Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia mada iliyopo Mezani. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai, na leo tuko hapa Bungeni. Napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuchaguliwa kuwa mgombea pekee wa Chama cha Mapinduzi. Pia, nampongeza Mgombea Mwenza, Mheshimiwa Balozi Dkt. Nchimbi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda nirudie kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kupata tuzo ambayo inaitwa The Gates Goal Keeper Award, ambayo ni tuzo pekee iliyotolewa kwa huku Afrika. Hongera sana kwake Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Mawaziri wote wa sekta zote, Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Dkt. Pindi Chana, pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Kitandula, pia Wizara ya Ardhi, Mheshimiwa Ndejembi, pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Geofrey Pinda, pamoja na watendaji wote wa Wizara zote, Maliasili na Ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, ninayo mambo ya kuchangia. Tumeona jinsi gani Royal Tour ambayo ilifanyika Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais, ilivyoweza kuleta watalii wengi nchini Tanzania. Tumekuwa na watalii wengi, wamependa kuja Tanzania kwa sababu Mheshimiwa Rais ameitangaza nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tatizo lililopo ni ukosefu wa vitanda, nikiwa na maana ya malazi. Malazi siyo ya kutosha nchini Tanzania, hasa kwenye mbuga zetu. Hivyo basi, inasababisha ukosefu wa vyumba vya kutosha, hasa kwenye mbuga zetu ambazo watalii wanapenda kwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Serikali ilibinafsisha hoteli takribani 23 nchini Tanzania, mwaka 1992, ilipokuwa na Sera ya Ubinafsishaji. Katika hoteli hizo, hoteli 17 zilikuwa zinamilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa hiyo, utaona ni jinsi gani hoteli hizo zingekuwa bado zinamilikiwa na Wizara hii, zingeweza kuisaidia nchi yetu kupata malazi kwa wageni ambao wameongezeka sasa hivi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika maazimio ya Kamati, azimio mojawapo ni kurudisha hoteli ambazo zilibinafsishwa kwa wabinafsishaji ambao hawajatekeleza masharti ya ubinafsishaji. Hoteli hizo ni nyingi.
Mheshimiwa Spika, ziko hoteli pamoja na lodge ambazo ziko mbugani, na nyingine kama vile ziko Serengeti, ziko Ngorongoro, na pia nyingine ziko Dar es Salaam. Mfano, Hoteli ya Embassy haijafanya kazi toka mwaka 2008. Takribani miaka 17, moja kwa moja unaona kwamba mwekezaji huyu hawezi kujenga tena hiyo hoteli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo, sioni haja ni kwa nini Serikali inashindwa kuzirudisha hoteli hizi mikononi mwake kwa sababu, moja kwa moja, hata kama una nyumba yako, mpangaji akishindwa kukulipa kodi, nadhani unachukua jukumu la kumtoa kwenye nyumba yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii ni suala la kuboresha miundombinu iliyoko kwenye hifadhi zetu, ambazo wageni wanakwenda. Ukifika kule Serengeti kipindi cha mvua zinapokuwa zinanyesha, madaraja yale ni madogo, miundombinu ni mibovu.
Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali iongeze bajeti, lakini iweze kufikiria sula la kuboresha miundombinu yetu iliyoko kwenye uhifadhi ili wageni wetu wanapokuja wasikwame kipindi cha mvua. Wizara ya Maliasili na Utalii inao uwezo wa kuingiza watalii wengi nchini, kama itarekebisha miundombinu kwenye hifadhi zote, lakini pia kama itaongeza vitanda vya malazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Wizara ya Ardhi. Wizara ya Ardhi imefanya kazi katika kuhakikisa wananchi wanapata milki kwenye baadhi ya maeneo. Wizara ya Ardhi ilijenga mfumo wa kuwawezesha wananchi kupata bili zao kwenye simu. Mfumo huu haujafanya kazi vizuri, na iko kwenye Maazimio ya Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mfumo huu umefanya kazi kwa 10% tu. Katika halmashauri 184 zilizoko nchini Tanzania, Wizara ya Ardhi imeweza kufunga mfumo kwa 10.6% tu. Kwenye bajeti yake ya mwisho ilisema kwamba mpaka kufika mwaka 2024 ingekuwa imefunga mifumo kwenye halmashauri zote. Naona suala hili linakwenda taratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini TANESCO wanaleta bili mkononi? Kwa nini Wizara ya Maji imeweza kufunga mfumo, na tunapata bili kwenye simu zetu? Kwa nini Wizara ya Ardhi mnashindwa kufunga mfumo wananchi wapate bili kwenye simu zao? (Makofi)
(Hapa, kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ...
SPIKA: Kengele imeshagonga.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, haya ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)