Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Dr. Paulina Daniel Nahato

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. DKT. PAULINA D. NAHATO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami nichangie katika mawasilisho mawili yaliyowasilishwa na Wenyeviti wa Kamati za Sheria. Awali ya yote, napenda kuwapongeza sana, wamewasilisha vizuri na kwa umahiri mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami pia, nichukue nafasi ya kumpongeza Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupendekezwa kuwa Mgombea wa Urais akiwa pamoja na Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uhakika tunategemea Chama cha Mapinduzi kitashinda uchaguzi wa mwaka huu kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, nawapongeza sana. Vilevile nachukua nafasi hii kumpongeza Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson, kwa jinsi anavyoendesha Bunge letu pamoja na Naibu Spika kwa jinsi pia, unavyoendesha Bunge kwa umahiri mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika Sheria Ndogo kama tulivyoziona katika Kamati yetu. Sheria Ndogo dhumuni lake ni kutoa ufafanuzi wa utekelezaji wa masharti yaliyowekwa na Sheria ya Bunge. Hata hivyo, wakati tukiendelea na uchambuzi katika sheria zetu, tulibaini dosari mbalimbali na mojawapo ambayo mimi nitaeleza ni kasoro za uandishi katika sheria hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano tu wa sheria ambazo zimeonesha makosa ya kiuandishi yaliyojitokeza wakati tunachambua katika Kamati yetu ya Sheria Ndogo. Moja ni Tangazo la Serikali Na. 778 la Mwaka 2024, Kifungu cha 11. Pia kuna Tangazo la Serikali Na. 814 la Mwaka 2024, Kifungu cha 12 na Tangazo la Serikali Na. 263 la Mwaka 2024, Kifungu cha Nne, pamoja na Tangazo la Serikali 366 la Mwaka 2024, Kanuni ya 8C. Hizo ni baadhi tu ya sheria ambazo tumeona zina makosa ya kiuandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa makosa haya ya kiuandishi unaweza kukwamisha lengo la Bunge kuhusu utekelezaji wa sheria zilizotungwa na Bunge. Makosa hayo yanaweza kupotosha lile jambo ambalo lilikusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, uandishi ni taaluma ambayo inatakiwa izingatiwe sana, kwani neno linapokosewa linaleta maana tofauti. Kwa hiyo, katika Kamati yetu tuligundua kwamba, makosa hayo ya sheria ambayo hayaendani na misingi yanaweza kuathiri maana iliyokusudiwa katika Sheria Ndogo inayohusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inaweza kuwa ni sehemu ya chanzo cha Sheria Ndogo kushindwa kufanikisha madhumuni ya sheria pale ambapo sheria hizo zimekuja katika Kamati zikiwa na makosa ya kiuandishi. Hivyo basi, Kamati inashauri mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, moja inasisitiza mamlaka zinazokabidhiwa madaraka ya kutunga Sheria Ndogo ziwe makini katika uandishi. Makosa ambayo hayana sababu kuwepo katika sheria hiyo yarekebishwe, ili yanapokuja katika Kamati basi tusitumie muda mrefu kukosoa uandishi ambao unajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kamati pia tulipendekeza zirekebishwe dosari hizo ili ziweze kuendana na sheria ambazo zinategemewa kutumika katika nchi yetu na hasa pale Bunge linapokuwa limetunga sheria zinapoenda kutumika zikiwa na dosari za uandishi zinapotosha maana ambayo ilitegemewa. Kwa kuondoa makosa hayo ya kiuandishi, basi sheria hizi zitakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Wizara zote ambazo walikubaliana na Kamati na kwenda kurekebisha makosa au dosari zote za uandishi zilizojitokeza na hivyo, sasa sheria zetu zimesomeka vizuri zikiwa na uandishi ulio mzuri. Ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii.