Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024 Na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2024

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupata nafasi hii. Awali ya yote, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote pamoja na taasisi zao ambao tunafanya nao kazi kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria. Wamekuwa na ushirikiano mzuri sana na tunawapongeza na kuwashukuru kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono Maazimio ya Kamati zote mbili, lakini nitazungumzia upande wa Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa za taasisi mbalimbali za Kimataifa zinaonesha kwamba, hali ya uchumi wa nchi yetu unakua. Ukiacha hizo taarifa, hata ukiangalia kwa macho unaona vitu viwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, unaona kweli hali ya uchumi wetu inakwenda vizuri sana; na cha pili unaona kwamba bado tunao uwezo mkubwa sana wa kuendelea kukuza uchumi wetu, hasa kwenye uzalishaji wa mazao ya chakula na hivyo kutufanya tujitosheleze kwa chakula na kuweza kuuza nje; pia mazao ya biashara ambayo ukiacha kuuza pia ni malighafi. Kwa hiyo, tuna potential kubwa ya kukuza sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo mito mingi, kwa hiyo, tuna uwezo wa kuzalisha umeme zaidi. Kwa hiyo, kwa maneno mengine ni kwamba nchi yetu ipo katika tipping point, yaani mazingira ambayo uchumi wake unaweza ukakua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, katika mazingira kama hayo ni lazima suala la utawala wa sheria litamalaki. Utawala wa sheria kama wengi mnavyofahamu historia yake kwenye Karne ya sita, saba, na nane huko India ulianza kwanza kwa kuwawajibisha watawala kwamba, Mfalme ambaye hawezi kuwalinda watu wake alikuwa anapigwa mawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakaenda, baadaye wakaja watu wenye akili zaidi (philosophers) wakasema haiwezekani kuwajibisha upande mmoja, lazima kuwajibisha pande zote mbili kwamba, lazima kuwe na kitu juu yetu ambacho kinatuongoza. Ndiyo mambo ya sheria yakaanza kutungwa na watu wote wawe sawa mbele ya sheria na waziheshimu sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo wazi kwamba kukosekana kwa utawala wa sheria kumevunja heshima ya nchi nyingi sana hasa za dunia ya tatu, kumewaletea vurugu nyingi sana. Kwa hiyo, ni jambo ambalo kwa kweli ni la msingi sana, ndiyo maana katika hatua hii ni lazima kwa dhati kabisa tumpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa champion kwenye eno hili la utawala wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamekuwa na uwekezaji mkubwa sana kwenye sekta ya sheria katika kipindi hiki kama alivyochangia rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Kikoyo, kwa sisi ambao tumekaa kwenye sekta hii muda mrefu tunaona kabisa kwamba, tulikotoka kulikuwaje na tulipo ni wapi, na mtumaini kule mbele ambako tunaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais pia amekuwa Mwalimu kwenye eneo hili, kwanza kwa kuanzisha 4R ili tuweze kutekeleza na kuweza kufaidi huu uwekezaji kwenye sekta ya sheria. Pia, suala zima la hii Tume ya Hakijinai pamoja na suala la Legal Aid ambalo sasa hivi linaendelea. Haya maeneo yote matatu ni muhimu katika kuvuna faida zinazotokana na uwekezaji mkubwa ambao umefanyika kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi sasa inabakia kwa watendaji na wataalam kufanya kazi yao kwa weledi bila uwoga ilimradi tu wanafuata sheria na kumshauri Mheshimiwa Rais kwa dhati katika maeneo yanayohusiana na sheria na masuala ya utoaji haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika nchi kama yetu ambayo tuna Katiba inayotambua haki za msingi za binadamu na pia tuna ile sheria ya kukazia zile haki (Basic Rights, Duty and Enforcement Act) Sura ya Tatu, Sheria ambayo inatuwezesha sasa kukaza zile haki ambazo zipo ndani ya ule mkataba wa haki za binadamu ili tuweze kuzipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mazingira kama hayo, hakuna sababu ya mtu kunyimwa haki yake iliyoko ndani ya sheria. Ni masuala tu ya utekelezaji, wakati mwingine unakuwa dhaifu, lakini kwa kweli ikikosekana haki, tusiilaumu Serikali wala sheria, tulaumu watendaji wanaohusika na maeneo hayo kwa sababu sheria zipo na zinatoa kila fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna sababu ya kuchelewesha au kunyima dhamana kwa kosa ambalo lina dhamana, kwa sababu hata kama sheria unayo-deal nayo haitaki, basi Katiba ipo na imeruhusu, na Katiba ndiyo sheria mama, hakuna asiyejua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siku zote nasema, sekta ya sheria Tanzania ina uwezo wa kukua na kutoa haki kwa kila mtu, kwa sababu ukishaanza na Katiba na sheria ku-enforce zile haki zilizoko ndani ya Katiba, basi hakuna sababu ya kukosa haki yoyote ndani ya nchi yetu hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mafanikio haya makubwa ambayo tunayo, lakini tunahitaji pia kuendelea kuwekeza hasa katika Ofisi ya DPP kwa sababu ndiyo custodian wa Hakijinai.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Hakijinai zinawahusu watu wadogo, ndizo ambazo zikikosekana, nchi inakuwa na vurugu nyingi sana. Kwa hiyo, tuwekeze zaidi Ofisi ya DPP, bajeti pamoja na watumishi na training.

Mheshmiwa Naibu Spika, pia, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo ndiyo inalinda haki zetu zote za mikataba na uwekezaji na sasa hivi dunia inakoelekea, lazima ofisi ile iweze kuwa na viwango vya Kimataifa. Kwa hiyo, nawatia moyo kwamba walete bajeti ya kutosha, nasi Wabunge tuipitishe, ili waweze kufanya kazi vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo niwaalike Jimboni kwangu Mwanga, tunahitaji Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya DPP na Ofisi ya TAKUKURU. Uwanja tunao, waweke kwenye bajeti waje pale tujenge. Mheshimiwa Simbachawene amenitazama, nina uhakika anataka kuleta Ofisi ya TAKUKURU pale kuijenga. Karibu sana Mheshimiwa Waziri pamoja na wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile kengele imelia, nimalizie na suala moja tu la madawa ya kulevya. Naipongeza sana Mamlaka ya Udhibiti wa Madawa ya Kulevya, wanafanya kazi nzuri sana na kila mtu anaona, lakini vita hii ni kubwa sana. Kila dunia inavyoendelea, population inavyokua na maendeleo yanavyoongezeka, hii vita inazidi kuwa kubwa. Kwa bahati mbaya sana inaendana na hii vita ya mambo ya ushoga.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba, lazima tu-integrate hili suala kuanzia kwenye mitaala yetu ya shule za msingi. Mtoto anapoingia Darasa la Kwanza afundishwe ubaya wa madawa ya kulevya, afundishwe ubaya wa ushoga, afundishwe ubaya wa ulevi wa kupindukia. Akienda Kanisani, akienda kwenye Sunday School, kwenye Madrasa nako afundishwe hivyo hivyo; na wakirudi nyumbani kwenye familia tutilie mkazo hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii vita inakwenda kuwa personal, yaani haitakuwa tena kutegemea Serikali. Itategemea kila mmoja amefundishwa nini na anakua kuelekea wapi? Tusitake kufikia hatua ambazo wenzetu huko nje wamefikia sasa hivi, mpaka Rais analazimika kutoa amri nyingi za kufuta vitu ambavyo vimeshajiingiza sana kwenye jamii kiasi kwamba vinakuwa shida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, machache yangu ni hayo. Naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)