Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Benaya Liuka Kapinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbinga Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nianze kwa kuunga mkono hoja, lakini pia, niwapongeze Wenyeviti waliotuwasilishia taarifa hapa, wamewasilisha kwa weledi sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee pale ambapo Mheshimiwa Dkt. Chamuriho amekomea, na hasa, eneo hili la majedwali. Kabla sijaendelea, kwa ujumla wake tu niipongeze Serikali kwa namna inavyofanya kazi nzuri ya utunzi wa sheria hizi, hasa hasa hizi Sheria Ndogo. Kwamba, ni jukumu ambalo wamekasimiwa, lakini wamelifanya kwa weledi mkubwa, hasa katika kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande huu wa majedwali ambao Mheshimiwa Dkt. Chamuriho alikua anauongelea, kuna baadhi ya maeneo ambapo ukamilifu wa sheria hizi ndogo na sheria kwa ujumla ni pamoja na majedwali yaliyopo mle. Ili sheria hizi ziweze kutumika vizuri ni pamoja na uandishi mzuri wa majedwali haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, jedwali linalohusu Sheria Ndogo ya Ada na Ushuru ya Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Tangazo la Serikali 811 la Mwaka 2024, katika Sehemu J, jedwali la kwanza ambalo linahusu Ushuru wa Kusafirisha Mifugo ya Samaki, hata Mwenyekiti hapa amelieleza vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kipengele kile cha 18B, ambacho kinatoza ushuru wa shilingi 300/= kwa ndoo ya lita 20 ya samaki, lakini hawajatuambia ni kiasi gani kitatozwa kwa vipimo vya chini ya ndoo ya lita 20. Kutokuwepo kwa kiasi hicho kwa kipimo hicho na kiasi hicho kinaleta mkanganyiko kwa vipimo vya chini ya ndoo ya lita 20.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wahusika wanapotunga majedwali haya, ni vizuri sana wakaweka vizuri chini ya kipimo kile kwa sababu, wananchi wengine siyo lazima wabebe samaki wa ujazo ule, kwa maana ya ndoo ya lita 20. Je, tukimkuta mtu amebeba ndoo ya lita 10, huyo atatozwa shilingi ngapi? Ukikuta wasimamizi wasio wazuri, basi wanaweza wakakanganya hapa, ikaleta kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Sheria ya Ada ya Ushuru wa Mazao ya Uvuvi, Halmashauri ya Kalambo, Tangazo la Serikali Na. 815, Jedwali la tatu, kuhusu kibali cha kusafirisha mazao ya uvuvi; jedwali linaweka sharti la kwamba, kila anayesafirisha mazao hayo ya uvuvi, ikiwemo hata ya kutumia nyumbani, awe na kibali. Sasa tunajiuliza, anayeenda kutumia samaki nyumbani, atakuwa na kibali cha kusafirisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, uhalisia ni kwamba siyo kweli, hawa watu watasafirisha kwa kawaida tu. Kwa hiyo, watunzi wa sheria wanapotunga haya majedwali na kuweka hizi sheria lazima wawe wazi kupunguza hii mikanganyiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ningeenda eneo lile ambapo sheria hizi ndogo zinakinzana ama zinaonekana kukinzana na Katiba. Kwa mfano, Sheria Ndogo ya Udhibiti na Usimamizi wa Mifugo ya Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga. Tangazo la Serikali Na. 266 la Mwaka 2024, Kifungu Kidogo cha Tano, kinaweka wajibu kwa mfugaji, kinaweka wajibu kwa wafugaji kwamba, mfugaji wa eneo husika hapaswi kumkaribisha mfugaji mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba, mfugaji wa pale Shinyanga hapaswi kumkaribisha mfugaji anayetoka eneo lingine, lakini wako na nia fulani. Wao kwenye Kanuni hii hawajaweka sharti kwamba, ni mfugaji yupi ambaye hapaswi kukaribishwa. Mfugaji mwenyewe tu hapaswi kumtembelea mfugaji mwenzake akajifunza ama mfugaji mwenye mifugo ndio hapaswi kukaribishwa? Lakini inawezekana kabisa wao walilenga mfugaji mwenye mifugo ndio hapaswi kukaribishwa na mfugaji aliyepo kwenye Manispaa ya Shinyanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kuweka masharti ya namna hii yanapingana kabisa na Katiba ambayo inaruhusu watu kutembea kutoka eneo moja. Watu wana haki ya kutoka eneo moja kwenda eneo lingine na hivyo, kama wana nia ya kukataza wafugaji na mifugo yao, basi wangeweka wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la kanuni ambalo pia, linapingana na Katiba ni Kanuni ya Nidhamu kwa Wanafunzi, ya Tangazo la Serikali 365, Kifungu cha 23 (3), ambacho kinaruhusu shauri kusikilizwa pasipo kuwepo kwa mtuhumiwa. Kifungu hiki kinapingana kabisa na Ibara ya 13B, Kifungu Kidogo cha A, ambacho kinataka pale ambapo maamuzi yanayofanyika juu ya mtu, awepo pale aweze kusikilizwa, lakini kanuni hii inasema shauri hili linaweza kusikilizwa pasipo kuwepo huyo mtuhumiwa, moja kwa moja inapingana na Ibara ya Katiba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono maazimio yote. Ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)