Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa hii kuchangia Taarifa ya Kamati hizi, naipongeza Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi ambayo imefanyika na inaendelea kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi napenda kuchangia suala la haki kwa watu wetu hususan Mahakama za Mwanzo. Naishukuru Serikali kwa kipindi hiki kwa maboresho makubwa ambayo yamefanyika na yanaendelea kufanyika kuboresha Mahakama zetu za Mwanzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye taarifa iliyowasilishwa na Kamati yangu ya Utawala, Katiba na Sheria, kipengele cha tatu, kipengele cha kwanza, namba moja, idadi ya majengo ambayo yamejengwa Mahakama za Mwanzo na tunaipongeza Serikali. Inasema mpaka Januari yalikuwepo majengo 935 ya Mahakama za Mwanzo, na kati ya hayo 191 yapo kwenye hatua nzuri ya ujenzi. Hii ni kazi kubwa ambayo imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia wingi wa watu wetu wanatumia hizi Mahakama za Mwanzo katika hatua zao za mwanzo za kutafuta haki, lakini hizi Mahakama za Mwanzo narejea kauli ya Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Siku ya Sheria juzi aliwaasa Majaji na Mahakimu wasiwe miungu watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara ya Sheria na Katiba ikazichunguze na kumulika jicho kwenye Mahakama za Mwanzo katika hatua za utoaji wa haki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili ipo Kamati ya Maadili ya kuwawajibisha hao Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo, lakini jukumu hili linaonekana Wakuu wa Wilaya wengi hawalifahamu au hawalifanyii kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali kupitia Wizara husika wakaandae waraka mahsusi kwa Wakuu wetu wa Wilaya, wakawachunguze Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo wote, pale wanapotoa haki, ili wananchi wetu wapate haki yao kulingana na makosa; au kesi wanazozipeleka Mahakamani, kwani kule kuna shida kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imeongelea uboreshaji wa sheria za nchi hii. Kwenye hili tunayo Tume ya Kurekebisha Sheria, imetajwa kwenye wasilisho la Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria. Tume hii inalenga kuboresha sheria zetu, lakini kazi ambayo inafanywa na hii Tume ni ndogo na tatizo ni ukosefu na ufinyu wa bajeti wanayopewa. Napendekeza na kushauri tunapokwenda kwenye bajeti, kwani tume hii ni muhimu sana katika kuboresha sheria zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa tunazo sheria nyingi zimepitwa na wakati, sasa, ni wajibu wa hii tume kufanya marejeo ya mara kwa mara kuhakikisha kwamba, sheria zetu zinaendana na wakati, lakini hawawezi kufanya hii kazi kama bajeti yao na mafungu yao hayawezi kuwaruhusu na hawawezi kuwa na watumishi ambao wanakidhi viwango. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napendekeza, kushauri na ninakubaliana na taarifa ya Kamati yangu kwamba tume hii iangaliwe hasa tunapokwenda kwenye kipindi cha Bajeti ya Serikali Kuu, tuwapatie fedha ya kutosha ili waweze kufanya kazi ya kurekebisha sheria zetu ziende na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwenye hili tena, kwa kweli yamefanyika maboresho makubwa sana kwenye Mahakama zetu. Sisi ambao tumetoka kwenye Mahakama, enzi za nyuma Mahakama nyingi kusema kweli kuingia ilikuwa ni shida, lakini ukiangalia sasa majengo mengi hasa Mahakama Kuu na Rufaa kweli kazi kubwa imefanyika na inaonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naipongeza Serikali kwa kuja na Mfumo wa TEHAMA hasa hii ambayo inaitwa Government of Tanzania eCase Management System, imerahisisha na kupunguza muda wa ku-file kesi Mahakamani na kufuatilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa tumezoea ukienda kwenye corridor mnaitwa na wakati mwingine hata sauti huisikii, lakini kwa sasa kwa mfumo uliopo kwa kweli asiyeona haambiwi tazama. Kazi imefanyika na naipongeza Serikali, naomba iendelee kufanya maboresho hasa kwenye sheria zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya sheria yanayofanyika yaingizwe kwenye sheria zetu haraka sana. Tunajikuta tuna sheria, lakini tuna viraka vingi ambavyo vipo nje ya sheria zenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali tunapofanya marejeo na marekebisho ya sheria, yale marekebisho yanayofanywa yaingizwe kwenye sheria mara moja ili watumiaji wa hizo sheria wasiwe wanababaika na wakati mwingine watumie sheria ambazo zimesharekebishwa, wakati mwingine kupata yale marekebisho inachukua muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naipongeza Serikali kwa msaada wa kisheria ambao unatolewa kwa wananchi hasa wale ambao hawana uwezo wa kutafuta na kuwalipa Mawakili. Kazi kubwa imefanyika hasa kwa wananchi ambao kipato chao hakiwaruhusu kuwatafuta wanasheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua wote hapa kumtafuta mwanasheria ni ghali sana, wananchi wengi wamekuwa wakipoteza haki zao kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kuwatafuta na kuwalipa Mawakili wa kujitegemea. Kwa msaada huu unaoendelea wa kisheria ukiunganishwa na Samia Legal Aid nina uhakika wananchi wetu watapata haki zao ambazo zilikuwa zinapotea kwa sababu ya kutoweza kuzilipia kwa mawakili wa kujitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono, na ninashukuru sana kwa kunipatia fursa hii. (Makofi)