kwetu hapa nchini ni ngeni, bado inahitaji tuone namna ambavyo tutaiendesha. Tunazo kampuni za ndani na za nje, lakini kampuni zetu, kwa wale ambao wana-deal na biashara hii, ambao ni wazawa kwenye biashara hii, wanafanya kazi kama middle man. Bado hatujawa na makampuni makubwa kutoka ndani ambayo yanaweza yakafikia masoko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunashauri sisi kama wanakamati, Wizara ijipange namna ya kusimamia suala hili muhimu sana ili makampuni yetu ya ndani, na kwa sababu itaongeza ajira na mapato kwa nchi, basi waweze kufikia masoko ya nje wao wenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekuwa ikisimamia mazingira kwa muda mrefu na tunaona jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ametuzawadia fursa nyingi, na rasilimali nyingi. Tunayo bahari, tunayo maziwa, tunayo misitu, tunayo mito. Haya yote yametengeneza mazingira mazuri ya nchi yetu. Tunalo Baraza la Mazingira ambalo limekuwa likisimamia juu ya uhifadhi wa mazingira.
Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwa fursa na rasilimali tulizonazo, wenzetu majirani zetu wameshasonga mbele. Sasa ni wakati ambao sasa tunatakiwa twende kwenye sheria yetu Na. 191 ya Mazingira ibadilishwe, ifanyiwe amendment ili iwezeshe Baraza la Mazingira kubadilika kuwa mamlaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuwe na Sheria ambayo sasa itaenda kusimamia Sera ya Mazingira ya 2022 na Sera ya Uchumi wa Buluu 2024 pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ya pili ya mchango wangu kwenye Wizara ya Maji, niwapongeze sana, nimeshawapongeza, lakini cha zaidi nisisitize Wizara imefanya kazi moja nzuri, kubwa sana na tunaona ina changamoto ya upatikanaji wa fedha. Nawapongeza kwa kutafuta vyanzo vingine vya fedha hasa kwa kuanzisha Hati Fungani ambao mfano wake ni Tanga – UWASA.
Mheshimiwa Spika, mfano huu wa Tanga – UWASA ambao walipata shilingi bilioni 53 kwenye green bond yao na wakaiuza na wakapata shilingi bilioni 54, ambayo ni chanzo kipya kabisa ambacho kinaweza kikasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maji bila kutegemea Mfuko Mkuu wa Serikali. Huu ni mfano mzuri na tunaiomba sasa Serikali isaidie mamlaka nyingine za maji ili ziingie kwenye matumizi, ziwezeshwe namna ya kuingia kutumia Hati Fungani ili kuweza kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache, naomba niunge mkono hoja kwa Kamati zote mbili, ahsante. (Makofi)