Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kusema Bungeni siku ya leo. Nianze kwanza kwa kuunga mkono maazimio yaliyoletwa mbele ya Bunge letu Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze kuchangia kwenye eneo la Kanuni za Bima ya Afya kwa Watu Wote za Mwaka 2024. Moja kwa moja, naomba nichangie kwenye Kifungu cha 16 cha Kanuni hizo. Kwa wanaofuatilia, wanaweza kupenda kufanya rejea ya sheria mama (Sheria ya Bima ya Afya kwa Watu Wote ya Mwaka 2023) hususan kwa kuzingatia Kifungu cha Tano, Kifungu cha 25 na Kifungu cha 35 cha sheria mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, vifungu vyote hivi vinahusiana moja kwa moja na bima ya afya kwa watu wasio na uwezo. Vifungu hivyo kwa sababu ya muda, sitavirejea vyote, lakini vinahusisha mambo yanayohusiana na namna ya kuwatambua na kuwahudumia watu wasio na uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maelekezo yanayotolewa na sheria mama, ni kwamba zitaundwa kanuni kwenye kile Kifungu cha 35 cha sheria mama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niliteuliwa na Mheshimiwa Spika kwenda kuungana na Kamati ya Sheria Ndogo ili kuzipitia kanuni hizo. Kwa hiyo, tulipoenda kukaa na Kamati ile tulibaini upungufu mwingi sana ambao unaelekezwa na sheria, lakini haujawekwa kwenye kanuni ambazo zililetwa tuzifanyie uchambuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, maeneo ambayo hayakufanyiwa kazi ipasavyo na Waziri aliyetunga hizo, kanuni mojawapo ni eneo la Kanuni ya 16 ambalo linahusiana na watu wasio na uwezo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ninazungumza haya na ninapenda tuzingatie Executive Order iliyotolewa na Rais wa Marekani Januari 20, ambapo kwa kiasi kikubwa unaona kuna shift ya health funding ambayo itatokea kwenye health system duniani, kwa sababu Marekani anajiondoa kwenye kuchangia baadhi ya huduma muhimu ambazo na sisi tulikuwa wafaidika wa huduma hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Executive Order, ile Rais wa Marekeni amesitisha kwa miezi mitatu (siku 90) kwamba tusipate mchango wa PEPFAR hapa Tanzania. PEPFAR inahudumia waathirika wa virusi vya UKIMWI kuanzia matibabu, orphans and vulnerable children na huduma za VCT za kupima virusi vya UKIMWI, wapatao 1.5 million ambao ni Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, hii inatosha kuwa-wakeup call hususan kwa sisi wawakilishi wa Tanzania hapa Bungeni kuanza kufikiria kuwekeza zaidi kwenye mfumo wa afya ambao utatutosheleza kuwahudumia Watanzania zaidi ya milioni 61.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tishio hili la kusitisha huduma kwa miezi mitatu kwanza wakati wanafanya uchambuzi hatujui baada ya miezi mitatu nini kitatokea? Vipi wakiamua kusitisha indefinitely. Katika hiki kipindi cha miezi mitatu Watanzania wanaopata dawa za kufubaza VVU zaidi wa milioni 1.5 wanahudumiwaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwa unazungumza Bungeni katika kipindi kama hiki halafu ukazitazama zile sheria zetu; Sheria ya Bima ya Afya, Sheria ya Bima pamoja na Kanuni za Bima ya Afya kwa Watu Wote, unaona wazi kabisa kwamba bado hatujaweka commitment ya kutosha ya jinsi gani tutatoa huduma za afya kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kwamba ili huduma za Bima ya Afya ziweze kufanikiwa, ni lazima kile Kifungu cha Tano cha kwenye sheria mama ambacho kimesitishwa ukisoma kwenye kanuni na Tangazo la Serikali Namba 700A la Agosti 14, 2024, kwamba Kifungu cha Tano kisifanye kazi na vifungu vingine vingi. Kwa nini kinasitishwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, inasitishwa kwa sababu Kifungu kile cha Tano cha kwenye sheria mama kinaweka ulazima wa kila Mtanzania kuwa na Bima ya Afya ya aina mojawapo (mandatory enrollment) kwenye universal health insurance.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, kama hakuna mandatory enrollment, maana yake hakuna Bima ya Afya kwa sababu katika pillars za Bima ya Afya kunatakiwa kuwe kuna population coverage, service coverage, pia kunatakiwa kuwe na financial protection. Haya mambo yote katika mfumo ambao tumeutengeneza hapa Bungeni na alioenda kumalizia Mheshimiwa Waziri hayaonekani, maana yake ni kwamba threat ya Watanzania kukosa huduma bora za afya ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu ya muda, napenda kupendekeza Serikali ikazifanyie marekebisho upya hizi kanuni ili waweke michango ya uhakika kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa Watu Wote, hususan watu wasio na uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama takwimu za NBS, wapo takribani 26.4% ambao kwa idadi, kwa kuzingatia Sensa ya Mwaka 2022 wanafika takribani Watanzania milioni 16.3. Kama utawachangia tu takribani shilingi 150,000/= kila mmoja kwa mwaka, maana yake Serikali inatakiwa iwe na bajeti isiyopungua shilingi trilioni 2.44 kwa ajili ya kuwakatia bima 26.4% tu ya Watanzania, jambo ambalo halionekani, na michango hiyo haijawekwa explicit kwenye hizi kanuni ambalo lilipaswa kuwa takwa la sheria mama ambayo linawekwa katika Kifungu cha 35 cha Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba mapendekezo hayo ya ushauri wangu yaende yakafanyiwe kazi ili mfumo wetu wa Bima ya Afya wa Watu Wote uweze kutimia. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)