Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ambao zipo Mezani kwetu. Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza Wenyeviti wote wawili kwa uwasilishaji wao mahiri. Pia nawapongeza Wajumbe wa Kamati hizi mbili, yaani ile ya Utawala, Katiba na Sheria na Wajumbe wa Sheria Ndogo kwa kazi zao ambazo zimewasilishwa hapa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni taarifa za kina na ambazo zinaonesha ni jinsi gani Kamati hizo zipo makini na zimetuletea taarifa ambazo zina mambo mengi ambayo yanatuonesha kwa kipindi cha muda huo nini kimefanyika katika Kamati zetu hizi mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaanza mchango wangu naomba nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Nampongeza kwa sababu ya uchapakazi wake na kazi kubwa anayoifanya katika kutuletea maendeleo Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nampongeza kwa tuzo maalumu ambayo ameipata jana. Hii inaonesha ni jinsi gani amewekeza katika sekta ya afya. Kwa hiyo, hongera sana Mheshimiwa Rais, hongerani Waheshimiwa Mawaziri kwa kazi nzuri ya kumsaidia Mheshimiwa Rais, pia, hongerani watendaji wote wa Wizara zote ambao wanamsaidia Mheshimiwa Rais katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa tukio ambalo linaendelea sasa hivi kule uwanjani kwa kuteuliwa kwake kuwa Mgombe wa Kiti cha Urais wa Chama chetu pendwa, Chama cha Mapinduzi. Siyo hivyo tu, nampongeza Balozi, Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, pia na Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi kwa kuteuliwa kupeperusha bendera kule Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matarajio yetu kwamba leo wametambulishwa, Wana-CCM, tutaingia kazini kutafuta kura na ushindi mkubwa utapatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyowasilishwa na Mwenyekiti wetu, kwamba malengo makuu ya kutungwa kwa Sheria Ndogo ni kuweka mazingira wezeshi ili Sheria Mama ziweze kutekelezwa, lakini kama ilivyowasilishwa pale kwenye taarifa, kuna sheria ndogo nyingine zimekuja na masharti ambayo hayana uhalisia, hivyo kusababisha mambo makubwa mawili: Kwanza, kutokutekelezeka kwa Sheria Mama, na pia, kuzua kero katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tumetoa azimio pale kwamba masharti yote ambayo hayana uhalisia, yarekebishwe ili yaendane na malengo ya kuanzishwa kwa kanuni hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nami nitajikita katika maeneo matatu; Sheria Ndogo tatu. Sheria ya kwanza ni kama ilivyosomwa pale; Sheria Ndogo ya Ushuru wa Madini ya Ujenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambayo ni GN na, 814 ya mwaka 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa wakati wanatafsiri hii Sheria ya Madini ya Ujenzi, wamejumuisha na tofali kwamba ni sehemu ya madini ya ujenzi. Sasa hii inaweza kuleta kero kwa watendaji ambao watatafsiri kwa jumla matumizi ya kifungu hiki kwamba, watakamata na tofali ambazo hazihusiki kama madini ya ujenzi kwa sababu, kimsingi siyo aina zote za tofali ni aina ya madini ya ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tofali zile za udongo, unaweza ukajumuisha kwenye madini ya ujenzi, lakini zile tofali nyingine siyo za madini ya ujenzi. Kwa hiyo, hii ni changamoto ambayo tumeibaini na inaweza kuleta kero wakati watumishi wa halmashauri wanatekeleza hiyo kanuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni nyingine ni Kanuni ya Bima ya Afya kwa wote ile GN namba 809 Kanuni Namba 24. Hapa inaweka ukomo wa wanachama katika Skimu ya Bima ya Afya. Inasema, mwanachama asipochangia kwa miezi mitatu, basi huduma itasitishwa. Sasa, huyu ni mtumishi wa umma na mtumishi wa umma hachangii kwa kupeleka yeye mwenyewe kwenye skimu. Wajibu wa mtumishi wa umma amepewa mwajiri wake kwamba lazima awasilishe kila mwezi. Sasa kwa kifungu hiki ataumizwa mtumishi wa umma ilhali yeye sio wajibu wake kupeleka kila mwezi, ni mwajiri wake ambaye anatakiwa apeleke kila mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa vifungu kama hivi vinasababisha kero kwa watumishi, vinasababisha malalamiko kwa watumishi na hivyo kusababisha watu kutoona umuhimu wa sheria iliyoanzishwa wakati kuna kifungu hiki ambacho hakina uhalisia.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana kwenye Kamati yetu tumependekeza kwamba vifungu kama hivi virekebishwe kuleta uhalisia. Kifungu hiki hakina uhalisia kwa sababu mtumishi hapeleki fedha kwenye skimu kila mwezi. Mtumishi wa umma anapeleka kwa kukatwa mshahara wake na mwajiri wake ndiyo anayetakiwa kupeleka kwenye mfuko kila mwezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunatarajia vifungu kama hivi vitarekebishwa, ili Sheria Ndogo zitimize lengo lake la msingi kurahisisha utekelezaji wa sheria mama.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nimetoa mifano miwili tu ya hizi Sheria Ndogo ambazo zimetungwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nachukua nafasi hii kuipongeza Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, chini ya Mheshimiwa Mchengerwa. Kwa kweli, kuna kazi kubwa sana wameifanya. Hapo zamani kulikuwa na dosari nyingi sana zinaonekana katika Sheria Ndogo ambazo zinawasilishwa katika Kamati yetu, lakini sasa hivi kuna makosa machache sana kama haya ambayo yanaweza kurekebishika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)